Na Joseph Ngilisho,Arusha
WASHTAKIWA wa kesi ya ugaidi na kusajili vijana kujiunga kundi la Al- Shabaab la Somalia, wameutaka upande wa Mashitaka kuwaeleza alipo mshitakiwa mwenzao namba mbili, Abdallah Thabit.
Malalamiko hayo waliyatoa jana mbele ya Hakimu Mkazi ,Rose Ngoka, wakati kesi hiyo ilipotajwa na kuiomba mahakama iwaeleze alipo mwenzao ambaye walikamatwa naye pamoja.
Swali hilo liliulizwa na mshitakiwa Ally Hamis ambaye alinyoosha mkono na kumuomba Hakimu Ngoka kwa kusema kuwa ni muda mrefu umepita tangu walipokamatwa lakini wanashanga mshitakiwa mwenzao Thabiti kutomwona mahakamani.
Alisema walikamatwa na mwenzao Thabiti lakini tangu wapandishwe kizimbani kwa mara ya kwanza Julai 24,hadi leo hii hajaletwa mahakamani.
Akitoa taarifa mbele ya mahakama hiyo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Gaudencia Joseph alidai kwamba ndio mara yake ya kwanza ameisikia taarifa hiyo hivyo atakwenda kuifanyia kazi.
“Taarifa hii ndio naisikia leo hapa na hii ni kwa sababu Mwendesha Mashitaka anayesimamia shauri hili leo hayupo, hivyo sikuwa na taarifa kama walishawahi kuwasilisha malalamiko yao na yeye atakapokuja siku nyingine atasema huyo mtuhumiwa yupo wapi,” alidai.
Alisdai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Hata hivyo Hakimu Ngoka aliingilia kati na kutoa ufafanuzi kwamba majibu sahihi yangeweza kutolewa na Mwendesha Mashitaka aliyekuwepo kwani hata Hakimu anayesikiliza shauri hilo naye hakuwepo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 3 mwaka huu huku.
Washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi, ambapo sheria namba 22 ya mwaka 2002 inasema upelelezi ukishakamilika, mahakama kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Mbali na mashitaka hayo pia wanahusishwa na tukio la mrpuko wa bomu lilitokea baaya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.
Washitakiwa hao ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti,Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajabu Hemedi, Hasani Saidi, Ally Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa,Swalehe Hamisi,Abdallah Yasini, Abdallah Maginga na Sudi Nasibu Lusuma.
Wengine walioongezwa katika shauri hilo ni Shaban Musa, Athuman Hussein, Mohamed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohamed na Said Michael Temba.