Na Hamida Maulid {ZJMMC}
Wananchi wa Shehia ya Kombeni Wilaya ya Magharibi wameilalamikia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutokana na tatizo la maji linaloendelea kuwakabili kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa na kusababisha kuzorotesha harakati zao za kiuchumi.
Wakizungumza na waaandishi wa habari wananchi wa shehia hiyo, wamesema upungufu maji katika vijiji vingi vya shehia hiyo na kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wengi.
Wamesema maji yamekuwa yakipatikana kidogo sana na baadhi ya vijiji hayatoki kabisa na wamevitaja vijiji hivyo kuwa ni Kombeni hospitali, Kombeni branji na Komboni michenzani.
“Maji yanatoka kiduchu kiduchu sisi hatupati, na tukipata ni kidogo sana na kwa muda mdogo na hayana muda maalumu”. alifahamisha mwanakijiji wa Kombeni branji bi. Afua Abdalla kwa masikitiko.
Sheha wa shehiya ya Kombeni Mussa Khamis Mussa amesema tatizo la maji lipo kwa muda mrefu na linawakabili baadhi ya wananchi wake licha ya juhudi aliyofanya ya kuwafuata maafisa wa ZAWA ili kutatua ufumbuzi wa tatizo hilo.
Sheha Mussa amesema amewafuata wahudumu wa maji katika kisima cha Dimani ambacho ndicho wanachotumia na kuelezwa kwamba mashine inayo tumika katika kisima hicho hivi sasa ni moja tu na yapili imeharibika na ndio ililiopelekea upungufu wa maji katika shehia hiyo.
Kutokana na kasoro hizo sheha ameiomba Mamlaka ya Maji Zanzibar kuwasaidia mabomba mengine ya maji ili kuyafunga katika kisima chengine cha Kombeni kwa ajili ya kupunguza tatito hilo la muda mrefu.
Hata hivyo Afisa uhusiano wa ZAWA Zahor Suleiman Khatib amekanusha kuharibika kwa mashine katika kisima cha Kombeni na wamesema kisima hicho kina mashinei tatu na zote zinafanya kazi.
Zahor amewatupia lawama wananchi wanaounga maji kiholela bila kufuata taratibu za Mamlaka na baadhi ya wakulima wanaotumia maji mengi kumwagilia mashamba yao jambo ambalo linapelekea ukosefu wa maji katika baadhi ya vijiji.