Na Kija Elias, Moshi
TAASISI ya Kuzuia na Kumbana na Rushwa (TAKUKURU), imeokoa kiasi cha shilingi bilioni 38.96, kupitia operesheni mbali mbali na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, iliyotekelezwa na serikali katika kipindi cha mwezi Julai,2013 hadi Juni 2014.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Edward Hosea,aliyasema hayo jana alipokuwa akitoa maelezo ya kazi za taasisi yake kwa kipindi hicho kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa siku tatu wa wakuu wa TAKUKURU, unaofanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema taasisi hiyo imeweza kuokoa kiasi hicho cha fedha, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 33.59, ikilinganishwa na fedha zilizookolewa mwaka 2013.
Alisema katika uchunguzi wa taasisi hiyo, imefanikiwa kufungua kesi mpya 327, pamoja na kesi kubwa tatu zinazowahusu viongozi wa serikali, ambao wamebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Alisema kazi hiyo ni juhudi ambazo zimefanywa na taasisi hiyo, ambayo hivi sasa imepiga hatua kubwa ya kiutendaji ikilinganishwa na taasisi kama hiyo kwa nchi nyingi za Afrika.
Akielezea mpango wa elimu kwa umma unaolenga kudhibiti rushwa, alisema hadi sasa taasisi hiyo imeweka mkazo kwenye ufunguzi wa klabu za wapinga rushwa katika skuli za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu.
Aliongeza kuwa hadi sasa taasisi hiyo ina jumla ya klabu 2,371 katika skuli za msingi kote nchini, zenye jumla ya wanachama 172,706, ambapo kwa upande wa skuli za sekondari zipo jumla ya klabu 4,016 zenye wanachama 270,422 na klabu 85 katika vyuo na taasisi za elimu ya juu zenye wanachama 9,643.
Awali akifungua mkutano huo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, aliitaka TAKUKURU kuongeza juhudi za kuwabana watumishi wa umma, wanaolalamikiwa kuhusika kwenye vitendo vya rushwa.
Alisema muundo wa taasisi hiyo unatakiwa kufikisha huduma zake kuanzia ngazi za wilaya,ili kuwasaidia wananchi kuwatatulia matatizo ya rushwa, ambayo yanafanywa na baadhi ya wachache.
Alisema rushwa imekuwa tishio katika baadhi ya maeneo na kuitaka taasisi hiyo, kuhakikisha inaanza kuwabana viongozi wa kisiasa wanaohusika kutoa rushwa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
Mkutano huo wa siku tatu, umewakutanisha Wakurugenzi wa idara mbali mbali za taasisi hiyo, maofisa wa TAKUKURU ngazi ya mkoa na wilaya zote nchini, wakiwemo wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Kilimanjaro.