Katibu Mkuu Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano Dr. Juma Malik mwenye miwani akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kulia yake harakati za ujenzi wa Bara bara ya Koani hadi Jumbi alipoitembea mapema asubuhi.
Kushoto ya Dr. Malik ni Mwakilishi wa Jimbo la Koani Mh. Mohd Raza na kulia ya Balozi Seif Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguija Dr. Idriss Muslim Hija na Mkuu wa Wilaya ya Kati Nd. Vuai Mwinyi.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uamuzi uliochukuliwa na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar wa kujadiliana na mjenzi wa Bara bara ya Koani hadi Jumbi ndio njia pekee itakayoweza kufanikisha ujenzi wa Bara bara hiyo.
Alisema uamuzi wa pande hizo mbili wa kupelekana Mahakamani hautowasaidia Wananchi ambao lengo lao ni kupata huduma za mawasiliano ya bara bara kwa kuendesha harakati zao za kimaisha.
Balozi Seif alisema hayo wakati akikagua ujenzi wa bara bara Koani hadi Jumbi inayojengwa na Kampuni ya Shapria unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu{ BADEA } akiwa katika ziara ya siku moja kukagua shughuli za maendeleo ndani ya Wilaya ya Kati.
Alisema changamoto zilizojitokeza katika ujenzi wa bara bara hiyo likiwemo suala la uchelewaji wa fedha za kuendesha mradi huo kutoka Nchini Sudan linapaswa kujadiliwa kwa makini na pande hizo mbili ili kufikia muwafaka utaoleta hatma njema kwa wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba nia ya Serikali ni kuona miundombinu inayoitekeleza kila siku ikiwemo sekta ya mawasiliano hasa bara bara inawafikia wananchi wote mjini na vijijini.
Aliupongeza Uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar kwa uvumilivu wake wa kuiridhia Kampuni hiyo kutokana na uchelewaji wa kazi walizokabidhiwa katika muda uliopangwa ambazo pia kwa upande mwengine zimesababisha na ufinyu wa bajeti kutoka Serikalini.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Dr. Juma Malik alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujenzi wa bara bara hiyo ya Koani – Jumbi umo ndani ya mradi wa kuimarisha bara bara tatu za Unguja unaofadhiliwa na Benki ya Badea.
Dr.Malik alisema mradi huo wa Kilomita 20 ambapo Bara bara ya Koani – Jumbi yenye urefu wa Kilomita 6 umechelewa kukamilika kama ulivyopangwa kutokana na ufinyu wa fedha.
Alisema jumla ya shilingi Milioni 300,000,000/- zinahitajika kwa ajili ya kazi ya usafishaji wa bara bara hiyo ghrama zitakazokwenda sambamba na ulipaji wa fidia za majengo na vipando vya wananchi vilivyomo pembezoni mwa bara bara hiyo.
Dr. Malik alifahamisha kwamba usafaishajiwote wa kazi hiyo utagharimu shilingi Milioni 408,000,000/- ambapo ujenzi wa jumla umeshachukuwa takriban miezi 22 na kazi imefikia asilimia 25%.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua jengo jipya la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kati liliopo Dunga na kuridhika na hatua iliyochukuliwa na Uongozi wa Wilaya hiyo kwa kuamua kuanzisha mradi huo utakaokidhi haja kwa wakati huu.
Mkuu wa Wilaya ya Kati Nd. Vuai Mwinyi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mradi huo Mkubwa ulioanza Tarehe 23 Mei Mwaka 2012 unatarajiwa kukamilika kwake mwezi Januari mwaka 2016.
Nd. Vuai alisisitiza kwamba ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kati umekuwa ukifanywa kwa awamu mbali mbali kulingana na makusanyo ya mapato pamoja na wafadhili tofauti.
Alisema ujenzi huo hadi sasa umeshafikia gharama ya shilingi Milioni 87,344,350/- zinazotokana na washirika wa maendeleo ndani ya nje ya nchi kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya hiyo lengo ni kukadiriwa kufikia gharama ya shilingi Milioni 700,000,000/-.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimaliza ziara yake kwa kukaguwa bara bara ya Kilomita Nane inayojengwa kati ya Cheju na Unguja Ukuu ambayo imepita kati kati ya bonde la mpunga cheju.
Balozi Seif alielezea kuridhika kwake na hatua iliyofikiwa ya ujenzi huo kwa hatua ya kuwekwa kifusi ambapo wajenzi wa Bara bara hiyo wameeleza kwamba mradi huo umepangwa kukamilika kwake Mnamo Mwezi wa Juni mwaka ujao.