Na Rose Chapewa, Morogoro
POLISI Mkoani Morogoro limemtaka Katibu wa Jumuiya ya Kiislamu Tanzania, Issa Ponda kujitokeza hadharani na kuuthibitishia umma ikiwa amejeruhiwa kwa risasi na jeshi la polisi kama inavyodaiwa.Polisi pia linawashikilia wafuasi wake wawili kwa tuhuma za kuwazuia askari kumkamata na kuwatafuta watano walioandaa kongamano.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Faustine Shilogile alisema jeshi hilo bado linaendelea kumsaka kiongozi huyo kwa tuhuma za uchochezi, pamoja na kukiuka amri ya mahakama.
Kamanda huyo alisema hadi sasa jeshi hilo halifahamu mahali alipo kiongozi huyo, lakini linaamini bado yupo mkoani hapa na kuomba wananchi pamoja na ndugu zake ambao wanajua mahali alipo wafike kituo cha polisi kudhibitisha kama amepigwa risasi.
Alikanusha taarifa zilizozagaa kwenye mitandao kuwa kiongozi huyo amepigwa risasi na askari polisi kwenye bega la kulia, na kwamba hakuna ushahidi kwa kuwa hajaonekana ili kuonesha kuwa amepata majeraha sehemu yoyote ya mwili wake.
“Jamani mtu yeyote aliyepigwa risasi huwa hajifichi, na hata kidonda chake kinajijulisha wazi,kama amepigwa angejitokeza ili kupewa kibali cha matibabu, na angepata matibabu kwenye hospitali kubwa sio vichochoroni,” alisema Shilogile.
Aidha alisema pamoja na kuwashikilia watu wawili ambao hakupenda kutaja majina yao kwa kuwa uchunguzi bado unaendelea, linawatafuta viongozi watano wa kundi ambalo liliandaa kongamano hilo ambalo liliandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa Kislamu mkoa wa Morogoro.
Alisema umoja huo ulipewa kibali na jeshi hilo kwa jili ya kufanya kongamano kwa masharti ya kutotoa lugha ya uchochezi ikiwa pamoja na Sheikh huyo kutokuwepo katika kongamano hilo kwa kuwa amekuwa akitafutwa na jeshi la polisi nchini, kwa tuhuma za uchochezi.
Alisema Ponda alikuwa kitafutwa kwa tuhuma za uchochezi Zanzibar pamoja na kukiuka masharti ya mahakama kwa kufanya miadhara ya uchochezi katika maeneo mbalimbali.
Alisema Agosti 10 saa nane mchana katika eneo la uwanja wa shule ya msingi kiwanja cha ndege Manispaa ya Morogoro kulifanyika kongamano hilo na kulikuwepo na wageni zaidi ya watano ambao walihutubia kongamano hilo.
Kamanda huyo alisema dakika 10 kabla ya mkutano kumalizika majira ya saa 12.50 jioni alifika sheikh Ponda na kukaa na baadaye kupewa dakika tano kuzungumza ambapo alieleza kuwa yeye sio mzungumzaji kwa siku hiyo na badala yake angezungumza Agosti 11 katika viwanja vya msikiti wa Jabalihira.
Alisema baada ya hapo mkutano ulifungwa na wafuasi wake wakaanza kusukuma gari alilokuwa amepanda katika barabara ya Tumbaku karibu na kituo cha mafuta cha El Saedy huku askari wakimfuata kutaka kumtia mbaroni.
Kamanda Shilogile alisema kabla ya polisi kumtia mbaroni wafuasi walianza kurusha mawe kwa askari, na ndipo walipofyatua risasi tatu za baridi juu ili kuwatawanya, na kumkamata katika mazingira salama, lakini walizidiwa nguvu na wafuasi hao ambao walikuwa zaidi ya 3000 na kufanikiwa kumtorosha kwa njia ya pikipiki.
Alisema baadaye zilizagaa taarifa kuwa amepigwa risasi ya begani na kukimbizwa katika hospitali ya mkoa na badaye kutoroshwa kusikojulikana na kwamba mpaka sasa polisi hawajathibitisha tukio hilo.
Alitumia muda huo kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la polisi watakapomuona Ponda ili akamatwe kwani jeshi hilo limejipanga katika mazingira yoyote ya kumkamata, na kwamba ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kuwazuia polisi kumkamata mhalifu.
Hata hivyo, watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Sheikh Ponda walivamia hospitali ya mkoa wa Morogoro na kufanya uharibifu wa kuvunja vioo katika wodi namba 6 ya watoto, wakishinikiza kufunguliwa geti ili wamtoroshe kiongozi huyo baada ya kumpeleka hospitalini hapo na kubaini usalama mdogo juu yake.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa na watoto wao katika wodi hiyo,Kibua Michael mkazi wa Kisaki Morogoro vijijini na Cecilia Clemence mkazi wa manispaa ya Morogoro walisema wafuasi hao walirusha mawe juu ya bati kwenye wodi hiyo, hivyo kuwafanya kuwa na hofu kubwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Litha Lyamuya alipoulizwa juu ya tukio hilo, alithibitisha wafuasi hao kufanya uharibifu hospitalini hapo ambapo walivunja kioo wodi namba sita pamoja na kuiba machela.
Alisema walifika chumba cha daktari wakiwa wamembeba mgonjwa wao kwenye machela, na kabla ya kumuona daktari waliamua kuondoka kwa kutumia geti namba mbili kupitia wodi namba sita.