Na Mwinyi Sadallah
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekiri kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu katika mji mdogo wa Mochuari kisiwani Pemba kutokana na kushamiri kwa matumizi ya dawa za kulevya - mihadarati
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Saleh Nassor Juma katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachofanyika Chukwani mjini hapa.
Alisema kutokana na tatizo hilo, polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba wameamua kuanzisha operesheni ya kila mara ya kuwasaka watumiaji wa dawa za kulevya pamoja na wauzaji na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Waziri Aboud alisema eneo la Mochuari ni sugu kwa vitendo vya uhalifu.
Alisema tayari operesheni saba zimefanyika katika eneo hilo na watu watatu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani baada ya kukutwa na pombe za kienyeji na dawa za kulevya.
“Mheshimiwa Spika, polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wataendelea kufanya oparesheni endelevu hadi kero za uhalifu zitakapokoma katika eneo la Moshuari,” alisema Waziri aboud. Awali, mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Saleh Juma alitaka kujua ni lini SMZ itachukua hatua ya kukabiliana na vitendo hivyo.
Chanzo : Mwananchi