Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Balozi Seif Aipongeza Kampuni ya Mizingo ya CMA CGM,

$
0
0
Na.Othman Khamis OMPR.  
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Zanzibar inapendelea kuona kwamba mizigo ya wafanyabiashara wake inayotoka Nchi mbali mbali Duniani inaletwa moja kwa moja Zanzibar ili ihudumie Jamii katika muda uliokusudiwa.

Alisema hatua na utaratibu huo unaweza kusaidia kupunguza au kuondosha kabisa malalamiko mengi ya Wafanyabiashara wa Zanzibar yanayodai kupotea kwa mizigo yao katika Bandari nyengine za mwambao wa Afrika Mashariki.

Balozi Seif alieleza hayo wakati wa tafrija maalum ya kuagwa kwa Meneja wa Tawi la Kampuni ya Kimataifa ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya maji 
Duniani  ya CMA CGM Bwana Burhan Moh’d ambae anastaafu kazi baada ya kuitumikia Kampuni hiyo kwa karibu miaka Sita.

Tafrija hiyo fupi ya chakula cha jioni  ambayo pia ilishirikisha baadhi ya wafanyakazi wa vitengo mbali mbali vya taasisi za usafiri wa Baharini Zanzibar ilifanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari kubwa katika eneo la Maruhubi Mpiga duri  ili kutoa nafasi zaidi kwa Wafanyabiashara wa ndani na nje ya Nchi  kuleta bidhaa zao kwa nafasi sambamba na kuongeza mapato ya Taifa.


Balozi Seif alisema kwamba Bandari hiyo ya Maruhuri kwa mujibu wa malengo ya Serikali inatarajiwa iwe kubwa nay a kisasa ikiwa na uwezo kamili wa kuhudumia Meli zozote kubwa zitakazoleta mizigo hapa Zanzibar.

Alisema mizigo mingi inayoteremshwa katika Bandari ya Malindi hasa makontena kwa sasa imekuwa na mtihani na changamoto kubwa  ya  kuwa na sehemu za kuhifadhia makontena hayo jambo ambalo huchangia kuzorota kwa shughuli za Bandari hiyo iliyolengwa kutoa huduma za Kimataifa.

Balozi Seif alifahamisha kwamba eneo la muda linalosaidia kuhifadhiwa makontena hayo kwa hivi sasa liliopo pembezoni mwa Hoteli ya Bwawani linahitajika kutumika kwa shughuli nyengine za uwekezaji kitega uchumi.

“ Uwepo na Makontena katika eneo la Hoteli ya Bwawani ambayo yalitakiwa kuhifadhiwa kwa muda kunaweza kuzorotesha kasi na malengo ya uwekezaji wa eneo hilo katika sekta ya utalii “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Meneja Mstaafu huyo wa Kampuni ya CMA CGM Tawi la Zanzibar Bwana Burhan Moh’d kwa kufanya kazi kwa mashirikiano na wenzake na kufikia hadhi ya kuagwa rasmi  kwa heshima na taadhima.

“ Tumeshuhudia kwenye Taasisi zetu baadhi ya wafanyakazi hasa wale wenye dhamana za  vitengo wanapostaafu wenzao  hufikia hatua ya kupika   biriani wakionyesha furaha yao kutokana na ukorofi  uliokuwa ukifanywa na  mstaafu huyo wkati wa enzi zake “. Alisema Balozi Seif.

Aliwashauri watendaji wengine wa Taasisi za Umma na hata zile Binafsi zinazotoa huduma kwa Umma waendelee kutekeleza  wajibu wao katika misingi ya maarifa, nidhamu na ustahamilivu ili wajijengee heshima nzuri wakati wanapofikia muda   wa kustaafu.

Mapema Naibu Meneja Mkuu wa Kampuni ya CMA CGM Bwana Peter Kirigini alisema kwamba mchango wa Bwana Burhan Moh’d ambao utaendelea kuheshimiwa na Uongozi wa Kampuni hiyo umeisaidia taasisi hiyo kuwa na ushirikiano mpana na Makampuni mbali mbali ya usafiri wa Baharini Duniani.

Bwana Kirigini alisema Mwaka ujao wa 2015 una matarajio makubwa kwa Kampuni hiyo kutokana na mizigo ya Wafanyabiashara wa Tanzania  kusafirishwa moja kwa moja kutoka nchi za Bara la Asia hadi Dar es salaam Tanzania.

Alisema mfumo huo mpya utakaopunguza muda wa karibu siku Nane kwa kusafirisha mizigo hiyo kuja Tanzania utatoa mchango katika uimarishaji wa uchumi kwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Akitoa nasaha zake kwenye tafrija aliyoandaliwa Meneja Mstaafu huyo wa Kampuni ya CMA CGM Tawi la Zanzibar Bwana Burhan Moh’d alisisitiza kwamba ushirikiano wa pamoja ndio njia pekee inayokuza na kuendeleza jambo au taasisi yoyote ile.

Bwana Burhan alielezea matarajio yake kwamba Kampuni hiyo Chini ya Meneja wake Mpya Bwana Hassan Jengo itaendelea kukua siku hadi siku na kutoa huduma nzuri zitakazoleta mafanikio makubwa kwa Kampuni na pamoja Taifa.

Kampuni ya Kimataifa ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya majini Duniani  ya CMA CGM yenye Makao Makuu yake Nchini Ufaransa hivi sasa ni ya tatu Duniani na ya kwanza Ufaransa na Tanzania kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Bwana Philippe Bablon.

Bwana Philippe alieleza kwamba Kampuni ya CMA CGM iliyoasisiwa Nchini Ufaransa mwaka 1978 inathamini na kuzingatia zaidi uhifadhi wa mazingira katika   uendeshaji wa shughuli zake.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>