Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein afungua mkutano wa kumi na moja wa chama cha majaji na mahakimu cha Afrika Mashariki

$
0
0

Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ni wakati muafaka kwa mahakama, vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria na jamii barani Afrika kushirikiana kwa pamoja katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo la kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu barani humo.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa kumi na moja wa Chama cha Majaji na Mahakimu cha Afrika Mashariki(EAMJA) unaofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort leo Dk. Shein amesema kumekuwepo na mjadala wa muda mrefu juu ya uhusiano wa ongezeko la vitendo hivyo na ufanisi wa utendaji kazi katika vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria.

“Kumekuwepo na mijadala mingi kuhusu utendaji wa vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa Sheria katika nchi nyingi barani Afrika na mingi ya mijadala hiyo inaonyesha kidole udhaifu katika utekelezaji wa sheria ambao unaelezwa kuwa unachangia ongezeko hilo la vitendo vya kihalifu” Dk. Shein.

Aliongeza kuwa tatizo hilo linatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazokwamisha maendeleo barani Afrika.

Katika mnasaba huo, Dk. Shein amewataka wanachama wa EAMJA kuendelea kufanyakazi kwa karibu na vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria pamoja na jamii ili kuhakikisha sheria zinatekelezwa ili haki iweze kutendeka.

Alivitaja baadhi ya vitendo vya kihalifu ambavyo vitachukua nafasi katika mijadala ya mkutano huo kuwa ni pamoja na rushwa na unyanyasaji watoto.

Dk. Shein aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejidhatiti kupambana na tatizo la rushwa nchini na imeunda mamlaka maalum ya kushughulikia rushwa na uhalifu wa kiuchumi.

“Serikali imeanzsiha Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhalifu wa Kiuchumi na tumekuwa tukifanya jitihada kubwa kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya rushwa, uhalifu wa kiuchumi na umuhimu wa kuzingatia maadili” Dk. Shein alifafanua.

Kwa hiyo ameeleza matumaini yake kuwa mkutano huo wa siku tano utakuwa wa manufaa sana kwa Zanzibar kwa kuwa utaimarisha ujuzi na ufahamu wa wataalamu wa sheria wa Zanzibar ambao ni miongoni mwa washiriki.

Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya mkutano huo ambayo ni ‘Haki ya kuishi: mtazamo na changamoto’ Dk. Shein alikiri kuwa baadhi ya masuala yatayozungumziwa chini ya kaulimbiu hiyo yanayoweza kugusa imani za kidini na hata itikadi za watu hivyo aliwataka washiriki wasiongozwe tu na taaluma bali kuzingatia mila, silka na utamaduni wa Afrika.

“Katika mijadala yenu ningewaomba muzingatie utamaduni na silka za watu wa Afrika. Si kila kitu kizuri kwa jamii nyingine kwa mfano Ulaya na Marekani lazima kiwe kizuri kwetu sisi Afrika” aliwasihi na kuongeza kuwa mijadala na maazimio ya mkutano huo ni vyema yazingatie tamaduni za nchi za Afrika  Mashariki.

Katika mkutano huo miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa na kutarajiwa kuzua mjadala mkubwa ni pamoja na hukumu ya kifo na suala la utoaji mimba. Masuala hayo yamekuwa yakichukua nafasi kubwa katika mijadala mbalimbali ya kisheria kutokana na kuwepo mitazamo tofauti na hoja mbalimbali zinazokataa au kuunga mkono zote zikihusisha haki za binadamu.

Dk. Shein ameishukuru EAMJA kwa kuiteua Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kueleza uamuzi huo unathibitisha imani ya wanachama wake kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

“Uteuzi wenu za Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano huu unathibitisha imani ya wanachama wa EAMJA kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa” Dk. Shein alibainisha.

Ameongeza kuwa mkutano huo unafanyika katika kipindi muhimu cha historia ya Zanzibar kwa kuwa ndio inaelekea kuadhimisha mika 50 ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964”alisema Dk. Shein na kubainisha kuwa “ ni wakati mzuri kushirikiana na majirani zake hivyo mkutano huu ni mwanzo mzuri”

Wakati huo huo Chama cha Mahakimu na Majaji cha Afrika Mashariki kimeishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake katika kufanikisha maandalizi ya mkutano wake wa mwaka.
Rais wa chama hicho ambaye anamaliza muda wake Dk. Fauz Twaib amesema wamefurahishwa na msaada na ushirikiano uliopata chama chake kutoka Serikali katika kufanikisha mkutano huo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>