Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Norway yaahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar

$
0
0
  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                                                  4.11.2014
---
NORWAY  imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya  maendeleo na kueleza kufarajika kwake na utekelezaji wa miradi iliyofadhiliwa na nchi hiyo hapa Zanzibar kwa jinsi ilivyopata mafanikio.

Balozi mpya wa Norway Bibi Hanne Marie  Kaarstad aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Balozi Kaarstad alimueleza Dk. Shein kuwa Norway inajivunia mafanikio yaliopatikana hapa Zanzibar katika miradi yake yote iliyoiunga mkono Zanzibar ukiwemo mradi mkubwa wa umeme kutoka Pangani Tanga hadi Wesha, kisiwani Pemba.

Aidha, Balozi huyo wa Norway alieleza kuwa mbali ya mradi huo mradi wa kusambaza maji vijijini nao umepata mafanikio makubwa hatua ambayo imeweza kukuza uchumi na kuimarisha sekta za maendeleo kwa wananchi wa vijijini.

Kutokana na hatua hiyo, sambamba na mafanikio makubwa yaliopatikana katika miradi mbali mbali ambayo Norway imesaidia hapa nchini, Balozi Kaarstad alimueleza Dk. Shein kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imo katika orodha ya kuendelea kufaidika na misaada ya nchi hiyo.

Alisema kuwa nchi yake hivi sasa imetenga nchi maalum ambazo itaendelea kuzisaidia na kuziunga mkono katika kuimarisha miradi ya maendeleo kutokana na juhudi kubwa ilizopiga katika kuendeleza miradi yake ambayo Tanzania ikiwemo Zanzibar tayari imepiga hatua kubwa kwa hilo.

Pamoja na hayo, Balozi huyo wa Norway alisisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria utaendelezwa na kuimarishwa na nchi yake huku akisisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono miradi mbali mbali hapa Zanzibar.

Kwa upande wa uimarishaji wa sekta ya uvuvi, Balozi huyo aliemueleza juhudi zitakazochukuliwa na afisi yake katika kuhakikisha suala hilo nalo linapewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimueleza Balozi Kaarstad kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wake wanathamini sana ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo sambamba na misaada ya Norway kwa Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa  wananchi wa Zanzibar hasa wa kisiwa cha Pemba kamwe hawatosahau juhudi za nchi hiyo katika kuiunga mkono Zanzibar kwa kuhakikisha kisiwa hicho kinapata umeme wa uhakika.

Alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa umeme huo wa uhakika ni kichocheo kikubwa cha uwekezaji katika kisiwa hicho huku akieleza mafanikio makubwa yaliopatikana kupitia mradi wa Shirika la Misaada la Norywa NORAD kwa awamu zake zote sambamba na usambazaji wa umeme vijijini ambapo Norway ilisaidia.

Aidha,Dk. Shein alimueleza Balozi Kaarstad kuwa azma ya Serikali anayoiongoza katika uimarishaji wa sekta za maendeleo ni kuimarisha sekta ya uvuvi hasa wa bahari kuu na kwa kutambua kuwa Norway imefanikiwa katika sekta hiyo aliona haja ya kuwepo kwa mashirikiano kwa pande mbili hizo

Akizunguzia kuhusu sekta ya afya, Dk. Shein alitoa pongezi kwa nchi hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kwa kupitia chuo chake Kikuu cha Haukland kilicho Norway kwa mashirikiano mazuri kati yake na Hopitali Kuu wa Mnazimmoja.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa Norway kwa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kusaidia uimarishaji wa Chuo cha Kilimo kiliopo Kizimbani, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akimueleza mafanikio yaliopatikana katika uimarishaji wa amani na utulivu hapa nchini, Dk. Shein alisema kuwa kuwepo kwa amani na utulivu ndio sababu kubwa inayowapelekea watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani kuja kuitembelea Zanzibar sanjari na wawekezaji kutoka kila pembe ya dunia.


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>