Na Hafsa Golo
MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar, imesema itamchukulia hatua mfanyabiashara yeyote wa vyakula na viburudishaji anaetoa huduma kwa wizara na taasisi za serikali, ambae amekuwa akitoa risiti tupu kwa wanunuzi.
Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Mussa Haji Ali alisema kufanya hivyo ni sawa na kuruhusu rushwa.
Alisema kitendo cha utoaji wa risiti tupu kwa wanunuzi kutoka taasisi za serikali, ni miongoni mwa kuhujumu uchumi na rushwa na kurejesha nyuma juhudu za serikali za kuwaletea wananchi maendelei.
Alisema katika uchunguzi wa awali wamebaini kuwepo vitendo hivyo ndani ya taasisi za serikali,ambapo wanunuzi hupewa risiti tupu na baadae hujaza kiwango cha fedha kinyume na hali halisi ya manunuzi.
Alisema tayari ameshakaa pamoja na wafanyabishara wanaotoa huduma hizo na kuwaelimisha madhara ya rushwa na kuwashauri kuacha tabia hiyo.
“Baadhi ya wanunuzi wasio waaminifu wamekuwa wakitumia fursa hiyo kujinufaisha bila ya kujali hasara serikali inayoipata,” alisema.
Baadhi ya wafanyabishara waliozungumza na gazeti hili walikiri kufanya biashara hiyo lakini baada ya kupewa elimu hiyo, sasa wataacha.