STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 6.12.2014
WITO umetolewa kwa wananchi kuwa sasa iwe basi kwa maneno na vitendo katika kuwafanyia ukatili na udhalilishaji wanawake na watoto na watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo wapelekwe kwenye vyombo vya sheria sambamba na kuwepo mashirikiano katika kutoa ushahidi bila ya kumuonea mtu.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito huo leo huko katika ukumbi wa Salama, Bwawani mjini Zanzibar katika hotuba yake aliyoitoa kwenye uzinduzi wa Kampeni ya miaka miwili ya Kupiga Vita Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto Zanzibar.
Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa jambo ambalo linampa huzuni na kumsikitisha ni kuendelea kusikia kila uchao kushamiri kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto katika jamii.
Alisema kuwa hili ni suala ambalo linatokea katika jamii mbali mbali duniani, lakini kwa silka, mila, utamaduni, dini na historia ya jamii ya Kizanzibari tatizo hilo halikustahili kufikia katika kiwango kilichopo sasa nchini.
“Lazima sote tulionee aibu jambo hili ambalo siyo tu linaipa taswira mbaya jamii yetu lakini vile vile, lina athari kubwa kijamii na hasa wanawake na watoto wanaoishi kwa hofu, kwa wasiwasi na kwa masikitiko makubwa pamoja na kukosa raha na furaha”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto ni uvunjaji wa haki za binadamu na haki za kikatiba kwa hivyo ni lazima jamii yote ichukue hatua madhubuti na kutekeleza dhamira ya kuendeleza utawala bora ulioipa nchi hii heshima kubwa.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua za kuzirekebisha sheria kila inapobidi kwa lengo la kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto vinadhibitiwa.
Alisema kuwa taarifa kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali zinaeleza kuwa zimeripotiwa kesi 149 za wanafunzi waliopewa ujauzito kati ya mwaka 2010 hadi 2014 kutoka Wilaya kumi za Zanzibar ambapo pia katika kipindi hicho kuna matukio 229 ya wanafunzi waliokatishwa masomo yao na kuozeshwa waume wengine bila ya ridhaa zao.
Akitoa nasaha zake Dk. Shein aliitaka jamii kurudi katika misingi ya maadili mema na malezi bora ya watoto kwa mujibu wa utamaduni wa Kizanzibari na mafundisho ya dini na kuwataka wazazi kufuatilia nyendo za watoto wao hasa katika matumizi ya mitandao ambao watoto hujifunza mienendo isiyokubalika katika utamaduni na maadili ya Kizanzibari.
Dk. Shein alitoa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa, viongozi wa vyombo vya habari na viongozi wa taasisi za kiraia na jumuiya zisizo za kiserikali, kuzidi kuelimisha wananchi kwa njia mbali mbali juu ya athari na ubaya wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wananwake na watoto kwa mujibu wa dini, sheria na tamaduni ziliopo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa kufanikiwa kwa Kampeni hiyo kunategemea sana juhudi za pamoja na kuimarishwa kwa mikakati inayotumiwa katika kukabiliana na suala hilo ikiwa ni pamoja na kuifanyia kazi Sheria ya Mtoto namba 6 ya mwaka 2011 ikiwa muongozo mkuu wa kusimamia haki za watoto.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali itafanya kila jitihada, ili Mkakati wa Mageuzi ya Mfumo wa Sheria kwa watoto unafanikiwa ikiwa ni hatua muhimu ya kuipa nguvu kampeni hiyo ya kupambana na ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Alieleza kuwa kwa bahati mbaya sana baadhi ya kinababa huwaachia sana ulezi kina mama peke yao, jambo ambalo baadhi ya wakati matokeo yake huwa si mazuri na matokeo yake wanaume huanza kuwalaumu wanawake na wakati mwengine kuonesha kiburi.
Pia, Dk. Shein alikemea tabia ya kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili ikiwemo kupigwa kwani haitoa taswira nzuri hasa kwa wanaume na kusisitiza kuwa mke hapigwi na badala yake huengwa engwa “Mke hapigwi kwa fimbo hupigwa kwa ncha ya kanga”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa ongezeko la talaka nalo limekuwa likichangia sana kuleta matokeo mabaya ya malezi kwa watoto na wakati mwengine kuwa chanzo cha vitendo vya udhalilishaji dhidi yao na kuwataka wanandoa kustahamiliana, kupendana na kumuomba Mungu alete baraka na kuzidumisha ndoa.
Mapema Dk. Shein alipokea matembezi ya hiyari yaliozishirikisha Wizara za Serikali pamoja na taasisi binafsi pamoja na wananchi kutoka sehemu mbali mbali ambazo zilipeba ujumbe mbali mbali katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa watoto na wanawake na baadae alikagua mabanda ya maonesho yaliofanyika katika viwanja vya hoteli ya Bwawani na kupata maelezo kutoka kwa wahusika.
Akitoa maelezo yake Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mhe. Zainab Omar Mohammed alisisitiza haja ya kuwepo mashirikiano ya pamoja katika kupiga vita udhalilishaji na ukatili wa watoto na wanawake.
Nae Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya kwa nyakati tofauti katika maelezo yao walieleza kusikitishwa na hali hiyo na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kupambana na ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Nayo risala ya Wanawake na Watoto iliyosomwa na Bi Hidaya Makame ilieleleza kuwa miongonim mwa sababu zinazopelekea ukatili na udhalilishaji wa wanawake ni pamoja na mila na desturi potofu katika jamii za kumuona mwanamke kuwa ni kiumbe dhalili, mwenye hali duni ya kiuchumi pamoja na kuporomoka kwa maadili.
Alidha risala hiyo ilieleza kuwa watoto wanakabiliwa na mazingira magumu zaidi kutokana na kukosa uwezo wa kujitetea, pia, risala hiyo ilieleza changamoto zinazowakabili wanawake na watoto wenye ulemavu na wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Risala hiyo ilieleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji, ikiwa pamoja na kubakwa, kukosa matunzo stahiki, kunyanyapaliwa, kufanyiwa mambo mabaya kinyume na maadhili na kuishi katikamazingira magumu.
Katika uzinduzi huo ambao ulizinduliwa kwa maelezo yaliotolewa na viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikiristo juu ya udhalilishaji wa watoto na wanawake ambapo viongozi hao walieleza kuwa dini zote hizo zinakataza udhalilishaji huo na ukatili.
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika uzinduzi huo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mama Pili Balozi, Mawaziri, na viongozi wengine wa serikali, dini na kisiasa, taasisi binafsi, Mashirika ya Kimataifa pamoja na wanachi mbali mbali.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk