Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Maseneta wa Marekani wafika Zanzibar kukagua miradi wanayoifadhili

$
0
0
Na Salum Vuai, Maelezo
WIZARA ya Afya Zanzibar, imeelezea kuridhishwa na misaada mbalimbali ya kiafya inayotolewa na Marekani na taasisi nyengine binafsi za nchi hiyo.

Naibu Waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya, ameueleza ujumbe wa wasaidizi wa Maseneta kutoka Marekani uliomtembelea ofisini kwake jana, kuwa mchango wa nchi hiyo umesaidia sana kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Unguja na Pemba.

Ujumbe huo umewasili jana kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Marekani na mashirikia mingine ya misaada ya nchi hiyo katika sekta ya afya. 

Dk. Sira alisema, misaada inayotolewa na nchi hiyo kwa Zanzibar, imekuwa na mchango mkubwa katika jitihada za  serikali kuhakikisha huduma za afya kwa wananchi zinakuwa bora pamoja na kuviimarisha vituo vya afya mijini na vijijini. 

Alifahamisha kuwa kupitia miradi hiyo, huduma za afya ya mama na mtoto ikiwemo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi zimekuwa nzuri kulinganisha na siku zilizotangulia. 

Aidha, alisema kufanikiwa kwa mradi wa kupambana na ugonjwa wa malaria unaofadhiliwa na taasisi ya Clinton Foundation inayoongozwa na Rais mstaafu wa Marekani Bill Clinton, ni kielelezo cha faida itokanayo na juhudi za nchi hiyo.

Kwa upande wa maambukizi ya virusi vinavyosababisha UKIMWI, Naibu Waziri huyo alisema kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wananchi kujitokeza kupimwa afya zao na kupatiwa ushauri nasaha. 

Alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la watu kupima afya zao kwa ajili ya kuangalia maambukizi hayo, kutoka watu 13,000 mwaka 2005 na kufikia 80,000 mwaka 2013.

Aidha alieleza ingawa vijana wanaotumia dawa za kulevya wanaendelea kujidunga sindano, lakini wamepata uelewa mkubwa na kuacha kutumia sindano moja kwa watu wengi, na hivyo kusaidia kupunguza maambukizi ya maradhi ya UKIMWI. 

"Mbali na mafanikio hayo, pia misaada ya Marekani imetuwezesha kusambaza elimu kwa wananchi juu ya mambo mbalimbali ya afya, ikiwemo kuwahamasisha akinamama wajawazito kujifungulia nyumbani, na wengi wameitikia wito huo", alisema.

Alieleza matumani yake kuwa, katika ziara yao wajumbe hao wataona na kuridhishwa na hatua iliyopigwa, ili ziara yao iwe chachu kwa Zanzibar kuendelea kunufaika na misaada ya Marekani.

Alisema serikali ya Zanzibar inathamini uhusiano mzuri na wa karibu kati yake na Marekani, kwani umelenga kustawisha hali za wananchi wa pande hizo na kuzidi kushirikiana.

Naye Naibu Mkurugenzi wa taasisi ya Path Finder International Dk. Pasien Stephen Mapunda kutoka Tanzania ambaye anafuatana na ujumbe huo, alisema ziara yao itawafikisha katika hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja kujionea maendeleo yaliyofikiwa. Maeneo mengine watakayofika ni baadhi ya nyumba za kubadilisha tabia kwa vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya (Sober Houses), Zayedesa na 'Key Population Network iliyoko Miembeni mjini Zanzibar, na makundi kadhaa hatarishi.    

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>