STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26 Novemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kutokubali kurubuniwa na watu wanaojidai kutetea maslahi ya Zanzibar kwa kupinga Katiba iliyopendekezwa na kubainisha kuwa lengo la watu hao ni kurudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumza na viongozi wa Mashina na Maskani za Chama cha Mapinduzi wa wilaya ya Kusini Unguja leo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kitendo cha watu hao kuipinga Katiba iliyopendekezwa kinamaanisha kudhoofisha jitihada za serikali na wananchi wa Zanzibar za kujiletea maendeleo.
Dk. Shein alifafanua kuwa baadhi ya watu hao walikuwa wamesimama kidete kutaka masuala ya mafuta yashughulikiwe kwa kufuata Sera na Sheria za Zanzibar lakini leo wamegeuka kupinga jambo hilo kwa kuikataa Katiba ambayo inalitekeleza suala hilo.
“Watu hawa ni vigeugeu…wakati walishiriki kupitisha na kuamua azimio la kutaka Zanzibar ichimbe mafuta na gesi kwa kutumia Sera na Sheria zake badala ya kuwa suala la muungano leo hii jambo hilo limetekelezwa katika Katiba iliyopendekezwa wanaipinga” Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao na kusisitiza kuwa watu hao wapuuzwe na wala wasipewe nafasi ya kuivuruga Zanzibar.
Alifafanua kuwa watu hao ni wapinga Muungano na kuwa wanafanya kila hila za kuuvunja na kueleza kuwa wanafahamu fika kuwa “endapo Katiba iliyopendekezwa itapitishwa itakuwa imemaliza fitina zao za kutaka kuvunja Muungano” Dk. Shein alieleza.
Alisema kuwa haiingii akilini kuona watu wanapinga jambo hilo na kuizuia Zanzibar isiweze kuendelea na jitihada zake za kuendeleza sekta ya mafuta na gesi kwa kizingizio cha kuipinga Katiba.
“wanataka Zanzibar tubaki nyuma wakijua kuwa tukiweza kuchimba gesi na mafuta tutaweza kupiga hatua za haraka. Hivi sasa Tanzania bara wanachimba mafuta na gesi na majirani zetu wote” Dk. Shein alisema na kusisitiza kuwa nia ya watu hao ni kuona Zanzibar inabaki nyuma na wao wanapata la kusema.
Kwa hivyo alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kuchukua tahadhari na kuisoma kwa makini Katiba iliyopendekezwa ili waweze kufanya maamuzi sahihi wakati watakapotakiwa kuipigia kura.
Aliwatahadharisha wananchi hao kuwa wasisahau kuwa bado wapo watu wanaoitaka Zanzibar kwa kuwa baadhi yao wanaamini kuwa Mapinduzi yaliwaonea na ndio maana kila wazanzibari wanaposimama majukwani kutamka Mapinduzi daima wao inawauma na kuchikizwa na kauli hiyo.
Wakati huo huo Dk. Shein amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Kusini Unguja kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za jamii kwa kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazokwamisha ufanisi katika utoaji wa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi.
Akijibu baadhi ya maelezo ya viongozi katika mkutano huo, Dk. Shein alieleza kuwa tatizo la ukosefu wa madaktari katika hospitali ya mkoa ya Makunduchi, Kivunge na pamoja na vituo vingine vya afya katika mkoa wa Kusini Unguja amelipokea kwa uzito unaostahiki na ataiagiza wizara kulishughulikia haraka.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa hospitali hiyo ya Makunduchi na Kivunge zinapata watumishi wa afya wa kutosha wakiwemo madaktari ili huduma zitolewazo ziweze kwenda sambamba na lengo la Serikali la kuzipandisha hadhi hospitali hizo”.
Kuhusu suala la Shirika la Umeme-ZECO na Mamlaka ya Maji Zanzibar –ZAWA kuwakatia wateja wanaochelewesha malipo ya huduma, Dk. Shein aliahidi kuwasiliana tena na uongozi wa taasisi hizo kuwataka kutoa taarifa mapema kabla zoezi la kukata huduma kuanza.
Hata hivyo aliwakumbusha wananchi kuwa taasisi hizo zinayo mamlaka ya kusitisha huduma kama hawatakuwa wanalipa bili zao hivyo nao wanapaswa kulipa bili zao kama itakiwavyo.
Mapema Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kusini Bwana Abdulaziz Hamad Ibrahim alipongeza Serikali kwa kutimiza ahadi zake katika Mkoa huo ikiwemo uimarishaji wa huduma za afya, maji na uboreshaji wa Halmashauri pamoja na kusifu ufuatiliaji wa utekelezaji wa ahadi za Rais unaofanywa na wasaidizi wa Mhe Rais.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuisoma Katiba iliyopendekezwa ili kupambana na upotoshwaji wa makusudi wa maudhui ya Katiba hiyo unaofanywa na baadhi ya viongozi wa upinzani kwa maslahi yao ya kisiasa.
“Katiba hiyo ina maslahi makubwa kwa pande zote lakini tunaweza kusema kuwa wakati mwingine wenzetu wa Tanzania Bara wameonesha uungwana sana wa kukubali baadhi ya mambo ambayo ni dhahiri yameipa maslahi zaidi Zanzibar kuliko Tanzania Bara”
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822