Na Salim Said Salim
MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP) wa Zanzibar, Ibrahim Mzee, hivi karibuni aliwataka watumishi wa umma kutokutoa maelezo ya uwongo kwa wajumbe wa Kamati za Baraza la Wawakilishi (BLW).
Akitoa mada juu ya kazi za kamati za BLW alisema watumishi wa serikali wanaotoa taarifa za uwongo, wanaokataa kujibu masuala au kuwatisha waliotoa maelezo kwa kamati wanaweza kushitakiwa kwani kufanya hivyo ni kutenda makosa ya jinai.
Tahadhari hii ni muhimu ukizingatia uzoefu uliopatikana kwa Wawakilishi kupewa taaarifa za ubabishaji, kuwekewa ngumu na kuwepo watumishi wanaokwepa kukutana na wajumbe wa kamati hizi wanapotakiwa kufanya hivyo.
Vile vile zipo taarifa za baadhi ya wakubwa kuwakomoa watumishi wanaotoboa siri za rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha au mali za serikali.
Hapana ubishi juu ya wajibu wa kikatiba wa kamati hizi katika kusimamia shughuli za serikali katika sekta mbalimbali na kuratibu mwenendo wa wizara, idara na taasisi zake.
Mara nyingi tumesikia Wawakilishi wakilalamikia jeuri, kibri na kejeli za baadhi ya watendaji wakuu wa serikali. Lakini kinachotokea ni kuonywa, kuombwa au kutahadharishwa kufanya hivyo sio vizuri na wanavunja sheria.
Hivyo, tujiulize kwa nini tuendelee kila siku na huu mtindo wa kuwabembeleza watu wanaotenda makosa ya jinai serikalini. Mbona hatuwabembelezi wanaoiba ndizi za mkulima au maandazi ya Mama Ntilie?
Kwa kweli tabia ya kubembelezana kama afanyavyo mama kwa mtoto wake mchanga imezoeleka na kupelekea watumishi sugu kudeka kama wafanyavyo watoto kwa wazazi wanaoonyesha.
Kinachohitajika ni kwa sheria kuchukua mkondo wake na sio kubembelezana. Hii ndio njia pekee itakayotoa fundisho kwa wengine wanaozuia kamati hizi kufanya kazi zake kama ilivyoanishwa kisheria.
Kama hili halitafanyika tutaendelea kuwa na Kamati za Baraza ambazo sio butu tu bali pia ni kibogoyo, yaani haziwezi kukata wala kuwatafuna wafanyakazi wa serikali ambao hawaitendei haki jamii wanayotarajiwa kuitumikia.
Hata hivyo, Wawakilishi nao wanapaswa kuoyesha mfano mzuri wa uadilifu wa kutoa taarifa za kweli wanapochangia hoja na masuala mbalimbali katika vikao vya Baraza la Wawakilishi.
Haitakuwa haki kuwataka watumishi wa serikali wasitoe taarifa za uwongo kwa Wawakilishi wakati Wawakilishi nao hawatoi taarifa za ukweli wanaposhiriki katika mijadala ya vikao vya bajeti au vile vinavyojadili miswada ya sheria au hoja mbalimbali.
Kwa kiasi fulani wananchi wengi wamekuwa na mashaka na uadilifu wa baadhi ya Wawakilishi wakati wanapochangia katika Baraza.
Ukifuatilia vikao vya Baraza na hata Bunge la Muungano, iwe vya bajeti au vingine, utawasikia hawa Waheshimiwa wakiunga mkono au kukataa hoja mia kwa mia.
Wengine huenda masafa ya mbali zaidi na kusema wanaunga mkono kwa asilimi 200 kwa niaba ya wananchi waliowachagua katika majimbo ya uchaguzi.
Hapana ubishi kama tunataka kuwa wakweli, kama DPP anavyotaka wawe watumishi wa serikali, kuwa baadhi ya kauli za Wawakilishi wanapotoa matamshi yao ya kuwa ni kwa niaba ya wananchi waliowachagua hayana ukweli, bali ni usanii uliozoeleka.
Ni kawaida akisimama Mwakilishi na kudai anazungumza kwa niaba ya watu katika jimbo lake, wenzake na hasa wa chama chake, humshangilia ili na wao watakapofanya watashangiliwa.
Ukichunguza utaona ni kawaida kwa Wakilishi kuwasilisha maoni yao binafsi katika Baraza na kudai walifanya hivyo kwa niaba ya wapiga kura katika majimbo yao.
Hii sio haki na ninaweza kusema kwa kiasi kikubwa ni unafiki kwa sababu sio kawaida kwa Wawakilishi kuitisha vikao majimboni ili kukusanya maoni na ushauri juu ya kipi awakilishe akizungumze katika Baraza au kupata ushauri kwa bajeti au miswada ya sheria mbali mbali.
Mimi binafsi naishi katika eneo moja kwa karibu miaka 20 sasa na sijawahi kuarifiwa au kusikia Mwakilishi au mbunge amefanya kikao cha aina hiyo.
Kinachofanyika ni kungojea uchaguzi ukikaribia, mwakilishi au mbunge kuwa na mkutano na kuhutubia kama mwalimu wa darasa la imal.
Wananchi hutakiwa kusikiliza na kuitikia “ Amin” au kukaa kimya kama wanavyokuwa watu katika ibada misikitini na makanisani.
Hali hii ipo katika karibu majimbo yote, iwe Mwakilishi au mbunge wake ni kwa tiketi ya CUF au CCM. Huu ndio ukeli na wanaonuna kwa hili kusemwa shauri yao.
Lazima tuambizane ukweli kwani kudanganyana kunadumaza fikra. Hatuwezi kujenga demokrasia ya kweli na yenye mtandao wa kila mwananchi kujivunia kwa kujiona naye anashiriki kwa mwenendo tulionao wa wabunge na wawakilishi wetu kufanya kazi kwa niaba yetu bila ya kutusikiliza.
Ni vizuri kwa Ofisi ya Spika ikachukua hatua kuzuia udanganyifu na ubabaushaji unaofanywa na baadhi ya Wawakilishi wetu wanaodai kuzungumza kwa niaba ya wananchi wakati hawajakutana nao hata kuulizana hali.
Miongoni mwa njia za kuwabana Wawakilishi (hata wabunge) ni kupeleka ratiba ya vikao walivyofanya na kukutana na wananchi na kushauriana (sio kuwahutubia) katika majimbo yao.
Hii iwe pamoja na ripoti zenye ushahidi wa kutosha utakaoonyesha hawa waheshimiwa walizungumzia mada gani, lini, na ushauri waliopata kutoka kwa wananchi katika mikutano hiyo juu
ya kila suala linalofikishwa mbele ya Baraza kwa mjadala.
Kwa Wawakilishi waliopitia hivyo vinavyoitwa viti maamlum (lakini ukweli ni vya vyama) na wale wanaochaguliwa na Rais wanaweza kupata uhalali wa kuzungumza kwa niaba ya wananchi kama watakuwa na vikao na taasisi za kiraia au katika vyuo na sehemu za kazi.
Kwa sasa Wawakilishi hawa wapo tu na hungojea vikao ili wachangie na kupata posho na kinachoonekana ni kufanya kazi ya kuwakilisha mawazo yao na sio ya wananchi wa eneo lolote lile.
Hawa nao pia harakati zao za kukutana na wananchi ziratibiwe ili pawepo na uhalali wa kuitwa Wawakilishi wanaowakilisha maoni ya wananchi wa maeneo na sehemu mbali mbali za Visiwani.
Huu mtindo wa mwakilishi kuona yeye ndiye anayejua matatizo ya wananchi na wanataka nini kama vile wanazo mashine majumbani kwao za kusoma vilivyomo kwenye nyoyo na vichwa vya watu katika majimbo yao unafaa ukomeshwe haraka.
Wapo wanaokutana na watu wachache, lakini zaidi kutokana na ukaribu wa kifamilia au urafiki, ili kupata maoni. Ni vizuri kwa wigo huu kupanuliwa zaidi.
Wananchi wanayo mawazo mazuri ya kuisaidia serikali juu ya masuala mbali mbali au hata kufichua maovu yenye sura ya rushwa na ufisadi yanayoigharimu nchi mamilioni ya shilingi.
Fedha hizi zinazotafunwa na waroho wachache wasiokuwa na imani na nchi wala wanachi wenao wenye shida za maisha zingeweza kwa kiasi kikubwa kutumika kuimarisha huduma muhimu kama za maji safi na salama, shule na afya.
Lakini kwa bahati mbaya nafasi hiyo hawana na matumaini ya wahehimiwa hawa kutoa uwakilishi wa uhakika na wenye mawazo yenye kushirikisha wananchi waliopo katika majimbo yao ya uchaguzi kwa hali ilivyo hivi sasa ni mdogo.
Wakati ni huu wa kufanya mapinduzi na mageuzi juu ya namna ambavyo Wawakilishi na wabunge wetu wanavyofanya kazi. Tunachokitaka ni kuwakilisha umma na sio fikra zao.
Chanzo : Tanzania Daima