Na Salim Said Salim
UTAWALA wa kifashisti na udikteta huwa na sura nyingi na nyingine huwa za kuvutia ili kuuhadaa umma (watawala huuona umma kama kundi la mabwege).
Madikteta huwa hawajali wala hawaheshimu haki za binadamu, sheria za kimataifa za utawala bora au utu wa mtu ,haki za mke au mume wala watoto, watu wenye ulemavu, vizuka au mayatima.
Kwao kusema uwongo, kutesa, kujeruhi au hata kuuwa ili kubaki madarakani ili wafurahi na waimbe “ Tunawatesa” ni mambo ya kawaida.
Hawa madikteka wanapozungumzia amani na utulivu basi ogopa kwani huwa ndio wapo jikoni wanalipika jungu la kukamata watu na kuwafungulia mashitaka bandia.
Wanapoamua kusisitiza umoja na mshikamano ndio huzusha kauli za kibaguzi kama za “Wapemba waende kwao” na kunyanyasa watu na kuwatangaza wale wanaowakosoa kuwa si raia wa nchi hii kama Tanzania ni mali yao wao peke yao kwa vile chama chao kipo madarakani iwe kwa kwa kura au kwa mbinde.
Ukweli ni kwamba utawala wa kiditeta ni wa kinyama zaidi kuliko wa wanyama wanaofugwa au waliopo kwenye mbuga za Jozani (Unguja), Manyarana na Serengeti (Bara).
Madikteta hutoa kauli za kutisha watu. Kwa mfano, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, aliwahi kusema katika mkutano wa hadhara mjini Unguja kwamba kuuwa hata watu 10 ili ubaki madarakani sio vibaya kwa sababu kiti cha Ikulu ni kitamu.
Ili kuonyesha yeye ni mwenye nguvu alikuwa akiuliza :” Mnaniona komandoo…?” waliokuwa wakimshabikia kwa kuvunja haki za binadamu hawakuacha kumshangilia komandoo..komandooo.
Masikini Salmin, alijisahau na hii leo watu wanajifanya hawamuoni na kujidai wamesahau kwamba alikuwepo Fulani aliyeitwa komandoo.
Katika nchi yenye utawala wa kidikteta watu husombwa na kupigwa na askari hata majumbani mwao na usiku na hupelekwa sehemu zisizojulikana kwa familia zao.
Hali kama hii ya kinyama nilielezea mara nyingi kuwa ilikuwa ya kawaida Zanzibar kwa zaidi ya miongo miwili baada ya Mapinduzi ya 1964 na kusababisha watu wengi kupotea na mpaka leo hapajaelezwa kilichowakuta.
Waliobahatika kuachiwa waliathirika kiafya kwa mateso waliyoyapata mafichoni kulikojulikana kwa kwa jina la “ Ba Mkwe” na hadithi zake mpaka leo zikisimuliwa husikitisha na kutisha.
Hapajatolewa taarifa mpaka leo ya kilichowakuta watu waliopelekwa kwa “ Ba-mkwe” na kupotea, lakini upo uthibitisho kuwa wameshaiaga dunia, lakini vipi walikufa (inaaminika waliuliwa) haijaelezwa.
Hata makaburi yao hayajulikani yalipo. Hii ni dhulma ambayo haitasahaulika na itabakia kuwa sehemu chafu ya historia ya Zanzibar.
Hofu ya watu kukamatwa ovyo ndio iliopelekea maelfu ya Wazanzibari kukimbilia Bara, nchi za jirani, Arabuni, Aisa, Ulaya, Asia, Marekani, Canada na hata Australia kutafuta maisha ya salama.
Kinachosikitisha ni kuona dalili za hali hii kujirudia Visiwani na kutanda wingu la hofu juu ya wa watu kukamatwa majumbani na kupotea. Watu wameanza kuulizana kama kinachoendelea Visiwani ni historia kujirudia?
Matokeo ya karibuni ya watu kukamatwa na kupelekwa mafichoni yanashuhudiwa wakati Zanzibar ikijanasibu kuwa na utawala bota, lakini kinachoonekana ni udikteta na ujahili.
Kama Serikali imeamua kuirejesha sheria ya kidikteta ya kuweka watu kizuizini ieleleze ili umma ujue kuwa udikteta umerejea rasmi Visiwani.
Sio vibaya pia yakaandaliwa maandamano kuunga mkono uamuzi huu wa “ busara” wa serikali wa kurudia siasa za vitisho zinazosababisha watu kupotea.
Vinginevyo wanaohusika na kuweka watu kizuizini wawajibishwe kwani wanapandikiza mbegu za utawala wa kifashisti.
Katika baadhi ya nchi siku hizi, viongozi wa polisi na usalama wa taifa huwekwa gerezani na kuteswa kwa wiki mbili au tatu ili waone machungu ya mtu kuwekwa mafichoni na kuteswa.
Mfumo huu pia huwasaidia kuelewa namna familia zao zilivyopata tabu wakati walipokuwa hawajulikani walipo. Ni vizuri Zanzibar ikawa na mtindo huu ili kuwapa mafunzo ya vitendo wakuu wa vikosi vya ulinzi wanaopenda kuweka watu mafichoni.
Kuwanyamazia wanaoweka watu kizuizini na kutesa familia zao hakutoi tafsiri yoyote ile isipokuwa ya kwamba viongozi wa serikali wanaruhusu vitendo hivi.
Sheria zinataka mtu anayeshutumiwa na kosa la jinai akishakamatwa afikishwe mahakamani haraka na sio kuvumbikwa mafichoni kama embe mbichi inayongojea kuwiva ndio ipelekwe sokoni.
Ni muhimu umma kuelezwa watu waliokamatwa walipelekwa wapi na kosa lao ni lipi. Hili halifanyiki na wakubwa wa nchi wanajigamba ati wanaongoza kwa misingi ya uwazi. Hapana uwazi bali ni ujambazi.
Watu wanapokamatwa ovyo na kuwekwa kizuizini huzuka hofu na hili likifumbiwa macho litawafanya wanaotafuta mwanya wa kurejesha maovu Visiwani kuendelea na udhalimu wao.
Kama tahadhari isipochukuliwa mapema Zanzibar inaweza kujikuta na wimbi jingine la watu kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola .
Hapo tena panaweza kuzuka uvumi wa kila aina na watu kuishi kwa hofu na wengine kukimbia Zanzibar kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Wale wasioitakia mema Zanzibar nao hawatokuwa nyuma kuimba nyimbo za visiwa hivi havikaliki hivyo kukimbiza watalii wanaotegemewa kuingia fedha za kigeni.
Kulea uovu wa ina hii kutasababisha athari za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwani usalama wa watu unapokuwa shakani maendeleo nayo husuasua.
Ni vizuri viongozi wa nchi wakawa makini kupima hatari na athari za kuweka watu kizuizini zilizoanza kuiharibia sifa Zanzibar iliyonza kuonekana tena kuwa nchi inayojali haki za binadamu.
Siku hizi usalama wa nchi ni miongoni mwa vigezo vya uhusiano wa kimataifa. Nchi zinazoelezwa kuwa haziheshimu haki za binadamu hutengwa na kunyimwa misaada na hili lilifanyika kwa Zanzibar miaka ya nyuma.
Ni vizuri tukazuia mazingira yanayotoa taswira mbaya kwani nchi inayotengwa na Jumuiya ya kimatifa huathirika katika maendeleo.
Zanzibar lazima ijifunze kutokana na makosa iliyofanya miaka ya nyuma, kama ikirejea itapswa ijilaumu yenyewe badala ya kuelekeza lawama zake kwa washirika wa maendeleo wameiwekea ngumu wakati ni yenyewe ndio iliyoosabaisha kususwa.
Hapo tena kunung’unika na kutafuta mchawi hakutasaidia kwani wenyewe ndio wachawi.
Njia pekee ya salama kwa Zanzibar ni kuheshimu katiba na haki binaadamu na wanaoivunja katiba au kudhalilisha watu, wawe watoto wa Ba mkwe au wa Ba- Mjomba wasipewe nafasi ya kutamba.
Viongozi wa Zanzibar wakiruhusu watu wachache kutumia vibaya madaraka yao wataujuta kwa namna historia itavowazungumza baya kama inavyofanya kwa komandoo Salmin hivi sasa.
Udikteta na ufashisti, hata ukipewa visingizio gani vya kuuhalalisha, hauisaidii nchi yoyote ile kujenga demokrasia.
Nchi haiongozwi kwa mabavu na ukomandoo, bali kwa katiba na sheria. Mungu inusuru Zanzibar na wanaotaka kuvirejesha visiwa hivi katika utawala wa kinyama kama ulioshuhudiwa miaka ya nyuma.
Chanzo : Tanzania Daima