Na Khamis Amani
WAZIRI wa zamani katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mansoor Yussuf Himid, ameachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu ya Zanzibar .
Mansoor ambae alikuwa Mwakilishi wa jimbo la Kiembe Samaki kabla ya kufukuzwa na CCM, alikaa kizuizini kwa muda wa siku 14 kutokana na kukabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kupatikana na silaha katika mahakama ya mkoa Vuga.
Jaji wa Mahakama Kuu, Abraham Mwampashi, alimpatia dhamana mshitakiwa huyo baada ya kunyimwa na mahakama ya mkoa Vuga, chini ya hakimu Khamis Ramadhan Abdalla alipofikishwa kwa mara ya kwanza.
Masharti yaliyotolewa na mahakama kuu ni kuwa na wadhamini wawili wenye kuaminika na kukubalika vizuri ambao kila mmoja atasaini bondi ya shilingi milioni tano.
Kabla ya kutoa maamuzi hayo, Jaji Mwampashi alitupilia mbali hoja za upande wa mashtaka kwamba shitaka linalomkabili halina dhamana kwa kusema kwa mujibu wa sheria, hakuna shitaka lolote lisilokuwa na dhamana na wala mtu kukutwa na silaha sio hatari.
Mansoor aliwasilisha ombi la kupatiwa dhamana chini ya kifungu cha 150 (4) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7 ya 2204 sheria za Zanzibar .
Masharti mengine ni fedha taslimu shilingi milioni tatu, kuwasilisha mahakamani hati ya kusafiria pamoja na kumtaka kutoondoka nchini bila ya idhini ya mahakama.
Alisema kauli hizo (mashtaka yasio na dhamana) zitahitajika kuangaliwa ni wapi zinatumika kwani mahakama za mwanzo hadi mkoa ndizo zisizopaswa kutoa dhamana kwa makosa yaliyoainishwa katika kifungu cha 150 (1) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar .
Alisema Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutoa dhamana kwa makosa yaliyoainishwa katika kifungu hicho kwa mujibu wa kifungu kidogo cha nne (4) cha sheria hiyo.
Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Raya Issa Mselem, aliiomba mahakama kukizingatia kifungu kidogo cha kwanza, kutokana na kwamba tayari kuna watu kadhaa wanashikiwa kwa sheria jambo ambalo Jaji Mwampashi hakukubaliana nalo.
Kutokana na kauli hiyo, Jaji Mwampashi alisikitika kuona watu hawaitumii sheria hiyo ambapo sio kila mtu anaweza kunyimwa dhamana bali kuna wengine wanahitajika kupatiwa kutokana na vigezo mbali mbali, na kuomba watu wakitumie kifungu hicho ili waweze kupata haki zao za kikatiba.
Akipingana na hoja za upande wa wapingaji dhamana, (DPP) kuhusu hatari ya muombaji huyo ya kukutwa na silaha, Jaji Mwampashi alisema kukutwa na silaha si hatari bali hatari ipo katika matumizi ya silaha.
Alisema, upande wa wapingaji umeshindwa kuonesha hatari ya muombaji ya kumiliki silaha ambayo alikamatwa nayo nyumbani kwake baada ya upekuzi na wala hawakuonesha madhara aliyoyafanya ya kuitumia silaha hiyo kinyume cha sheria.
Pamoja na mambo mengine Jaji Mwampashi alisema, muombaji ni mtu anaejulikana na kufahamika ambae ni mdau mkubwa wa serikali katika harakati za maendeleo za ulipaji wa kodi kutokana na biashara zake anazozifanya.
Alisema, kukaa kwake kizuizini ni kuikosesha serikali mapato pamoja na kuitia hasara kutokana kuwepo kwake rumande kutakuwa ni mzigo kwa serikali wa kumtunza pamoja na gharama za usafiri wa kwenda na kurudi mahakamani na ilhali ni mtu mwenye shuguli zake ambazo zinatoa ajira kwa vijana.
Hivyo Jaji Mwampashi, alilazimika kumpatia muombaji huyo masharti hayo ya dhamana ambayo aliweza kuyatekeleza baada ya mahakama ya mkoa kutakiwa kuyasimamia.
Wakati huo huo, mahakama ya mkoa Vuga mara baada ya kumwachilia mshitakiwa huyo kwa masharti hayo ya dhamana, mahakama hiyo iliyo chini ya hakimu Khamis Ramadhani Abdallah ameiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 28 mwaka huu kwa kutajwa kutokana na upelelezi wake bado haujakamilika.
Mansoor aliwasili mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi akitokea rumande ili kuendelea na kesi inayomkabili ambayo kwa mara ya kwanza ilifikishwa mahakamani hapo tokea Agosti 5 mwaka huu na kusomewa mashitaka ya kupatikana na sialaha, risasi na marisau kinyume cha sheria mashitaka ambayo aliyakana.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliongozwa na Wakili wa serikali Maulid Ame Mohammed na Khamis Juma Khamis na upande wa utetezi ulisimamiwa na Wakili wa kujitegemea Gaspar Nyika na Omar Said Shaabani.
Nje ya mahakama Mansoor alionekana akitembea barabarani huku akilakiwa na mkewe pamoja na ndugu, jamaa na marafiki kwa kumfariji na baadae aliondoka katika viunga vya mahakama majira ya saa 7:28 za mchana akiwa ndani ya gari aina ya PRADO yenye nambari za usajili Z 103 AE.