Na Mwantanga Ame
Serikali imesema migogoro inayojitokeza katika sekta ya afya kutokana na kuwepo wadau wengi, ndio sababu ya kuanzisha sheria mpya ya wauguzi na wakunga, ambapo mswada wake uliwasilishwa jana.
Waziri Afya, Mhe. Rashid Seif, alisema hayo jana wakati akiwasilisha mswada huo, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi.
Alisema sekta ya afya kumekuwa na wadau wengi walioamua kujiunga pamoja nao, lakini kulikuwa na migogoro iliyokuwa ikijitokeza kwa taasisi hiyo, hivyo serikali inapanga kuiondoa.
Alisema sheria hiyo mpya itatoa fursa ya kuwatambua waunguzi katika sekta ya umma na binafsi, kwani mabadiliko ya sekta ya afya ni kukuza utoaji huduma kwa wananchi.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleao ya Wanawake na Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi, Mhe. Mgeni Hassan Juma, alisema mabadiliko ya kiuchumi, ongezeko la watu na kutanuka taaluma ya uuguzi na ukunga, kumesababisha kufutwa sheria ya zamani ili kwenda na wakati.
Alisema baraza la wauguzi, litazingatia maadili ya wauguzi na wakunga na kuleta ufanisi zaidi kwa vile litasimamia kikamilifu utendaji wa taasisi hizo.
Wakichangia mswada huo, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wameitaka serikali kuviangalia baadhi ya vipele viliomo ndani ya mswada huo.
Mwakilishi wa Chambani, Mhe. Mohammed Mbwana Hamad, alisema kifungu 15(3) kinachoelezea masharti ya mtu anaetoka nje ya nchi kutaka kusajiliwa, kimeweka masharti yanayoweza kusababisha udanganyifu kwa baraza litakaloundwa kusimamia sheria hiyo.
Alisema kifungu 15 (3) (a) kimeeleza mtu atakaetoka nje ya nchi atalazimika kuwasilisha ushahidi utakaoliridhisha baraza kuwa amesajiliwa na anastahiki kusajiliwa kuwa muuguzi au mkunga katika nchi yake na kifugu kidogo cha (b) kinamtaka mtu huyo kuwasilisha ushahidi kuwa amehitimu na kufaulu mafunzo ya uuguzi.
Alisema hofu yake ipo zaidi katika kifungu cha 4 ambacho kinaeleza pindipo ikitokea kutokuwepo kwa lolote kati ya yalioelezwa katika kifungu kidogo cha (a) na (b) na kifungu kidogo cha (3), baraza hilo litamfanyia mtihani na muombaji naye atapaswa kufaulu mtihani huo.
Alisema hiyo ni kasoro inayoweza kutumiwa vibaya na wageni watakaotaka kufanya kazi za aina hiyo nchini kwani wanaweza kutumia mwanya huo kufanya udanganyifu katika vyeti.
Alisema serikali inapaswa kuchukua tahadhari hiyo, kwa sababu baadhi ya watu wana uwezo wa kutumia mitandao kutengeneza vyeti bandia.
Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, baraza hilo linatakiwa kuwa na sifa za ziada katika uthibitishaji wa wanaoomba kufanya kazi hiyo.
Naye Mwakilishi wa Kiwani, Mhe.Hija Hassan Hija, alisema atakuwa mgumu kupitisha mswada huo kama haujaelezea wazi hadhi watakayopewa wakunga wa jadi.
Alisema wakunga wa jadi bado wana hadhi na haiwezekani kutohusishwa ndani ya sheria hiyo kwa vile wanaendelea kufanya kazi hiyo.
Mhe. Mwakilishi wa Wanawake, Mhe. Asha Bakari Makame, alisema mswada huo utaondoa matatizo mengi yanayowakabili wafanyakazi wa sekta ya afya.
Wanu Hafidh Ameir, aliiomba serikali kufikiria kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuwapatia vifaa wauguzi.
Mwakilishi wa Kitope, Mhe. Makame Mshimba Mbarouk, aliwataka watendaji wa taasisi hiyo kutumia vyema sheria hiyo, kwa kuwa imejengeka tabia ya kuziweka makabatini sehria badala kuzitumia.
Mapema Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Pandu Ameir Kificho, alimuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Said Hassan Said, na kuwaomba wajumbe kumpa ushirikiano.
Alisema uteuzi wa Mwanasheria huyo utasaidia shughuli za baraza hilo na wako tayari kushirikiana nae.
Wajumbe wa Baraza hilo walisimama kwa dakika moja kuomboleza kifo cha aliyekuwa Spika wa pili wa baraza hilo, Ali Khamis, aliyefariki dunia Septemba 8, mwaka huu akiwa na miaka 100.