HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA KUMI NA SABA WA BARAZA LA WAWAKILISHI, ZANZIBAR.
TAREHE 31 OKTOBA, 2014
UTANGULIZI:
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutukutanisha hapa tukiwa katika hali ya uzima na afya njema na kufanikiwa vizuri kushiriki katika Mkutano huu wa Kumi na Saba wa Baraza la Wawakilishi.
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mhe. Said Hassan Said kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kuteuliwa kwa Mhe. Said kunaonyesha imani kubwa ambayo Mheshimiwa Rais anayo juu yake, hasa kutokana na uzoefu wake na uwezo wake mkubwa wa kuchapa kazi. Tunamtakia kila la kheri na mafanikio mema katika kazi yake hiyo mpya. Tunakuhakikishia ushirikiano wetu kila wakati.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa, niruhusu nitoe shukurani zangu za dhati kwako wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti na wasaidizi wako wote kwa kuendelea kuliendesha Baraza hili Tukufu kwa busara na umakini mkubwa. Pia nawashukuru Waheshimiwa Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati mbali mbali wa Baraza hili kwa busara zao katika kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, pongezi maalum nazitoa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuendelea kuiongoza nchi yetu kwa hekima, busara na uadilifu mkubwa. Aidha, nachukua fursa hii kumpongeza Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuendelea kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi, Mawaziri, Naibu Mawaziri kwa umahiri wao mkubwa katika kuchangia mijadala mbali mbali ndani ya Baraza hili. Aidha, nawashukuru Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, pia navipongeza vyombo vyahabari vya hapa Zanzibar, hususan Shirika la Habari la Zanzibar (ZBC) kwa kuwapasha habari mbali mbali wananchi wetu kwa kupitia redio, TV na magazeti. Hali ambayo ilipelekea urahisi kwa wananchi kufuatilia kwa makini matukio yote yaliyojiri Barazani. Vile vile, nawapongeza wakalimani wetu wa lugha ya alama kwa kazi nzuri walioifanya ya kutafsiri mawasilisho na mijadala katika kipindi chote cha kikao hikina kuwawezesha wananchi wenzetu wenye ulemavu wa kusikia kufuatilia shughuli za Baraza kwa ukamilifu.
Mheshimiwa Spika, mwisho navipongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama pamoja na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wao mkubwa katika kudumisha amani, usalama na utulivu uliopo hapa nchini.
MASUALA MUHIMU YALIYOJIRI NCHINI
Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba nchi yetu inaendelea na mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo kwa sasa katiba inayopendekezwa tayari imekabidhiwa kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein. Makabidhiano hayo yalifanyika katika uwanja wa Jamhuri huko Dodoma, tarehe 8 Oktoba, 2014.
Mheshimiwa Spika, kutokana na tukio hili kubwa la kihistoria katika nchi yetu, hatuna budi kuwapongeza viongozi wetu hawa kwa kuanzisha na kufanikisha kupata Katiba Inayopendekezwa kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawanasihi wananchi wote kupata muda wa kuisoma kwa kina katiba hiyo inayopendekezwa ili kuielewa na hatimaye kutumia haki yao ya kidemokrasia kushiriki katika zoezi la upigaji kura ya maoni wakati muda utakapofika.
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nachukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mheshimiwa Samuel John Sitta na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna walivyoliendesha Bunge hilo Maalum kwa ufanisi na mafanikio makubwa. Pia, nawapongeza wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba walioshiriki katika kuandaa Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu inajivunia hazina kubwa aliyotujaalia Mwenyezi Mungu ya amani na utulivu tulionao ambao ni nyenzo kubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Hivyo, hatuna budi sote kwa pamoja kuilinda na kuidumisha hazina hiyo kwani amani ikivurugika hakuna hata mmoja miongoni mwetu atakaebaki salama. Serikali itaendelea kwa juhudi zake zote kusimamia amani na utulivu tulionao na ni vyema viongozi na wananchi tukatoa ushirikiano katika kufanikisha azma hii.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo bado inaendelea kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa moja katika kujikimu kimaisha, kuwa na uhakika wa chakula, lishe na afya za wananchi walio wengi vijijini na mijini. Takriban zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hii kwa kuendeleza maisha yao. Kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sekta hii ilichangia wastani wa asilimia 30 ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwa Msimu wa Kilimo cha Mpunga cha Masika 2013/2014, jumla ya ekari 30,444 (Unguja 12,548 na Pemba 17,896) zililimwa katika maeneo ya juu, sawa na asilimia 87 na ekari 1,736 zililimwa katika maeneo ya umwagiliaji maji (Unguja ekari 1,143.61 na Pemba ekari 592.8) sawa na asilimia 88 ya lengo lililowekwa.
Mheshimiwa Spika, katika msimu huo, jumla ya tani 21,895 za mpunga zimevunwa katika maeneo ya juu (tani 14,354 Pemba na Tani 7,541 Unguja) na tani 2,070 za mpunga katika maeneo ya umwagiliaji maji (Unguja tani 1,302 na Pemba tani 768) zilivunwa.
Kupungua kwa uzalishaji wa mpunga katika msimu ulioainishwa umetokana na uvamizi wa viwavi jeshi hasa katika mkoa wa Kaskazini Unguja na kupungua kwa maeneo ya ukulima wa mpunga ekari 3,400 (Upenja ekari 700 na Mahonda ekari 2,700) kwa maeneo ambayo yanamilikiwa na Kiwanda cha Sukari cha Mahonda ambapo tayari mashamba hayo yamepandwa miwa kwa ajili ya uzalishaji wa Sukari.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuliendeleza eneo la hekta 2,410 Unguja na Pemba kwa ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji maji kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini na Serikali ya Marekani. Utekelezaji wa mradi huu mkubwa utasaidia sana katika kuendeleza kilimo cha mpunga kwa uhakika na kuongeza uzalishaji na hivyo kuwaongezea kipato wakulima wetu na kuchangia katika kupunguza umasikini.
Mheshimiwa Spika, matayarisho ya uzalishaji wa zao la mpunga kwa kipindi cha 2014/2015 yamefikia hatua ifuatayo:
·
Serikali imeweza kununua matrekta 20 kutoka SUMA JKT pamoja na kuyafanyia matengenezo matrekta 24 makongwe ambayo tayari yameanza kazi ya ukulima katika kwa msimu wa kilimo cha mpunga 2014/2015. Lengo ni kuweza kulima eneo la ukubwa wa ekari 32,100 (Unguja 12,901 na Pemba 19,199).
· Kwa upande wa pembejeo Serikali imefanya zabuni ya ununuzi wa mbolea tani 750 (Urea tani 600 na TSP tani 150), dawa ya kuulia magugu lita 15,000 pamoja na mbegu ya mpunga tani 150.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali zetu, Serikali imekamilisha mapitio ya Sera na Sheria ya Misitu pamoja na Mpango wa muda mrefu wa matumizi ya maliasili. Aidha, juhudi za kuendeleza zao la karafuu nchini zinaendelea kwa matayarisho ya uzalishaji wa miche ya mikarafuu 650,000 katika vitalu vya Serikali na watu binafsi na hatimae kuisambaza kwa wakulima katika msimu ujao wa masika 2014/2015.
Mheshimiwa Spika, katika kuiendeleza Sekta ya Mifugo, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji bora. Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2014, jumla ya wafugaji 5,432 wamepatiwa elimu hiyo kupitia vikundi vya wafugaji, mashamba darasa ya mifugo na mfugaji mmoja mmoja.
Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka tani 8,118,519 hadi tani 8,397,540 na uzalishaji wa mayai umeongezeka kutoka mayai 40,924,594 hadi mayai 49,900,389 kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2014. Aidha, huduma za upandishaji ng’ombe kwa sindano zinaendelea kuimarika na upatikanaji wa mbegu za kupandishia ng’ombe si tatizo tena kwa wafugaji.
Mheshimiwa Spika, kuhusu migogoro ya ardhi bado Serikali inaendelea kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo. Hali halisi inaonesha kwamba migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na wananchi wenyewe. Kesi nyingi zilizopo zinatokana na migogoro ya mipaka, uvamizi wa ardhi na mauziano yasiyo rasmi. Baadhi ya migogoro inasababishwa na muingiliano wa majukumu miongoni mwa taasisi na mamlaka zinazosimamia masuala ya ardhi katika utoaji wa vibali usiozingatia masharti na miongozo ya matumizi ya ardhi inayotolewa katika ngazi mbali mbali zikiwemo Halmashauri za Wilaya, Madiwani pamoja na Masheha. Aidha, kuna baadhi ya migogoro inasababishwa na watendaji wasio waaminifu ambao humilikisha na hata kushiriki katika mauziano ya ardhi yasiyo rasmi hali ambayo inapelekea wananchi kuuziana zaidi ya mara moja.
Mheshimiwa Spika, idadi ya kesi zinazowasilishwa katika Mahakama ya Ardhi zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku na hili linatokana na hali halisi ya ufinyu wa ardhi katika visiwa hivi vya Zanzibar ukilinganisha na ongezeko kubwa la watu ambalo linaenda sambamba na ongezeko la harakati za kiuchumi na kijamii. Pamoja na kwamba idadi ya kesi zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka lakini kasi ya usikilizaji na utolewaji wa maamuzi nayo kwa kiasi kikubwa imeongezeka. Kwa mfano mwaka wa fedha 2011/12 jumla ya kesi 188 zilifunguliwa kwa Unguja na Pemba na kwa mwaka 2013/14 kesi zilizofunguliwa ni 210.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudiakukabiliana na hali hii kwa kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi inapungua au kumalizika kabisa. Ili kuhakikisha hilo linafanikiwa Serikali inajipanga katika kutekeleza mikakati ifuatayo:
- Kutoa elimu kwa wananchi kufuata taratibu na miongozo ya ardhi hasa katika umiliki na ujenzi wa nyumba.
- Kukamilisha maandalizi ya Sera ya Ardhi ambayo hivi sasa ipo katika hatua za mwisho.
- Kuimarisha zoezi la utambuzi na Usajili wa Ardhi ili kuepusha migogoro ya ardhi.
- Kuandaa Mpango Mkuu wa Taifa wa matumizi ya ardhi ambao utawezesha wananchi kutumia ardhi kwa kuzingatia miongozo imara.
- Kuzipitia tena na kuzifanyia marekebisho Sheria za Ardhi ikiwemo Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 1959.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeongeza idadi ya Mahakimu wa Mahakama ya Ardhi kutoka watatu hadi watano na kuongeza idadi ya wakadiriaji (assessors) kutoka 11 hadi 26. Hali hiyo imepelekea kuimarika kwa Mahakama hiyo kiutendaji. Vile vile, juhudi zinazoendelea hivi sasa za kupatikana majengo kwa ajili ya Mahakama za Ardhi katika ngazi za Mikoa zitaimarisha zaidi utendaji wa Mahakama.
Mheshimiwa Spika, dira ya Serikali kuhusu Sekta ya Mifugo na Uvuvi ni kuibadililisha Sekta ya Mifugo na Uvuvi kutoka katika mfumo wa uzalishaji wa kujikimu hadi kufikia kilimo cha biashara ifikapo mwaka 2020. Azma hiyo, itafikiwa kwa mkakati wa kuimarisha hali ya uchumi na kijamii kwa jamii za wafugaji na wavuvi kwa kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji, kutoa huduma za ugani, kuongeza thamani na upatikanaji wa taarifa za masoko ili kuongeza uzalishaji na kipato.
Mheshimiwa Spika, hali ya sekta ya mifugo na uvuvi nchini inaendelea kuimarika siku hadi siku kutokana na kukua kwa soko la ndani, linachangiwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya soko la utalii nchini ambalo ni mtumiaji mkubwa wa bidhaa za mifugo na samaki, sambamba na ongezeko la watu mijini. Hali hii imesababisha wananchi kuendelea kujiajiri katika sekta hizi hasa vijana kutokana na tija zake.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mnasaba huo, mwelekeo wa Serikali hivi sasa ni kutatua changamoto muhimu zilizopo ili kuweza kutoa matokeo makubwa sasa (Big Results Now). Hizo ni pamoja na hizi zifuatazo:
1. Kuendeleza utafiti na utoaji wa huduma za ugani kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi, ili wafugaji wetu waweze kupata faida kubwa, jambo ambalo litawafanya wananchi wengine hasa vijana kuendelea kujiajiri katika sekta ya ufugaji na uvuvi. Suala la utafiti ni kikwazo kwa sekta zetu hizi, kuanzishwa kwa idara ambayo pia inasimamia suala la utafiti haitoshi, bali kuwepo kwa taasisi zinazojitegemea kushughulikia utafiti kisekta pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa utafiti, Serikali tayari imo katika mpango wa kufanikisha suala zima la vituo vya utafiti kwa kuanzia na sekta ya uvuvi na Serikali ya China na KOICA.
2. Kuongeza uwezo wa kitaaluma kwa wafanyakazi na kuajiri wataalamu zaidi ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma mbali mbali kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi ikiwemo huduma za ugani, ujasiriamali katika shughuli za ufugaji na uvuvi. Aidha, Serikali imo katika kuandaa mpango wa kuanzisha Chuo cha Uvuvi hapa Zanzibar.
3. Kuongeza ajira kwa vijana kupitia shughuli za uzalishaji mifugo na uvuvi; ingawaje kila siku sekta hizi zimekuwa muajiri mkubwa wa vijana, lakini kwa makusudi Wizara itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kuweza kujiajiri na kufanya kazi zao kwa faida. Kwa hivyo, Serikali imekuwa ikiandaa programu tofauti zitakazowasaidia pamoja na kuwaunganisha na taasisi na mashirika ili kupata misaada na mikopo isiyo na masharti magumu.
4. Kuendelea kuhamasisha wananchi kupandisha ng’ombe wa maziwa na nyama kwa kufuga kibiashara na kuondokana na mazoea. Kwani hivi sasa ni kiasi cha asilimia 5 tu ndio ng’ombe wa kisasa wanaozalisha maziwa, bado fursa ipo kwa watu kubadilisha ng’ombe wa asili.
5. Kuimarisha miundombinu ya kuendeleza uzalishaji wa mifugo ikiwemo vituo vya uzalishaji na utabibu wa mifugo (animal health and production centres) karantini na majosho.
6. Kuimarisha shughuli za mazao ya baharini kwa kujenga kituo cha uzalishaji vifaranga vya samaki hapo Beit el Ras kwa mashirikiano na Shirika la FAO na KOICA.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia itaendelea kuandaa mazingira mazuri ya kisera, sheria, kanuni na miongozo mbali mbali ili kuifanya sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta endelevu, ufugaji wa ng’ombe pamoja na uwekezaji wa viwanda vya usarifu wa samaki na mifugo bila kuathiri mazingira yetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imo katika kuandaa Mkakati Maalum wa Kuendeleza Sekta ya Uvuvi hapa Zanzibar, pamoja na Mkakati wa Kusimamia Utawala wa Baharini. Aidha, Wizara inakusudia kutoa taaluma kwa wadau wote wa sekta ya uvuvi ikiwemo wavuvi pamoja na kushirikisha jamii katika kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kufanya tathmini ya shughuli za uvuvi; na pia kushirikiana na wanajamii na vyombo vya sheria kuendeleza doria katika maeneo ya hifadhi na shughuli nyengine za baharini.
MAMBO MUHIMU YALIOJITOKEZA BARAZANI
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa 17, Baraza lako Tukufu lilikamilisha mambo makuu manne yafuatayo:
i. Kujibu maswali yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wajumbe.
ii. Uwasilishwaji wa miswada minne (4) ya Sheria ambayo ina umuhimu mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu.
iii. Kiapo cha uaminifu kwa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
iv. Hoja ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuliomba Baraza la Wawakilshi kutoa maazimio kuhusu uimarishaji wa huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu Wajumbe waliuliza na kujibiwa maswali ya msingi na maswali ya nyongeza. Jumla ya maswali ya msingi 48 na maswali ya nyongeza 100 yaliulizwa na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta husika. Nawapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliouliza maswali ya msingi ambayo yalikuwa na lengo la kudadisi utekelezaji na ufanisi wa shughuli za Serikali. Aidha, nawapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kutoa majibu sahihi ambayo yamewejengea uelewa Waheshimiwa Wawakilishi pamoja na wananchi kwa jumla.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa mwanzo uliowasilishwa ni Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Wauguzi na Wakunga (uanzishwaji wa Baraza la Usajili wa Wauguzi na Wakunga) Nam. 9 ya mwaka 1986 na kuanzisha badala yake Sheria mpya ya Wauguzi na Wakunga na Mambo Yanayohusiana na Hayo.
Mheshimiwa Spika, Mswada huu una madhumuni ya kukabiliana na hali halisi ya mabadiliko yaliyopo hivi sasa ulimwenguni katika sekta ya Uuguzi na Ukunga ambapo Sheria Nam. 9 ya 1986 inaonekana kutokidhi haja kwa matumizi ya wakati huu.
Mheshimiwa Spika, Waheshimwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu walipata fursa ya kuchangia Mswada huu kwa kina ambapo wengi wao waliiomba Serikali kuwa makini katika kusimamia utekelezaji wake ili kuleta ufanisi uliokusudiwa. Pia wameiomba Serikali kuyaangalia upya maslahi ya wauguzi na wakunga ili kuwapa motisha katika kutekeleza majukumu yao. Serikali imekisikia kilio hicho.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Pili uliowasilishwa ulikuwa ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Shirika la Nyumba la Zanzibar. Madhumuni ya Mswada huo ni kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba la Zanzibar kwa mujibu wa sheria ili kuweza kuziendeleza nyumba ziliopo nchini, kusimamia kodi, kujenga nyumba mpya na kutoa huduma nyengine zinazohusiana na masuala ya nyumba.
Mheshimiwa Spika, katika michango ya Waheshimiwa Wajumbe wameiomba Serikali kuwa makini na kuangalia madhumni ya kuanzishwa nyumba za maendeleo zilizopo nchini ambazo zimeanzishwa na Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na dhamira ya uanzishwaji wa sheria hii. Aidha, Waheshimiwa Wajumbe walionesha kuwepo kwa tatizo la umiliki na ukodishwaji wa nyumba kwa wananchi ambao wanaishi katika nyumba hizo.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Tatu uliowasilishwa ulikuwa unahusu kufuta Sheria ya Baraza la Manispaa Nam. 3 ya mwaka 1995 na Halmashauri za Wilaya na Mabaraza ya Miji Nam. 4 ya mwaka 1995 na kuanzishwa upya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2014 kwa madhumuni ya kuanzisha Serikali za Mitaa, uwezo wake, kazi na wajibu, muundo, mpangilio, fedha na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mswada huo Wajumbe wameishauri Serikali kuwa na tahadhari kubwa na kuangalia kwa makini suala la kijiografia juu ya mipaka ya Serikali za Mitaa. Aidha, waliishauri Serikali kumfanya Naibu Meya kuwa mfanyakazi wa kudumu na pia wameiomba Serikali kuboresha maslahi ya Madiwani kwa kuwapatia mishahara na sio kuwapa posho tu.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Nne uliowasilishwa unahusu kufuta Sheria Nam. 1 ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1998 na kuanzisha Sheria mpya ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 2014 na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Mswada huu unalenga kuweka mfumo wa Kiutawala wa Serikali Kuu kuanzia ngazi ya Shehia hadi Mkoa kwa kuzingatia mageuzi ya Serikali za Mitaa na kuondoa kasoro zilizojitokeza katika sheria ya sasa ya Tawala za Mikoa na kuweka mtiririko ulio bora zaidi kwa mujibu wa mahitaji ya sasa. Aidha, madhumuni ya mswada huu ni kupata Sheria itakayoonesha wajibu, muundo, kazi na uwajibikaji kwa kila ngazi ya Serikali Kuu kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na Shehia na kukuza uhusiano baina ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imesikia na kuzipokea hoja za Waheshimiwa Wajumbe kuhusiana na miswada yote minne iliyowasilishwa na itazizingatia na kuzifanyia kazi hoja hizo kadri hali itakavyoruhusu.
HITIMISHO:
Mhesimiwa Spika, kwa mara nyengine tena naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa umahiri wako na umakini mkubwa katika kuliendesha Baraza letu. Vile vile, narudia kuwapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kwa kazi zao nzuri katika kusimamia utendaji wa Serikali na kwa michango yao yenye tija katika kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika Serikali.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wote waliosaidia kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wajumbe. Pia nawashukuru waandishi wa habari na wakalimani wa lugha ya alama kwa kazi yao nzuri ya kuwapatia taarifa wananchi kuhusu majadiliano ya Baraza katika mkutano huu wa kumi na saba.
Mheshimiwa Spika, naomba tena kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe kwamba Serikali yao chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein itajitahidi kuhakikisha kwamba inaimarisha utendaji na uwajibikaji katika Serikali na kuendelea kudumisha amani na utulivu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo,sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 21 Januari, 2015 saa 3.00 asubuhi panapo majaaliwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.