Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Maalim Seif Azungumza na Balozi wa Norway

$
0
0
Na Khamis Haji OMKR
Norway imeihimiza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na maelewano yaliyopo, ambayo ni matunda ya maridhiano ya kisiasa yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Wito huo umetolewa na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bibi Hanne Marie Kaarstad wakati alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.

Balozi Kaarstad amesema kutokana na uzoefu wa hali ya siasa huko nyuma, hivi sasa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kudumisha amani, maelewano na utulivu, mambo ambayo yemejenga mazingira mazuri kwa Serikali kujikita kwenye maendeleo, na kwa wananchi kufanya shughuli zao bila matatizo.

Naye, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesifu ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Norway na ameahidi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itafanya kila jitihada kuona ushirikiano huo unazidi kuimarika.

Maalim Seif amesema Norway imetoa mchango wa kipekee katika kuhakikisha Zanzibar inapata mafanikio makubwa katika nyanja mbali mbali, ikiwemo kudumishwa Utulivu wa Kisiasa pamoja na kusaidia sekta mbali mbali za kiuchumi, maendeleo na kijamii.

Amesema mchango wa Serikali ya Norway katika kufanikisha kufikiwa kwa Maridhiano ya Kisiasa yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Zanzibar ni wa kipekee na njia muafaka ya kuuenzi ni kuhakikisha Zanzibar hairudi tena kwenye siasa za chuki na uhsama.

Aidha, Maalim Seif amesema ili Maridhiano hayo yaweze kudumu, kasoro zinazojitokeza ambazo zinaweza kurejesha nyuma taswira na dhamira njema ya kufikiwa kwake, hazina budi kupatiwa ufumbuzi kwa haraka pale zinapojitokeza, ili kuzidi kujengwa hali ya umoja na kuaminiana.

Maalim Seif amezitaja baadhi ya chanagamoto zilizopo kuwa ni Maridhiano na Maelewano hayo kueleweka na kutekelezwa zaidi katika ngazi za juu Serikalini, ambapo mkazo zaidi unahitajika katika  ngazi za chini, kama vile kwenye Shehia.

Amesema ipo haja kwa Serikali na taasisi zote zinazosimamia haki kutekeleza wajibu huo na kila mtu aweze kupata haki anayostahili, bila kujali itikadi yake kisiasa, kabila au dini yake.

Aliyataja baadhi ya maeneo yanayo lalamikiwa kuwa ni baadhi ya wananchi wenye sifa kunyimwa vitambulisho vya Ukaazi, kukoseshwa haki za kushiriki katika chaguzi mbali mbali, pamoja na kuwepo malalamiko kuwa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baadhi ya wakti hutumika vibaya hasa katika masuala ya uchaguzi. 

Hata hivyo, Maalim Seif amesifu mchango wa Norway kwa Zanzibar katika kusaidia kukuza demokrasia, upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini, pamoja na kusifu mchango mkubwa wa nchi hiyo katika suala la uhifadhi wa mazingira Zanzibar.

Maalim Seif ametoa wito kwa Noway kuzudi kushirikiana na Zanzibar katika nyanja za uvuvi wa Bahari Kuu, sekta za Elimu na Afya na kuendeleza elimu ya uhifadhi na mazingira, ili kuilinda Zanzibar na hatari inayojitokeza ya eneo lake la ardhi kuliwa na maji ya bahari.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>