HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA MAENDELEO YA WANAWAKE NA USTAWI WA JAMII KUHUSIANA NA BAJETI YA WIZARA YA AFYA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku uhai na Afya njema na kutuwezesha kukutana tena leo hii kwa madhumuni ya kuwatumikia wananchi wetu na manufaa ya taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
Pili napenda nikushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kwa niaba ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii kuwasilisha maoni ya Kamati kuhusiana na makadirio ya mapato na matumizi ya kazi za kawaida na maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Waziri wa Afya, Naibu Waziri, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa mashirikiano yao waliyotupa wakati wa kupitia na kuichambua bajeti ya Wizara, kwa kweli mashirikiano yao yamefanikisha kumaliza kazi hii kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Sitokuwa nimetenda haki hata kidogo iwapo nitakosa kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi kuniwezesha leo hii kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kuwasilisha maoni ya Kamati juu ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa Fedha 2013/2014. Naomba niwatambue kwa kuwataja majina wajumbe wa Kamati kama hivi ifuatavyo:-
1. Mhe. Mgeni Hassan Juma Mwenyekiti.
2. Mhe. Hassan Hamad Omar M/Menyekiti.
3. Mhe. Abdi Mosi Kombo Mjumbe.
4. Mhe. Ali Salum Haji Mjumbe.
5. Mhe. Farida Amour Moh'd Mjumbe.
6. Mhe. Mwanaid Kassim Mussa Mjumbe.
7. Mhe. Mohamed Mbwana Hamad Mjumbe.
8. Ndg. Maryam Rashid Ali Katibu.
9. Ndg. Asha Said Mohamed. Katibu.
Mheshimiwa Spika, Baada ya utangulizi huo, naomba kutoa maoni ya Kamati kuhusiana na Bajeti ya Wizara ya Afya.
Jengo la Ofisi Kuu – Pemba.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imesikitishwa na hali ya Wizara ya Afya Pemba Kukosa ofisi yake. Ofisi kuu Pemba imekuwa haina jengo kwa muda mrefu na inatumia chumba kimoja kidogo kilichopo katika hospitali ya Wete; hali ambayo hairidhishi kwani chumba hicho kinakuwa hakikidhi haja kwa matumizi ya wizara nzima. Afisa mdhamini anashindwa kuwa karibu na wasaidizi wake mbali mbali kutokana na ufinyu wa Ofisi.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Serikali kutatua tatizo la Of
isi ya wizara Pemba. Kiukweli Kamati haikuridhika na hali ya ufinyu wa Ofisi kwasababu utekelezaji wa majukumu ya Wizara unakuwa ni ngumu. Upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba katika Hospitali na Vituo vya Afya Pemba.
Mheshimiwa Spika, Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni muhimu katika hospitali na vituo vya afya; lakini Kamati ilipotembelea vituo vya afya na hospitali mbali mbali ilibaini upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba. Sambamba na hilo, Kamati ilifanya mahojiano na timu nne za afya Pemba zilizopo katika Wilaya ya Micheweni, Wilaya ya Wete, Wilaya ya Chakechake na Wilaya ya Mkoani; nazo zilikiri kuwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni tatizo katika wilaya zao.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa huduma za afya na dawa, Kamati inaishauri Wizara kutafuta kampuni nyingine ya kuagiza na kuingiza dawa nchini badala ya kutegemea Ghala kuu ya Dawa ya Dar es Salaam pekee MSD (Medical Store of Dar es Saalam) ambao nao huchangia uhaba wa upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo vyetu vya afya katika muda unaotakiwa.
Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Kamati haikuridhishwa na utekelezaji wa miradi unaondeshwa na wizara. Katika bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha 2012/2013 wizara ilijipangia kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo. Kamati imebaini utekelezaji usio wa ufanisi katika programu shirikishi ya afya ya mama na mtoto, mradi wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na mradi wa kuvipandisha hadhi vituo vya huduma za afya. Malengo ya miradi hiyo hayakuweza kufikiwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Katika utekelezaji wa programu shirikishi ya afya ya mama na mtoto ambayo ilikusudia kujenga vyumba vya baridi na kufanya ukarabati wa ofisi ya chanjo Pemba, Kamati ilisikitishwa sana kuwa utekelezaji wake haukuweza kufanyika, na hakukuwa na sababu za msingi kwani fedha za wahisani ziliingizwa na kushindwa kufanyiwa kazi katika muda uliokusudiwa. Kitendo hichi ni kuwavunja moyo wahisani wetu na Kamati inamtaka Waziri atoe maelezo juu ya jambo hili.
Mheshimiwa Spika, PiaKamati inaiagiza wizarakatika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2013/2014 kuhakikisha kuwa wanafanya ujenzi wa haraka wa vyumba vya baridi pamoja na ukarabati wa Ofisi ya chanjo, kwani chanjo zote kwa upande wa Pemba zinahifadhiwa katika ofisi hiyo, kuendelea kuchelewa kufanya ujenzi kutapelekea kutokuwa na uhakika wa usalama wa chanjo zetu pamoja na wafanyakazi wanaohudumia ofisi hiyo.
Mheshimiwa Spika,katika Mradi wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, Wizara ilikusudia kufanya matengenezo katika vituo vya afya vya Mzambarauni na Wesha kwa Upande wa Pemba na kwa Unguja Kituo cha Afya Mwera. Vituo vyote hivyo vilikosa kukarabatiwa katika Kipindi husika, ukarabati uliofanyika ni wa kituo cha Afya cha Bogoa pekee ambacho utekelezaji wake ulikuwa wa tangu bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Spika, Aidha katika mradi wa kuvipandisha hadhi vituo vya huduma za afya, lengo lake lilikuwa ni kufanya utanuzi wa majengo ya Hospitali ya Kivunge na Micheweni pamoja na ununuzi wa vifaa mbali mbali kwa ajili ya utoaji mzuri wa huduma za afya katika hospitali hizo. utekelezaji wake haukuwa wa kuridhisha.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaitaka Serikali kuingizia fedha Wizara kwa Wakati ili iweze kutekeleza mipango yake iliyojipangia ikiwemoutekelezaji wa miradi kwa lengo la kuimarisha huduma za afya nchini na kuinua sekta hii muhimu.
Idara ya Utumishi na uendeshaji.
Mheshimiwa Spika katika mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ilikamilisha mpango mkuu wa mafunzo kwa wafanyakazi ambao utekelezaji wake utaanza kutumika rasmi katika mwaka huu wa fedha. Kamati inaipongeza Wizara kwa kuweza kukamilisha mpango huo muhimu ambao utasaidia katika kupunguza upungufu mkubwa wa wafanyakazi wa afya katika kada mbali mbali kwa hospitali na vituo vya afya.
Mheshimiwa Spika Katika nchi yetu tumekuwa na upungufu mkubwa wa madaktari wa magonjwa ya akili, madaktari wa X-ray, madaktari wa magojwa ya damu na madaktari wa kensa.
Kamati inaishauri Wizara katika mpango mkuu wa mafunzo kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kuwahimiza wafanyakazi watakaoenda masomoni kuchukua fani zilizokuwa pungufu katika nchi yetu na pia kuwepo na motisha maalumu kwa watakaokubali kuchukua fani hizo.
Mheshimiwa Spika, pia Kamati inaisititiza Wizara kusimamia vyema mfumo wa takwimu za rasilimali watu, mfumo ambao husaidia katika kupangia wafanyakazi sehemu za kazi kwa mujibu wa mahitaji.Wizara imekuwa inakabiliana na changamoto ya wafanyakazi wengi wa afya kutopendelea kufanya kazi vijijini na badala yake kupendelea zaidi kubakia mijini pekee.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Wizara ijitahidi kusimamia maslahi ya wafanyakazi na ihakikishe inasimamia ipasavyo mapendekezo ya rasimu ya maposho kwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika mazingira ya hatarishi na pia kuwazingatia wale wanaofanyakazi katika mazingira ya vijijini yaliyokosa huduma muhimu. Kufanya hivyo kunaweza kuwavutia wafanyakazi wetu kubakia katika ajira na kupunguza idadi kubwa ya wafanyakazi wanaokimbia kufanya kazi vijijini na katika nchi yetu kwa jumla.
Idara ya Sera, Mipango na Utafiti.
Mheshimiwa Spika, Kamati inapongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na idara katika mchakato mzima wa kuanzisha bima ya afya kwa wananchi. Kiukweli bima hiyo ni muhimu na itawasaidia wananchi kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya kila watakapokuwa wanasumbuliwa na maradhi mbali mbali.
Mheshimiwa Spika, Kumekuwa na wananchi ambao hushindwa kuhudhuria katika hospitali na vituo vya afya kutokana na kushindwa kumudu gharama za afya. Kamati ina matumaini makubwa kwamba kuanzishwa kwa bima ya afya kutawawezesha wananchi walio wanyonge kufaidika na huduma za afya kwa kadri watakavyokuwa wanazihitajia.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaisisitizaWizara kuendelea na hatua mbali mbali zinazohusiana na kukamilika kwa bima hiyo na pia kuandaa utaratibu mzuri ambao utapelekea kupatikana kwa huduma kwa wepesi na kunufaisha wananchi wote.
Idara ya Kinga na Elimu ya Afya.
Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa majukumu ya Idara ni kukinga na kukabiliana na maradhi ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza. Katika miaka ya hivi karibuni, katika visiwa vya Zanzibar kumekuwa na ongezeko kubwa ya magojwa yasio ya kuambukiza ikiwemo shindikizo la damu, kisukari, saratani na magojwa mengine sugu ya mapafu kama vile pumu.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Wizara kwa kuweza kufanya utafiti katika hospitali nne za vijiji na hospitali tatu za Wilaya na kuweza kubaini hali halisi ya magojwa na kutambua mahitaji ya taaluma, vitendea kazi na rasilimali watu.
Mheshimiwa Spika, Kitengo cha kupambana na magojwa yasio ya kuambukiza kinaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na magojwa hayo na Kamati inaisisitiza wizara, pamoja na kuwepo kwa kitengo, kuendelea kuusimamia muongozo wa matibabu ya magojwa yasioambukiza ili uweze kukamilka na kuanza kutumika.
Mheshimiwa Spika, Aidha kwa upande wa maradhi ya malaria,Kamati inapenda kuipongeza Wizara kwa jitihada wanayoendelea kuchukua ya kudhibiti maradhi hayo. Kamati iliweza kujionea wenyewe kisiwani Pemba shehia ya Tumbe kuwa ugojwa wa malaria katika kijiji hicho umeweza kutokomezwa. Kamati inaiomba Wizara kuendelea na juhudi ya kudhibiti maradhi ya malaria ili yasije yakaibuka tena kwa kuendela kutoa elimu ya kinga ya maradhi hayo.
Mheshimiwa Spika, Kamati ina matumaini makubwa kuwa Idara itaendelea kufanya vizuri katika majukumu yake mbali mbali kutokana na ongezeko la bajeti kutoka milioni mia mbili thalathini na moja (231,000,000) katika mwaka wa fedha 2012/2013 mpaka kufikia milioni mia tatu hamsini (350,000,000) katika mwaka huu wa fedha.
Idara ya Tiba.
Mheshimiwa Spika, Idara hii inajumuisha hospitali za Wilaya na Vjiji na pia inasimamia mradi wa kupandisha Hospitali za vijiji na wilaya. Kiujumla hospitali zetu zinakabiliana na changamoto za msingi ikiwemo hali mbaya ya upatikanaji wa dawa na vifaa, uchakavu wa majengo, uchache wa wafanyakazi, kuwepo kwa madeni makubwa ya maji na umeme, kukosekana kwa uzio katika vituo vya afya, walinzi nakadhalika.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaitaka Serikali kuisadia wizara katika kukabiliana na changamoto hizi.Kamati imeweza kushuhudia uchakavu na ufinyu wa majengo katika hospitali zetu za vijiji na wilaya. Kwa upande wa hospitali ya vitongoji Pemba, maabara, wodi na nyumba za madaktari zimekuwa ni chakavu na hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa sio mzuri.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaona kama kweli ile adhma ya Serikali ya kuzipandisha hospitali za vijiji kuwa za wilaya, na zile za wilaya kuwa za mkoa inafikiwa lazima Serikali ihakikishe inaongeza fedha, majengo, vifaa na vitendea kazi katika hospitali hizo.
Mradi wa Kuimarisha Huduma za Afya Wilayani.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huu unategemea ufanisi mkubwa wa Timu za afya za wilaya pamoja na mfumo ulioanzishwa na Wizara wa kuendesha kazi za timu za wilaya ambapo mfuko maalum wa pamoja wa fedha( District Health Services Basket Fund) hutumika katika kuwapatia fedha timu hizo.
Mheshimiwa Spika, Kamati imegundua kuwa utaratibu unaotumika wa kuwapatia fedha timu za Afya za wilaya bado haujafahamika kwa timu zewenyewe na hivyo kupelekea timu hizo kukosa fedha kwa wakati. Kamati inaiomba Wizara kuendelea kutoa elimu juu ya mfumo ulioanzishwa ili maafisa wa timu za afya za wilaya wapate fedha kwa wakati na pia wapewe madaraka ya kuzitumia fedha kwa kufanikisha kazi zao.
Mheshimiwa Spika, timu za afya za wilaya zimeweza kufikia vituo mbali mbali vya afya na kuona utekelezaji wa huduma zinazotolewa katika vituo. Mbali na jitihada za kufikia vituo hivyo, timu hizo ziliweza kugundua changamoto zilizopo kama ufinyu wa vituo, upungufu wa wafanyakazi, kukosekana kwa uzio katika vituo, madeni makubwa ya umeme na maji, matokeo ya uvamizi na wizi na ukosefu wa vifaa tiba.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Serikali kuisaidia wizara katika kuzitafutia ufumbumbuzi changamoto hizo ili hatimae huduma za afya za wilayani ziweze kuimarika.
HITIMISHO:
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya kwa bajeti ya mwaka 2012/2013 imepata mafanikio katika baadhi ya maeneo huku ikiwa bado baadhi ya maeneo yanahitaji kufanyiwa kazi. Kamati yetu kiujumla haijaridhika kabisa na uingizwaji wa fedha katika Wizara ya Afya kwa matumizi ya kazi za kawaida na kazi za maendeleo. Uingizwaji wa fedha usioridhisha unaendelea kuikwamisha wizara katika kutekeleza majukumu yake. Hivyo Kamati inaiomba Serikali kuipa kipaumbele wizara kwa kuingizia fedha ipasavyo ili iweze kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, nawaomba wajumbe wenzangu wa Baraza lako Tukufu, kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2013/2014 Jumla ya Tshs 21,318,000,000 (Bilioni ishirini na moja na milioni mia tatu kumi na nane) kwa kazi za kawaida, Ruzuku, Mishahara na maposho na Tshs 6,333,000,000( bilioni sita, milioni mia tatu na thalathini na tatu)kwa kazi za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana kwa kunisikiliza na kwa niaba ya Kamati naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Ahsante.
..............................
Mhe. Hassan Hamad Omar
Kny:Mwenyekiti,
Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii.
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.