Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Uraia pacha kitanzini

$
0
0
Serikali yataja athari mbili endapo utaruhusiwa

 
Ndoto ya kuwapo kwa uraia pacha nchini yaelekea kitanzini na dalili zake ni dhahiri, baada ya serikali kupigilia msumari kuwa kama azma hiyo itaruhusiwa italeta athari kubwa zikiwamo za kiusalama.
 
Msimamo huo wa serikali ulitolewa mjini Dodoma jana na Idara ya Uhamiaji wakati wa semina ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba iliyokuwa na lengo la kuwapa uelewa wa suala la uraia pacha baada ya kushindwa kufikia muafaka kwenye kamati za Bunge hilo.
 
Wasemaji wakuu katika semina hiyo walikuwa ni Afisa Mwandamizi wa Uhamiaji, Paul Msele, Kamishna wa Idara ya Uhamiaji, Donald Ndagula na Katibu Mtendaji Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, Dk. Philipo Mpango.
 
Suala hilo ambalo lipo katika Sura ya 5 ya Rasimu ya Katiba inayohusu Uraia katika Jamhuri ya Muungano, lilileta mvutano mkali wakati wa mijadala kwenye kamati hali iliyosababisha Bunge hilo kualika viongozi hao wa Uhamiaji kulitolea ufafanuzi wa faida na hasara zake kwa nchi endapo litaruhusiwa.
 
Baada ya semina hiyo ambayo waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia, viongozi hao wa Uhamiaji walikataa kuzungumza na waandishi kwa madai kuwa waliitwa kuzungumza na wajumbe tu na si waandishi wa habari.
 
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe waliohudhuria semina hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe aliliambia NIPASHE kuwa viongozi hao walieleza athari kuu mbili endapo suala la Uraia pacha litaruhusiwa.
 
Alizitaja sababu kuu zilizotolewa na viongozi hao wa Uhamiaji kukataa uraia pacha uruhusiwe nchini kuwa ni Usalama wa Taifa na Uzalendo.
 
Sababu za kiusalama akasema kuwa mtu anayekuwa na uraia wa nchi mbili anaweza kufanya tukio ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa nchi na kukimbilia nchi ambako ana uraia mwingine na kupata hifadhi na ulinzi.
Kuhusu uzalendo, alisema watasababisha watu wengi kukimbia nchi na kwenda kuomba uraia wa nchi nyingine na kuukana u-tanzania.
 
Habari zinasema wakati wa mjadala ulitokea mvutano miongoni mwa wajumbe, wengi wao wakikataa suala hilo kuruhusiwa hasa wajumbe kutoka Zanzibar.
 
Akizungumza baada ya kumalizika kwa semina hiyo, Makamu mwenyekiti wa Kamati Namba 11, Hamad Yusuph Masauni, alisema suala la kuruhusu mtu kuwa na uraia wa nchi mbili halitawezekana kutokana historia za nchi ya Tanzania Bara na Zanzibar.
 
Alisema wamefurahishwa kuandaliwa kwa semina hiyo, ambapo walipata uelewa wa faida na hasara ya kuwa na mfumo huo ndani ya nchi.
 
Alisema katika historia ya nchi hizo, kuruhusu watu kuwa na uraia wa nchi mbili ni sawa na kukaribisha maadui ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kuyumbisha hali ya usalama na amani ya nchi.
 
Akitoa mfano, alisema Zanzibar ilipata uhuru wake kwa njia ya mapinduzi na kusababisha watu wengi waliokuwa wakipinga serikali kukimbilia nje na upande wa Tanzania Bara watu wengi walikimbia wakati wa Sera ya Uhujumu uchumi.
 
“Watu wengi walikimbia nchi kutokana na kuchukizwa na matukio haya mawili, sasa unapowaruhusu kurudi nchini lazima mioyoni yao watajenga vitu fulani ambavyo vinaweza kuleta chokochoko,” alisema.
 
Alisema kwa wale ambao walitaifishiwa mali zao watarudi na kuzidai hali ambayo inaweza ikasababisha migogoro mikubwa na wale waliokimbia kwa sababu za kisiasa ikiwamo Mapinduzi ya Zanzibar wanaweza kurudi na kutaka kulipiza kisasi.
 
Alisema katika mapendekezo ya Katiba Mpya wanaweza wakaweka utaratibu maalum wa kuwatambua Watanzania hao na kuwapa fursa ya kuendeleza nchi bila kutoa nafasi ya kuwa na uraia zaidi ya nchi moja.
 
Kwa upande wake, Mjumbe anayewakilisha Watanzania waishio Nje (Diaspora), Kadari Singo, alionyesha kusikitishwa na serikali pamoja na wajumbe wengi kulipiga vita suala hilo.
 
Alisema endapo uraia pacha utaruhusiwa utaleta faida kubwa kwa nchi, tofauti na wasiwasi walioonyesha wajumbe wenzake.
 
Singo alisema kulingana na kauli ya makamishna wa Uhamiaji ambao walitoa mada ndani ya semina hiyo, serikali inahofia kukubali Watanzania kuwa na uraia zaidi ya nchi moja kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo uzalendo na usalama wa nchi.
 
Alisema kwamba katika maelezo hayo ya serikali inaonekana wazi haipo tayari kuruhusu kipengele cha uraia pacha kuingizwa katika Katiba Mpya, kitendo ambacho kitawavunja moyo Watanzania zaidi ya milioni moja wanaoishi nje ya nchi.
 
“Sikufurahishwa na kilichotokea ndani, serikali iliegemea kuelezea hasara pekee ya uraia pacha na kuacha kusema faida zake, ifahamike wazi kwamba uraia pacha una faida kubwa na nchi nyingi zinanufaika na utaratibu huu,” alisema Singo.
 
Alisema kutokana na hatua hiyo, Watanzania wengi walio nje ya nchi  watanyimwa fursa ya kushiriki kuinua uchumi wa nchi yao kikamilifu kutokana na kutotambuliwa kisheria.
 
Alifafanua kwamba katika nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zinanufaika na utaratibu huo, ambapo raia wake wanaingiza pesa nyingi nchini mwao kwa ajili ya maendeleo.
 
Alisema kwamba wapo Watanzania kati ya milioni moja hadi milioni tatu ambao wamekuwa wakiingiza nchini dola za Marekani kati ya milioni 10 hadi 37 kwa mwaka.
 
Hata hivyo, alisema endapo uraia pacha utaruhusiwa wapo tayari kuondoa baadhi ya haki hasa zinazoonekana kuathiri Usalama wa Taifa.
 
Suala hilo baada ya kukwama katika kamati, sasa litasubiri mjadala mpana ndani ya Bunge zima ambalo litajadili na kupigiwa kura kama likubalike au la.
*Imeandaliwa na Abdallah Bawazir, Moshi Lusonzo na Jacqueline Massano.
 
CHANZO: NIPASHE

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>