Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk akizungumza na Wamiliki wa Mahoteli pamoja Wenye kusambaza Bidhaa katika Mahoteli ili kutatua matatizo yao huko katika ukumbi wa Wizara ya Habari Zanzibar.
PICHA NA YUSSUF SIMAI-MAELEZO ZANZIBAR
Na Fatma Abdalla Mzee –Maelezo
Waziri wa Habari, Utalii,Utamaduni na Michezo Saidi Ali Mbarouk amewataka Wamiliki wa Mahoteli ya Kitalii Zanzibar wanaodaiwa na Wasambazaji wa Bidhaa katika Mahoteli kulipa Pesa zao ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Amesema kama Wamiliki hao watashindwa kuwalipa Wazawa hao ambao husambaza Bidhaa mbali mbali katika Mahoteli hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa Leseni zao.
Waziri Mbarouk ametoa uamuzi huo mara baada ya mazungumzo yake na Wasambazaji wa bidhaa yaliyofanyika katika Ofisi yake Kikwajuni mjini Unguja.
“Natoa Mwezi mmoja tu walipwe pesa zao na itapokuwa hawajalipwa wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo
kunyang’anywa leseni zao”alisisitiza Waziri Mbarouk.
Aidha Waziri Mbarouk ameeleza kuwa malengo ya Serikali ni kupunguza umasikini kwa wanachi wake wa Zanzibar na sio kuongeza umasikini kwa wananchi wake.
Amesema suala la kutowalipwa wasambazaji pesa kwa wakati ni njia moja ya kuongeza umasiki kitu ambacho kinapigwa vita nchini.
Ameeleza kuwa tabia kama hyo ikiachwa iendelee itarudisha nyuma juhudi za serikali,hivyo hatua za kinidhamu zinapaswa zichukuliwe kwa haraka sana.
Hata hivyo Waziri Waziri Mbarouk alishindwa kutaja Majina ya Hoteli zinazodaiwa kwa kuhofia kuwaharibia biashara Wamiliki wake kwa vile ni waekezaji halali.
Kwa upende wao Wasambazaji bidhaa wamesema Jumla ya Shilingi Bilioni moja zinadaiwa na wasambazaji wa bidhaa mbalimbali katika Mahoteli ya kitalii hapa Nchini.
kwa mujibu wa Wasambazaji hao wamedai kuwa Wamiliki wa hoteli Walikubaliana wapelekewe bidhaa ili kuendesha Hoteli zao jambo ambalo wamelifanya lakini wamekosa kulipwa pesa zao.
Wamesema Vikao mbalimbali vya kupata Suluhu la deni lao vimeshafanyika mara nyingi na kwamba wanachosubiri kwa sasa ni utekelezwaji wa agizo hilo la Waziri.
Miongoni mwa Bidhaa ambazo Wasambazaji hao huzipeleka katika Mahoteli ni pamoja na Matunda ikiwemo Matikiti na Maziwa.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR