Na Salama Salim, ZJMMC Pemba
WAKULIMA wa zao la mwani katika kijiji cha Tumbe wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba, wanaendelea kukaa na mwani wao majumbani, baada ya kampuni ya Sea Weed, kusitisha kununua zao hilo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijiji huko, juu ya ukosefu wa soka la kuuzia mwani wao, wakulima hao walisema kwa sasa wanalia njaa baada ya kampuni hiyo kusitisha ununuzi.
Walisema ni muda wa miezi mitatu sasa tokea kampuni hiyo ilipoingia mitini jambo ambalo limekuwa likiwakosesha usingizi hasa kwa vile tayari wanao mwani mwingi wa kuuza kwa kampuni hiyo.
Walisema ukosefu wa soko unawatiwa hofu na unasababisha kuishi maisha ya kubahatisha.
Mmoja kati ya wakulima hao, Abdallah Haji Juma alisema ana kiwango kikubwa cha mwani nyumbani mwake, unaofikia magunia nane.
Nae Raya Salim Ali alisema kutokana na kutonununuliwa kwa zao hilo kwa kipindi hichi chote, hali ya maisha imekuwa ngumu.
‘’Ilikuwa maisha yanakwenda vizuri maana hata kwa mahitaji yetu madogo madogo sio lazima kumsubiri baba, ilikuwa tunajikumu lakini kwa sasa tumedorora,” alisema.
Mkulima mwengine wa zao hilo, Salama Juma Ali, alisema zao la hilo kwa sasa limekuwa vigumu kuendelezwa kwani kampuni inayonunua zao hilo haijawapitia wakulima kwa kipindi chote hicho.
Meneja wa Seaweed Cooperation,Hamial Said Soud, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema walisitisha kutokana na kuwa na mwani mwingi kwenye maghala yao.