Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad,akizungumza na Balozi Mpya wa Ujerumani Nchini Tanzania Mhe,Egon Kochanke,alipofika Ofisini kwake migombani Mjini Zanzibar leo kujitambulisha.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad,akisalimiana na Balozi Mpya wa Ujerumani Nchini Tanzania Mhe,Egon Kochanke,alipofika Ofisini kwake Migombani Zanzibar leo kujitambulisha.[Picha na Salmin Said.OMPR]
Na.Khamis Haji, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameiomba Ujerumani kuiunga mkono Zanzibar katika hatua inazozichukua za kukabiliana na tatizo la vijana wengi kukosa ajira na kuwapatia shughuli za kujiletea maendeleo.
Maalim Seif ametoa ombi hilo alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe. Egon Kochanke aliyemtembelea huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, kwa ajili ya kujitambulisha baada ya kupewa wadhifa huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema miongoni mwa matatizo makubwa yanayoikabili Zanzibar kama zilivyo nchi nyingi Barani Afrika ni vijana wengi kukosa ajira na shughuli za kujiletea maendeleo, hivyo Ujerumani inayo nafasi kubwa ya kusaidia kukabiliana nalo.
Amesema miongoni mwa njia muafaka kuweza kufanikisha azma hiyo ni nchi hiyo kuelekeza nguvu zaidi katika kusaidia elimu ya amali, ambayo itawawezesha vijana wa Zanzibar, wakiwemo wale wanaomaliza masomo kuweza kupata mbinu za ajira.
Maalim Seif amesema Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa katika sekta ya elimu na sasa inakaribia kufanikisha malengo ya Milenia, lakini bado elimu inayotolewa haijakuwa na bora unaowawezesha vijana kukabiliana na changamoto za uhaba wa ajira.
Maalim Seif amesema hatua nyengine ni kwa nchi hiyo kupanua uwekezaji hapa Zanzibar katika nyanja za viwanda vidogo vidogo pamoja na uwekezaji wa bahari kuu, ambapo Zanzibar kuna fursa kubwa katika sekta hizo kutokana na maumbile yake.
Mbali na maeneo hayo, Maalim Seif amesema fursa nyengine muhimu za mashirikiano kati ya nchi mbili hizo ni katika sekta za utalii na kilimo.
Naye Balozi Kochanke amesema amepokea maombi hayo na yatazingatiwa katika mipango ya mashirikiano ya nchi yake na Tanzania kwa lengo la kusaidia jamii kuondokana na ukosefu wa ajira, elimu duni na kuimarisha afya za wananchi.
Amesema yeye binafsi atakuwa Balozi mzuri katika kuiuza Tanzania na Zanzibar kwa wawekezaji wa Ujerumani katika muda wake wa kazi, kwa azma ya kukuza ushirikiano na maendeleo ya wananchi wa pande hizo.
Balozi Kochanke amesema anaelewa kuwa Zanzibar inazo fursa nyingi za kiuchumi na biashara, ikiwemo kilimo cha viungo na Utalii ambazo wawekezaji wa Ujerumani wanaweza kuzitumia katika kufungua miradi yao.
Katika mazungumzo yake, Balozi huyo wa Ujerumani ameipongeza Zanzibar kwa juhudi kubwa ilizozichukua kufanikisha maridhiano ya kisiasa na kufikia maamuzi ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Akizungumzia suala la utafutaji wa Katiba mpya hapa nchini, Balozi Kochanke amesema wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya mchakato huo na wanasubiri kuona hatua zitakazoweza kuchukuliwa baada ya kujitokeza kwa mkwamo katika hatua hii ya Bunge la Katiba.
Awali Maalim Seif alimueleza Balozi huyo kwa urefu mchakato huo ulipofikia, ikiwemo kasoro zilizojitokeza tangu mchakato huo ulipoanza hadi kufikia sasa.