TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 16/8/2013
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa mara nyengine tena tunawakaribisha sana katika Afisi ya Baraza la Wawakilishi, na kabla ya yote, tunapenda kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kwa mashirikiano mnayoendelea kutupa kwa kututolea taarifa zetu kwa wananchi kuhusiana na shughuli mbali mbali zinazohusiana na Chombo chetu hiki cha Baraza la Wawakilishi.
Kwa kweli mchango wenu umekuwa ukitupa faraja kubwa na tunakuombeni muendelee kuwa karibu nasi kwa lengo lile lile la kuwapatia wananchi taarifa muhimu zinazohusiana na Baraza la Wawakilishi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kufuatia mabadiliko ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi kuelekeza Miswada kusomwa kwa mara tatu , imeshauriwa baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza na kabla ya kujadiliwa na Kamati husika, itangazwe kwa wananchi ili waifahamu Miswada hiyo na waweze kushiriki na kutoa maoni yao.
Miswada minne tayari imeshasomwa kwa mara ya Kwanza katika Mkutano uliopita yaani Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza hili la Nane na itajadiliwa katika mkutano ujao wa Oktoba.
Miswada yenyewe ni kama ifuatayo:-
- Mswada wa Sheria ya Kufuta na Kuandika Sheria inayohusu Kampuni na Jumuiya nyengine Kuweka Masharti Madhubuti zaidi ya Uratibu na wa Kampuni, Jumuiya na Mambo yanayohusiana na hayo.
- Mswada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria mbali mbali za Ardhi na mambo yanayohusiana na hayo.
- Mswada wa Sheria ya Kufuta na Kuweka Sheria ya Biashara ya Zanzibar No. 4 ya 1989 na Kuweka Vifungu vya Kuimarisha Biashara Zanzibar na Mambo yanayohusiana na hayo.
- Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya Marekebisho ya usimamizi wa Utoaji wa Leseni za Biashara na Mambo yanayohusiana na hayo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Pamoja na kwamba Kamati zinazohusika na Miswada hii zinakusudia kualika wadau wakati wa kuchambua Miswada hiyo , Afisi ya Baraza la Wawakilishi inapenda kutumia fursa hii kuwaomba wananchi, taasisi na makundi mbali mbali kutoa michango na maoni yao kuhusiana na Miswada hii, na tunaamini kwamba maoni hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika Kamati zitakazochambua Miswada hiyo Kabla ya Kusomwa kwa mara ya Pili katika Baraza la Wawakilishi.
Tunawasisitiza sana wananchi kuitumia fursa hii muhimu ambapo lengo ni kupata mawazo mengi zaidi kutoka pande mbali mbali na hatimae kupata Sheria zenye ubora na matakwa ya wananchi.
Nakala za Miswada hii zinapatikana katika Afisi ya Baraza la Wawakilishi Chukwani, na tovuti ya Baraza La Wawakilishi www.zanzibarassambly.go.tz na maoni yote yaletwe katika Afisi ya Baraza la Wawakilishi Chukwani kwa Unguja, na Wete kwa Pemba. Aidha maoni hayo yanaweza pia kutumwa kwa kupitia Sanduku la Barua 902, Zanzibar au kwa Njia ya barua pepe zahore@zanlink .co.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mwisho tunapenda kuwaahidi kwamba Baraza la wawakilishi litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uwazi ili kila mwananchi afahamu kinachoendelea kwa lengo la kuendeleza utawala bora hapa nchini.
Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mara nyengine tena napenda niwashukuru kwa dhati kabisa kwa kazi yenu ambayo sisi kama Baraza tunaithamini sana na kwa kiasi kikubwa inachangia kueneza Taaluma muhimu kwa maendeleo ya wananchi wetu.
Ahsante sana kwa kunisikiliza.
Imetolewa na
………………………..
(Yahya Khamis Hamad),
Katibu,
Baraza la wawakilishi,
Zanzibar.