Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

DK. SHEIN AKABIDHIWA DIGRII YA HESHIMA YA COPECSA

$
0
0
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                      26 Septemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekabidhiwa rasmi digrii ya heshima ya Chuo cha Wataalamu wa Patholojia cha Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika(COPECSA).
 Digrii hiyo alitunukiwa katika mahafali ya kwanza ya COPECSA yaliyofanyika mjini Arusha mwezi Agosti, 2014 akiwa mwanzilishi wa Chama cha Wataalamu wa Patholojia cha Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (APECSA) aliyetoa mchango wa kipekee.
 Kwa hivyo digrii hiyo imetolewa kumtambua Dk. Shein kuwa ni mwanataaluma wa fani hiyo na pia kwa mchango mkubwa wa siku nyingi katika kukuza na kuimarisha fani hiyo katika ukanda huu wa Afrika.
 Mkuu wa Chuo hicho Profesa Ephata Kaaya ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili (MUHAS) alimkabidhi Dk. Shein digrii hiyo katika sherehe fupi iliyofanyika Ikulu.
 Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa digrii hiyo, Dk. Shein aliishukuru Sekretarieti ya Chuo hicho kwa heshima iliyompa na kueleza kuwa si jambo alilolitarajia maishani mwake kupata heshima kama hiyo.
 Kwa hivyo aliahidi kuendelea kuwa karibu na chuo hicho na kueleza utayari wake kuendelea kufanya kazi na chuo kukuza taaluma ya uchunguzi wa magonjwa.
 Alibainisha kuwa kitendo cha kumpa digrii hiyo kimemuongezea nguvu na kueleza kuwa daima milango yake iko wazi kwa uongozi wa chuo kukutana nae kwa mashauriano kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya chuo hicho.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliipongeza sekretarieti ya Shirika la Afya la Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HCS) kwa kuanzisha Chuo mama cha kusimamia vyuo vya fani mbali mbali za afya kama hiyo ya Patholojia.
 Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Profesa Kaaya kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili na kuuelezea uteuzi wake kuwa ni jambo la heri kwake kukitumikia chuo hicho katika nafasi hiyo mpya.  
 Kwa upande wake Profesa Kaaya Chuo alisema heshima hiyo aliyopewa Dk. Shein haitokani na nafasi aliyonayo sasa bali yeye kama mwana taaluma wa fani hiyo pamoja na mchango wake mkubwa wa miaka mingi katika fani hiyo.

 Profesa Kaaya alieleza kuwa sekretarieti imefurahishwa sana na mchango wake wa hali na mali na kutambua dhamira yake ya kukisaidia chuo pamoja na kuwa nafasi yake kufanya hivyo imekuwa finyu kutokana na majukumu aliyonayo sasa.  
 Hata hivyo alimueleza Dk. Shein kuwa chuo kitaendelea kumpa taarifa mbalimbali zinazohusu maendeleo yake na fani ya taaluma ya magonjwa ili aendelee kutoa mchango wake katika kukuza taaluma hiyo kadri atakavyoweza.
 Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Shrika la Afya kwa Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika lenye Makao Makuu yake jijini Arusha, Profesa Yoswa Dambisya, Rais aliyemaliza muda wake wa Chama cha Wataalamu wa Magonjwa wa Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (APECSA) Dk. Edda Vuhahula ambaye pia ni Mweka Hazina wa Chuo pamoja na Afisa Utawala wa Chuo Bwana Austin Makani.
 Dk. Shein mbali ya kuwa mtaalamu wa Patholojia lakini pia amekuwa mwanachama wa Chama cha Wataalamu wa Patholojia cha Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (APECSA) kwa miaka mingi.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>