Na Othman Khamis Ame, OMPR
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba shughuli na harakati zozote za maendeleo popote pale nchini lazima zianzwe na wananchi wenyewe huku viongozi wao wakiongeza nguvu katika harakati hizo.
Balozi Seif alisema hayo wakati akijibu hoja, changamoto pamoja na kero zinazowakabili wananchi wa Kijiji cha Kichungwani kiliopo Kusini mwa Kijiji Kinduni ndani ya Jimbo la Kitope Wilauya ya Kaskazini “ B “ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kero zinazowakabili Wananchi hao zinaweza kupungua au kuondoka kabisa iwapo ushiriki wa pande zote mbili utakamilika katika utekelezaji wa pamoja.
Alifahamisha kwamba juhudi za upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ndani ya kijiji hicho zimechukuliwa ndani ya kipindi chake cha uongozi cha miaka minane iliyopita.
Balozi Seif aliwaahidi wananchi hao kwamba katika kipindi kifupi kijacho atajitahidi kuona mipira ya maji safi inapatikana ili kusambaza katika mitaa ambayo hadi sasa bado haijafanikiwa kupata huduma hiyo muhimu.
Hata hivyo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope alionyesha masikitiko yake kutokana na baadhi ya watu wa kijiji hicho kuamua kuikata kwa makusudi mipira iliyotandazwa kusambazia maji katika kijiji hicho jambo ambalo linarejesha nyuma juhudi za Uongozi wa nJimbo hilo.
Akigusia suala la Bara bara itokayo Kinduni, kupitia Kichungwani hadi Kitope Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi hao kuitekeleza ahadi aliyopitoa kipindi kilichopita ya kuweka kifusi ili kupunguza mashimo yaliyomo ndani ya bara bara hiyo.
Alisema hatua ya awali ya matengenezo ya bara bara hiyo itaanza kwa kupitisha burdoza lakini akawaasa wananchi hao kuridhia mazao au mali zao wakati wa kupitisha burdoza hilo.
“ Maendeleo katika maeneo yetu hupatikana kwa ushirikiano wa pande zote mbili. Sisi Viongozi kwa kushirikiana na nyinyi Wananchi. Sasa wakati tunajiandaa na hili ile tabia ya baadhi ya watu kudai fidiaya migomba yao lazima wafikie pahali kuridhia ikiwa kama mchango wao wa kushiriki kwenye maendeleo hayo “. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia mradi wa umeme Balozi Seif alisema uongozi wa jimbo hilo umejaribu kufanya makisio kutoka kinduni hadi katika kijiji hicho yaliyoonyesha gharama kubwa ambazo juhudi za pamoja kati ya Wananchi, Viongozi na Washirika wa Maendeleo zitahitajika kufanywa kwa ubia.
Aliwahakikishia Wananchi hao wa Kichungwani kwamba yeye pamoja na Viongozi wenzake watakuwa mawakala wa kuomba nguvu kwa baadhi ya washirika wa maendeleo likiwemo shirika la Umeme Zanzibar ili kuona Wananchi wa Kijiji hicho wanafaidika na huduma hiyo muhimu katika maendeleo ya Jamii.
“ Bado umeme una gharama kubwa kwa makisio yetu kuutoa kinduni hadi Kichungwani. Tutalazimika kushirikiana pamoja na nyinyi wananchi mtapaswa kuingiza nguvu zenu ili tufanikishe kazi hiyo kwa ushirikiano “. Alisisitiza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.
Kuhusu tatizo la ajira kwa vijana walio wengi katika Kijiji hicho na hata baadhi ya maeneo mbali mbali hapa Nchini Balozi Seif akiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Vijana wa Kijiji hicho cha Kichungwani kuanzisha vikundi vya ushirika kwa lengo la kupata nguvu za pamoja.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaanzisha mfuko wa uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ikilenga zaidi kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira kutoka Serikali kuu ambazo kwa hivi sasa zinaonekana kuwa na upungufu.
Aliwahakikishia Wananchi hao wa Kichungwani hasa Vijana kwamba Uongozi wa Jimbo hilo chini ya usimamizi wake utajitahidi kadri ya uwezekano ili kuona mfuko huo pia unawafaidisha wananchi wa Kijiji hicho.
Mapema baadhi ya Wananachi wa Kijiji hicho walielezea kero na changamoto zinazowakabili kwa muda mrefu sasa waskizitaja kuwa ni pamoja na huduma za Bara bara, Umeme na Maji safi na salama.
Hata hivyo Wananchi hao walisema huduma za maji safi na salama tayari zimeaanza kupatikana katika baadhi ya mitaa ya kijiji hicho lakini changamoto inayowakabili ni kwa baadhi ya mipira iliyotandikwa katikia maeneo hayo kuvujisha maji na kuleta usumbufu.