STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 6.12.2014
MAREKANI imezipongeza juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa ambayo imepata mafanikio makubwa.
Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Marekani Mhe. Amina Salum Ali, aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed Shein Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Balozi huyo wa AU nchini Marekani alisema kuwa mafanikio yaliopatikana ndani ya miaka minne ya uongozi wa Dk. Shein ni makubwa na yana kila sababu ya kupongezwa kutokana na juhudi anazozichukua katika kuisimamia na kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa.
Alisema kuwa Marekani inazipongeza juhudi hizo sambamba na uongozi wa Dk. Shein kwa kuendelea kusimamia amani na utulivu hapa nchini.
Balozi huyo wa AU nchini Marekani alieleza kuwa mafanikio hayo yote yamepatikana kutokana na uongozi imara wa Dk. Shein ambao unaenda sambamba na busara zake hekima na kujali wananchi anaowaongoza. Pia, Balozi huyo alipongeza mafanikio yaliofikiwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar pamoja na mikakati iliyowekwa katika uimarishaji wake.
Aidha, Balozi Amina alieleza kuwa Zanzibar imeweza kujijengea sifa kubwa ndani na nje ya nchi na kuwa kigezo kwa nchi za Bara la Afrika ambazo zinaongozwa na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Nae, Dk. Shein kwa upande wake alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa imeweza kupata mafanikio makubwa hapa nchini.
Alisema kuwa kuwepo kwa Serikali hiyo kumeweza kuwaweka viongozi wa vyama vya siasa pamoja na kuweza kujalidi masuala mbali mbali ya nchi kwa mashirikiano ya pamoja bila ya kujali itikadi zao za kisiasa.
Dk. Shein alisema kuwa ndani ya miaka minne ya uongozi wake chini ya Serikali hiyo mafanikio makubwa yameweza kupatikana huku akisisitiza kuwa siasa ni maendeleo na kustahamiliana na si vyenginevyo.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani na pongezi kwa Marekani kutokana na juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Balozi Mdogo wa Msumbiji anayefanya kazi zake Zanzibar Mhe. Jorge Augusto Menezes aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.
Katika maenelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Msumbiji zina historia kubwa kutokana na wananchi wa nchi mbili hizo kuwa na uhusiano na mashirikiano ya muda mrefu.
Dk. Shein alisema kuwa sekta ya biashara kati ya Msumbiji na Tanzania imeweza kuimarika kutokana na wananchi wa nchi mbili hizo kupata fursa nzuri ya kufanya biashara na kusisitiza haja ya kuimarisha zaidi sekta hiyo pamoja na sekta nyenginezo.
Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuwepo kwa mashirikiano kati ya Msumbiji na Zanzibar katika kuimarisha zao la mpunga kupitia kituo cha Utafiti kiliopo Kizimbani Zanzibar.
Alisema kuwa kutokana na nchi hiyo kupata mafanikio makubwa katika kilimo hicho itakuwa ni jambo la busara kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa mafanikio yaliopatikana kwenye sekta ya uvuvi nchini Msumbiji ni ya kupongezwa na kueleza haja ya kuwepo mashirikiano na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uvuvi hapa nchini kwani tayari juhudi mbali mbali zimeweza kuchukuliwa na Serikali ya Mmapiduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo.
Nae Balozi Menezes alipongeza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Msumbiji na Zanzibar na kuahidi kuendelezwa na nchi yake sambamba na wananchi wa nchi hiyo ambao wamekuwa na mahusiano mazuri na ya kihistoria na wananchi wa Zanzibar.
Balozi Meneza alipongeza juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein na kueleza matumaini yake ya kuendelezwa kwa uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo.
Pamoja na hayo, Balozi huyo alitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Shein mafanikio ya kisiasa yaliofikiwa nchini Msumbiji sambamba na mafanikio ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni nchini humo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk