Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani akimfahamisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hatua zilizochukuliwa za kuheshimu hifadhi ya urithi wa Kimataifa wakati wa ujenzi wa Hoteli ya Park Hyatt iliyopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Nyuma ya Nd. Sarboko ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi, Kulia ya Balozi ni Naibu Waziri wa Ardhi, Maji Nishati na Madini Mh. Haji Mwadini pamoja na Mratibu wa Mradi wa Hoteli ya Park Hyatt Bwana Yaqoub Osman.
Balozi Seif akikagua moja ya vyumba vya watu Mashuhuri { VIP } kwenye Hoteli ya Park Hyatt na kuridhika na kiwango kilichofikiwaMakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkonhwe Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani akikagua hitimisho la ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Park Hyatt hapo Forodhani Mjini Zanzibar.
Hoteli hiyo inatarajiwa kufunguli wa rasmi kwenye shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 51 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar zinazotarajiwa kuanza rasmi mapema mwezi ujao wa Januari 2015.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ
Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alitembelea na kukagua hatua za mwisho za ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Park Hyatt iliyopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujenzi wa Hoteli hiyo umezingatia mazingira halisi ya hifadhi ya Mji Mkongwe likiwemo jengo lililokuwa ofisi ya Mrajisi wa Vizazi na vifo ambalo linaendelea kubakia katika mazingira yake ya kiasili.
Nd. Sarboko alisema Uongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni { UNESCO } lilikuwa makini katika kufuatilia ujenzi wa Hoteli hiyo kwa kuzingatia kwamba Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa miaka kadhaa sasa umekuwa miongoni mwa miji iliyopewa hadhi ya kuwa urithi wa Kimataifa.
Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe alifahamisha kwamba kazi hiyo ilikwenda sambamba na uhifadhi ya eneo la fukwe iliyopo pembezoni mwa Hoteli hiyo ambayo hutoaa mandhari nzuri na ya kuvutia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Hoteli hiyo na kuupongeza uongozi wa Hoteli hiyo pamoja na wahandisi wa ujenzi huo kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi kutoka Jamuhuri ya watu wa China ya CRJ.
Hoteli hiyo yenye hadhi ya kiwango cha Kimataifa inatazamiwa kufunguliwa rasmi katika shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 zinazotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi wa Januari mwaka ujao.