Na Mwandishi wetu
SERIKALI imetangaza kuzifuta ajira 200 za Konstebo na Koplo wa Uhamiaji, baada ya Kamati iliyoundwa kufanya uchunguzi, kugundua kwamba watu waliokuwa na sifa waliachwa.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak Abdul Wakil, alisema ajira hizo ni pamoja na zile 28 za upande wa Zanzibar.
Alisema Kamati iligundua kwamba kulikuwa na upendeleo mkubwa na kwamba waombaji wengi waliokuwa na sifa waliachwa na kuchukulia watu wengine wakiwemo ndugu wa watumishi wa Idara hiyo.
Hivyo, alisema usaili huo utafanywa upya na utasimamiwa na serikali badala ya Idara ya Uhamiaji.
Ajira hizo zilisitishwa mwezi uliopita baada ya vyombo vya habari kufichua upendeleo uliofanywa na watumishi wa Idara hiyo, ambapo wengi wa walioajiriwa walikuwa ndugu au watu wa karibu wa wafanyakazi.
Zaidi ya waombaji 15,707 waliomba nafasi hizo na majina ya 200 ya waliofaulu kutoka Tanzania Baraza yalitangazwa kupitia vyombo vya habari pamoja na 28 kutoka Zanzibar.