Na.Othman Khamis Ame. OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuomba Uongozi wa Bodi ya Chakula,Dawa na Vipodozi Zanzibar { ZFDB } kuwaelimisha wananchi juu ya mfumo bora wa matumizi ya vyakula na vinywaji ili kulinda afya zao.
Alisema afya za jamii zitaendelea kuimarika na kuwa salama endapo vyakula na vinywaji wanavyotumia vinakuwa salama katika kiwango kinachokubalika kwa matumizi ya mwanaadamu popote pale Duniani.
Balozi Seif alitoa ombi hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kulikagua jengo jipya la Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar liliopo katika Mtaa wa Mombasa Wilaya ya Magharibi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema hatua ya kuuelimisha umma kupitia vyombo mbali mbali vya Habari na mawasiliano inafaa iongezwe kwa lengo la kuitanabaisha jamii kujiepuka na hila za baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia mwanya wa kusambaza bidhaa zisizostahiki kutumiwa na mlaji.
Alieleza kwamba zipo bidhaa zinazoingizwa nchini na baadhi ya wafanyabiashara ambazo tayari zimeshapitwa na wakati wa matumizi wakijua fika kwamba zinaweza kuleta athari kwa umma lakini kinachowapa msukumo wa kufanya hivyo ni tamaa na utajiri wa haraka haraka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushukuru Uongozi na wafanyakazi wa Bodi hiyo ya Chakula, Dawa na Vipodozi kwa kujudi wanazochukuwa za kukabiliana na wajanja wanaojaribu kuingiza bidhaa zisizostahiki kutumika hapa nchini bila ya kujali afya za wananchi wenzao.
Balozi Seif pia akaupongeza uongozi wa Bodi hiyo kwa hatua iliyofikia ya kujenga jengo kubwa na la kisasa linalokwenda na wakati na kuuhakikishia Uongozi wa Bodi hiyo kwamba atachukuwa juhudi katika kuona yale mafungu yao wanayopangiwa katika Bajeti ya Wizara yao wanayapata ili kukamilisha ujenzi wao.
Mapema Mrajisi wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar Dr. Burhan Othman Simai alisema Bodi hiyo hivi sasa imejikita zaidi katika kuongeza uwezo wa kulinda afya za Wananachi kwa kutumia mfumo wa Taaluma.
Dr. Burhan alisema watendaji wa bodi hiyo watajengewa mazingira mazuri ya kupatiwa mafunzo ya kitaalamu zaidi ambayo yatakidhi mahitaji halisi ya mfumo huo.
Mrajisi huyo wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi alifahamisha kwamba Taasisi hiyo kwa mujibu wa vigezo na taratibu za Kimataifa kwa sasa inalazimika kuwa Mamlaka inayojitegemea.
Alisema licha ya juhudi za kwenda na vigezo hivyo iliyochukuliwa na Bodi hiyo kwa hatua ya kuandaa rasimu ya mabadiliko ya sheria iliyoandaliwa na Taasisi hiyo lakini ufinyu wa bajeti nao unachangia kuzorota kwa suala hilo.