HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA
MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN KATIKA
UFUNGUZI WA MICHEZO YA MAJESHI YA JUMUIYA YA
NCHI ZA AFRIKA YA MASHARIKI: ZANZIBAR
TAREHE 20 AGOSTI, 2014
_______
Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi;
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mliohudhuria,
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania;
Jenerali Davis Mwamunyange,
Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama,
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi;
Mheshimiwa Maalim Abdalla Mwinyi Khamis,
Viongozi mbali mbali mliohudhuria,
Wageni Waalikwa,
Ndugu Wapiganaji na Wanamichezo,
Mabibi na Mabwana,
Awali ya yote naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya na uhai tukaweza kukutana hapa siku ya leo tukiwa na furaha kubwa ya kuja kufanya ufunguzi wa Michezo ya Majeshi ya Jumuiya ya Nchi za Afrika ya Mashariki. Kwa dhati kabisa naipongeza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na makamanda wetu wakuu kwa uwamuzi wa kuyafanya mashindano ya nane ya Michezo na Utamaduni ya Majeshi ya Jumuiya ya Afika Mashariki haya Zanzibar ambayo yanafanyika kwa mara ya pili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007. Kwa hakika tumefurahi kwa ugeni huu na tunasema hongereni na ahsanteni sana.
Pili, natoa shukurani kwa Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa michezo hii yenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha fungamano na ushirikiano wa wananchi wa nchi za Afrika ya Mashariki wakiwemo wapiganaji wetu.
Tatu, natoa pongezi kwa waandaaji wa michezo hii kwa maandalizi mazuri na napenda kuitumia fursa hii kuwakaribisha Zanzibar wageni wetu wote hasa waliotoka nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkiwa hapa mtapata nafasi ya kuyatembelea maeneo mbali mbali ya kihistoria na kuushuhudia utajiri wa mazingira tulionao pamoja na kujionea ukarimu na moyo wa kirafiki wa wenyeji wenu. Tanzania ni nchi ya amani na watu wake tuna umoja na mshikamano na kwa hivyo, tunakukaribisheni Zanzibar yenye hali ya amani na utulivu. Kwa jumla, nasema karibuni nyote na ninakuombeni mnapokuwepo hapa basi mjione mpo nyumbani.
Ndugu Viongozi, Wapiganaji na Wanamichezo,
Nimepata faraja kubwa kushuhudia vuguvugu la michezo linalojumisha wanamichezo wanawake na wanaume wapatao 450. Vugu vugu la michezo ni jambo ambalo limo ndani ya damu yangu, tangu nikiwa mwanafunzi kwa kushiriki michezo mbali mbali. Mimi mwenyewe nilikuwa nikishiriki katika michezo hasa riadha na mpira wa miguu, wakati nikiwa katika Skuli ya Msingi ya Gulioni na skuli ya Sekondari ya Lumumba, Unguja; kwa wakati huo. Naamini wale tuliokuwa pamoja miaka hio, watakumbuka vizuri zama zetu hizo, jinsi tulivyokuwa tukishirikiana.
Ni matumaini yangu kuwa michezo hii tunayoifungua leo itatoa msisimko katika kipindi hiki cha mashindano na itaacha matokeo mazuri kwa wananchi kuipenda michezo na kufufua ari ya kuiendeleza michezo nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi wa michezo yetu katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki. Kadhalika, mashindano haya ya michezo na utamduni ya majeshi ni kielelezo halisi kitakachoithibitishia dunia umoja na mshikamano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ndugu Viongozi, Wapiganaji na Wanamichezo,
Ni dhahiri kuwa wanajeshi wetu wako mstari wa mbele katika kusimamia suala la amani na usalama katika Ukanda wa Afrika Mashariki na sehemu nyengine duniani. Jitihada za majeshi yetu zimechangia sana kuimarika kwa hali ya amani na utulivu. Masuala haya ndio msingi mkubwa unaochangia kuwepo kwa maendeleo tunayoshuhudia katika sekta zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Hali hiyo imechangia sana kuufanya ukanda huu kuwa ni kivutio kikubwa cha wawekezaji na watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Mtakubaliana nami kuwa Makubaliano ya Awali ya Ushirikiano wa Kiulinzi ya tarehe 30 Novemba 2001 baina ya nchi wanachama wa jumuiya yetu yaliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012 ili yaende vizuri zaidi na malengo ya kuwepo kwa Jumuiya yetu, yameweka msingi wa ushirikiano wa majeshi katika masuala ya mafunzo, kuendesha oparesheni za pamoja, mashirikiano ya kiufundi, kutembeleana na kubadilishana taarifa. Ni jambo la fahari kwamba majeshi yetu yameweza kufanikiwa vyema katika utekelezaji wa masuala hayo muhimu ya ushirikiano.
Ndugu Viongozi, Wapiganaji na Wanamichezo,
Kwa kipindi kirefu, vile vile majeshi yetu yamekuwa yakitoa mchango muhimu wa kupata wachezaji wa michezo mbali mbali wanaoziwakilisha timu zetu katika michezo ya kimataifa. Sote tunafahamu kuwa baadhi ya timu za majeshi katika nchi zetu za Afrika ya Mashariki ndizo zinazotoa upinzani mkubwa katika mashindano ya kitaifa na baadhi yao kuwa mabingwa na kuziwakilisha nchi zetu kimataifa.
Kadhalika, wapiganaji wetu wameendelea kuwa washiriki wazuri katika michezo ya riadha, mbio za baiskeli, kuogelea na michezo mengine. Napenda kuchukua fursa hii kuvipongeza vikosi vyetu vyote kwa kuzingatia umuhimu wa michezo kwa wapiganaji wetu na kuweza kuziwakilisha nchi zetu katika michezo ya kimataifa. Nakunasihini muendelee na utaratibu wenu wa kuifanya michezo kuwa ni miongoni mwa ya mambo muhimu yanapaswa yaendelezwe katika vikosi vyetu.
Ndugu Viongozi, Wapiganaji na Wanamichezo,
Wataalamu wanasisitiza umuhimu wa michezo kwa kuimarisha afya zetu. Upo usemi maarufu usemao “Akili bora hukaa katika kiwili wili chenye afya”. Kwa vile michezo huimarisha afya ya kiwiliwili ni dhahiri kuwa akili zenye kuzingatia masuala muhimu kama vile ya ulinzi na usalama wa wananchi wetu na mipaka ya nchi zetu hutegemea kuwepo kwa walinzi wenye afya nzuri ambao ndio nyinyi. Kwa mara nyengine napenda nikupongezeni kwa kuizingatia hali hiyo.
Kadhalika, michezo huimarisha ushirikiano na kuleta burudani na furaha mambo ambayo ni muhimu hasa kwa watu wanaosimamia na kuyatekeleza majukumu mazito kama haya ya ulinzi. Kupitia medani ya michezo, majeshi yetu yanaweza kuimarisha uhusiano na kuangalia maeneo mapya ya kushirikiana ili kuzidi kuyamudu vyema majukumu yao.
Natoa wito kwenu kuitumia vyema fursa hii na kubadilishana uzoefu na mbinu mbali mbali za kukabiliana na changamoto zinazoyakabili majeshi yetu kwa kuelewa kuwa nyote mna dhamana ya kusimamia amani na usalama wa wananchi wa Afrika
ya Mashariki na kuendelea kuhakikisha ukanda huu ni wenye amani ya kudumu.
Ndugu Viongozi, Wapiganaji na Wanamichezo,
Napenda nikukumbusheni kuwa michezo ni nidhamu. Hii ndiyo maana michezo yote huongozwa na sheria ambazo ndizo zinazotawala michezo yenyewe. Ni jambo zuri kuwa nidhamu katika shughuli za kiaskari ni jambo linaloongoza shughuli zenu za kila siku. Kwa hivyo, hapana shaka, kuwa uzowefu wenu wa kuzingatia umuhimu wa nidhamu utazidi kuendelezwa katika uendeshaji wa mashindano haya na kwa vyo vyote vile mtaiepuka migogoro isitokee; ambayo inaweza kuathiri lengo la kufanywa kwa mashindano haya.
Naamini viongozi, wachezaji na waamuzi wote watazingatia umuhimu wa kuepuka uwezakano wa mivutano. Kwa jumla tuendelee kuamini ule usemi maarufu wa Kiswahili usemao “Asiye kubali kushindwa, si mshindani”. Kwa hivyo, tuingie mashindanoni tukiwa tayari kwa matokeo yoyote. Mwishoni mwa michezo yetu sote tutakuwa washindi iwapo tutafanikiwa kuitumia michezo hii kwa ajili ya kuimarisha urafiki, udugu na umoja tulionao.
Ndugu Viongozi, Wapiganaji na Wanamichezo,
Ni lazima tukubali kwaba tuna changamoto kubwa kwa vile matokeo ya timu zetu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kwenye michezo mingi ya kimataifa si ya kuridhisha. Nyote mnajua kuwa hali ya ushiriki wa timu zetu katika mashindano ya mpira wa miguu na nafasi za nchi zetu katika viwango vya FIFA si nzuri. Kadhalika, hivi karibuni tumesikia matokeo ya timu zetu katika michezo ya Jumuiya ya Madola iliyomalizika katika mji wa Glasgow huko Uingereza nayo hayakuwa ya kuridhisha sana. Napenda kuwapongeza ndugu zetu wa Kenya, ambao wametuosha nyuso zetu kwa kurudi na medali nyingi kwa upande huu wa Afrika Mashariki. Wito wangu kwa timu zetu za majeshi ni kuweka mikakati na kutupatia wanamichezo wazuri ambao wataziwakilisha vyema nchi zetu katika mashindano ya kimataifa na kutuletea ushindi na medali mbali mbali.
Vile vile, ni vyema ukaandaliwa utaratibu kwa wanamichezo wa majeshi, ambao ndio wenye weledi mkubwa katika fani za michezo mbali mbali, wakapewa nafasi ya kueneza ujuzi na maarifa yao kwa raia, hasa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa taasisi za umma. Naamini kwamba utaratibu huu utasaidia sana katika kuibua vipaji vya riadha na michezo mengine kwa wananchi waliopo uraiani.
Ni jambo la fahari kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata fursa nyengine ya kuandaa michezo itakayozijumuisha nchi zetu za Afrika ya Mashariki kupitia michezo ya Skuli za Sekondari inayojulikana kama FEASSA. Michezo hiyo inayotarajiwa kuanza tarehe 23 Agosti na itafanyika katika jiji la Dar es Salaam. Timu yetu ya Zanzibar yenye wanamichezo wa michezo mbali mbali itashiriki kwa azma ya kushindana na sina shaka itafanya vizuri. Nawapongeza sana viongozi na walimu waliowaandaa vijana wetu na nawatakia mafanikio makubwa katika mashindano hayo.
Ndugu Viongozi, Wapiganaji na Wanamichezo,
Vile vile, napenda kuitumia fursa hii, kuzungumzia umuhimu wa kuendeleza uhusiano mwema kati ya majeshi yetu na raia jambo ambalo linaendelea vizuri na ni sehemu ya maisha yetu, kupitia huduma mbali mbali mnazozitoa vikosini, ikiwa ni pamoja na huduma za afya, elimu na kutoa huduma wakati wa majanga mbali mbali. Kadhalika, nawapongeza wanajeshi wa Kenya kwa mpango wao wa kutoa wapiganaji wao kusomesha katika skuli zenye upungufu wa walimu. Niliwaona hivi karibuni kupitia kituo cha televisheni cha Citizen. Hongereni sana. Kwa hakika nakupongezeni sana wanajeshi nyote kwa mafanikio yenu katika utoaji wa huduma kwa raia. Hapana shaka kwamba mtaongeza jitihada ya kuendeleza uhusiano mzuri na raia, kuzingatia maadili mema na kujijengea taswira nzuri.
Ndugu Viongozi, Wapiganaji na Wanamichezo,
Namalizia nasaha zangu kwa kukutakieni kila la kheri katika kuendesha mashindano yetu. Michezo hii iwe ni chachu ya kutuunganisha zaidi na kufanikisha malengo ya kuendeleza Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baada ya kusema hayo, ninafuraha kutamka kwamba Michezo ya Majeshi ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki hapa Zanzibar imefunguliwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.