Habiba Zarali na Abdi Suleiman,Pemba
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej, amewataka wananchi kisiwani Pemba, kusirikiana katika kupiga vita ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.
Alisema mashirikiano kati ya jamii nzima yatasaidia kupunguza maambukizi mapya ya visuri vya UKIMWI.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho, katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani, yaliyofanyika Machomanne mkoa wa kusini Pemba.
Alisema mashirikiano hayo ikiwemo kuwafichua wahalifu wa ubakaji,kupima kwa hiari na kutumia dawa kwa walioathirika, kutaleta mafanikio makubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha alisema kusini kwa bara la Afrika zipo nchi ambazo maambuziki yake yako katika silimia 5 hadi 10 ambapo hali ni ya kutisha.
Alisema Zanzibar kwa utafiti wa 2012 mambukizi mapya yalikuwa ni asilimia 0.6 ambapo hadi sasa yamefikia asilimia moja hali ambayo inatisha ikilinganishwa na idadi ya wananchi wake.
Alisema maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI bado yapo katika visiwa vya Zanzibar hivyo ni wajibu kila mmoja kuchukua juhudi za makusudi kuhakikisha anayazuia yasienee.
Akizungumzia vituo vya ushauri nasaha, alisema Zanzibar kuna vituo vya kutoa ushauri nasaha na huduma za mama wajawazito 156, kutoka 137 kwa mwaka 2012 ambavo vinasaidia kuhakikisha maambukizi yanapungua.
Aidha aliwataka akina mama waliobainika kuwa na virusi vya UKIMWI kuhudhuria kliniki mapema kwani ili kuondoa uwezekano wa mtoto kuzaliwa na maambukizi.
Aidha aliwasihi wananchi kuachana na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI badala yake wapewe mashirikiano katika kila hali kwani nao wana haki sawa na wengine.
Alilaani vikali vitendo vya udhalilishaji wa watoto, ikiwemo ubakaji na kulawitiwa na kuitaka jamii kutokuwafumbia mamcho wanaohusika.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla, aliwataka wananchi kupima afya zao ili kuishi kwa furaha na wale watakaobainika kuwa na maambukizi kuanza kutumia dawa mapema.
Alisema starehe ni miongoni mwa vichocheo vya kupata maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI hivyo kila mmoja awe makini juu ya suala hilo.
Alisikitishwa na vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa watoto, hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo na ustawishaji wao.
Akisoma risala ya Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Zanzibar (ZAPHA+), Katibu wa jumuiya hiyo, Saade Saaduni, aliishukuru serikali na wadau kwa jinsi wanavyowajali na kuwathamini watu wanaoishi na VVU na UKIMWI.
Walisema watu wanaoishi na VVU na UKIMWI wamekuwa wakishiriki katika programu mbalimbali za utoaji wa elimu ya UKIMWI kwa jamii, ikiwemo uhamasishaji wa watu kupima afya zao.
Aliishauri serikali kufikiria kuanzisha mfuko maaluma wa HIV, kuangalia uwezekano wa kurudisha misaada ya chakula kwa watu wanaoishi na VVU hasa akinamama wajawazito na watoto wanaotumia dawa za ARVs na walio katika mazingira magumu.
Wadau wa masuala ya mapambano ya UKIMWI Zanzibar, ABCZ walisema kuwepo mipango mizuri yenye kutekelezeka kutasaidia kutokomeza unyanyapaa na vifo kwa watu wanaoishi na UKIMWI.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Ukimwi Zanzibar, Prof. Saleh Idris Mohammed, aliiomba serikali kuongeza fedha katika kukabiliana na mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU.