Mh. Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dar-Es-Salaam
Tanzania
Kwa heshima tafadhali husika na mada ya hapo juu.
Wananchi wengi ndani na nje ya nchi kwa kupitia vyombo vya habari vinavyoaminika nchini Tanzania wamepokea kwa mshtuko mkubwa sana habari za kuhuzunisha kuhusu madhila na vitendo vya kishenzi vya udhalilishaji walivyofanyiwa Watuhumiwa wa Kesi ya Ugaidi waliokamatwa usiku wa manane nchini Zanzibar na vyombo vyako vya Dola na kuonekana baadae wakipandishwa kwenye Mahakama ya Kisutu iliyopo nchini Tanganyika. Watuhumiwa wakiwemo Masheikh wakubwa wenye kuheshimika katika Jamii walilalamika Mahakamani kwamba walifanyiwa mateso makubwa na vitendo vya kuwadhalilisha vinavyokwenda kinyume na Haki za Binaadamu kama kuwanajisi na kuwatia majiti na chupa kwenye sehemu zao za siri za nyuma.
Jumuiya yetu imeshtushwa sana kuona katika karne hii ya ishirini na moja chini ya Uongozi wako, Serikali yako inaweza kuwatendea Wananchi wake vitendo kama hivi vya udhalilishaji. Tanzania imekuwa ikijinata kuendeshwa kwa kufuata utawala wa sheria na kuheshimu haki za Binaadamu, lakini kadhia ya Masheikh na matukio ya udhalilishaji waliofanyiwa yametuthibitishia kinyume chake. Jumuiya yetu na wapenda haki wote sio tu tumeshtushwa na matendo ya kinyama ya vikosi vyako lakini pia tumefadhaishwa na utaratibu mzima uliotumika kuwakamata watu usiku usiku nchini Zanzibar kwa tuhuma za ugaidi na kuja kuwafanyiwa mateso na kuwafunguliwa kesi nchini Tanganyika. Hali hii inaonyesha dhahir shahir jinsi Tanganyika kila kukicha inavyozidi kuidhibiti na kuzikandamiza Mamlaka za nchi ya Zanzibar. Tumeona kwa mfano, Watu waliokamatwa Arusha kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya kigaidi, mashtaka yao yalifanyika mjini Arusha, lakini wale waliokamatwa nchini Zanzibar wamefunguliwa mashtaka Dar Es Salaam, nchini Tanganyika, ilhali Zanzibar ina Mahakama zenye uwezo wa kusikiliza kesi kama hiyo waliyoshtakiwa Watuhumiwa.
Jumuiya ya MUWAZA imewahi kulalamika kwako mara kadhaa juu ya namna ya vyombo vya dola vya Tanzania vinavyovunja haki za Binaadamu na kuitia dosari nchi lakini tunaona hali inaendelea kuwa vile vile au tunathubutu kusema inaongezeka kuwa mbaya zaidi.
Ikumbukwe, kwamba kwa mujibu wa sheria ya nchi Mtuhumiwa yeyote huwa hana makosa hadi pale Mahakama itakapothibitisha kwa ushahidi wa kutosha na kumtia hatiani. Hata hivyo, Serikali na Vyombo vyake vya Dola haina haki kwa njia yoyote ile kutumia vitendo vya utesaji na udhalilishajikwa Wananchi wake. Kwahivyo, Mtuhumiwa/Mwananchi yoyote anatakiwa Utu wake uheshimiwe kwa namna zote maana Utu wa kila Mtanzania haugawiki na ni adhimu . Kumnyima Mtanzania yeyote Utu wake ni kulinyima Taifa Utu wake na kulidhalilisha mbele ya macho ya Walimwengu.
Kwa mantiki hiyo Jumuiya ya MUWAZA inakuomba kuliingilia kati suala hili kwa haraka na kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki vitendo hivi viovu vya udhalilishaji vyenye kuvunja haki za Binaadamu.
MUWAZA inatarajia barua hii utaipa mashirikiano makubwa.
KATIBU
Jumuiya ya MUWAZA
UK
Nakala: Rais wa Zanzibar.
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Waziri wa Mambo ya Ndani – Tanzania.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – UK.
Balozi wa Kenya – UK.
Balozi wa Rwanda – UK.
Balozi wa Uganda – UK.
Balozi wa Burundi – UK.