Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Maazimio ya Baraza kuu la CUF baada ya kikao cha Dar

$
0
0

MAAZIMIO YA KIKAO CHA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA KILICHOFANYIKA DAR ES SALAAM  TAREHE 21-22 AGOSTI, 2013 

Baraza Kuu la Uongozi Taifa la The Civic United Front (CUF- Chama Cha Wananchi) limekutana na kufanya kikao chake cha kawaida kwa mujibu wa katiba ya chama, kikao ambacho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Shaaban Mloo, Dar es salaam, tarehe 21-22 Agosti, 2013. Katika kikao hicho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipokea, kuzijadili na kuzifanyia maamuzi agenda mbalimbali zilizowasilishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ikiwa ni pamoja na;
  1. Taarifa ya utekelezaji wa kazi za chama Mei-Julai, 2013.
  2. Taarifa ya utekelezaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
  3. Taarifa ya utekelezaji wa kazi za wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuanzia Januari-Julai, 2013.
  4. Taarifa ya kutekwa na kuteswa kwa viongozi wa CUF na JWTZ mkoani Mtwara.
  5. Program ya kuimarisha Chama Sept 2013-Julai 2014 na Uchaguzi wa ndani ya Chama. 
  6. Hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini, pamoja na masuala mengineyo yaliyojadiliwa na kufanyiwa maamuzi.

Baada ya mjadala wa kina kuhusiana na agenda hizo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo;

1. Kuhusu Taarifa ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Mei-Julai, 2013;
Baraza Kuu limepokea taarifa ya kazi za Chama kwa kipindi cha mwezi Mei-Julai, 2013 na kuipongeza Kamati ya Utendaji Taifa kwa kazi iliyofanywa katika kipindi hicho, ikiwa ni pamoja na kuipongeza kwa kufanikishan ushindi na kulirejesha Jimbo la Chambani, Mkoa wa Kusini Pemba kwa kukipatia chama chetu ushindi wa kutosha. Pia Baraza linawapongeza Wapiga Kura wa Wadi ya Ng’omeni katika Jimbo la Mkoani, Wialya ya Mkoani kwa ushindi iliofanyika Miezi Michache iliopita. CUF inawashukuru wananchi wote wa Chambani na Wadi ya Ng’omeni na kuwaahidi utumishi wa dhati kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Baraza Kuu limeiagiza Kamati ya Utendaji ya Taifa kufanya utafiti wa kina juu ya matokeo yasioridhisha ya uchaguzi mdogo wa marudio katika kata 26 uliofanyika nchini na kuleta mapendekezo ya utekelezaji katika kikao kijacho cha Baraza kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

2. Taarifa ya Utekelezaji Kazi za Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Baraza kuu la uongozi la Taifa linawapongeza Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa kusimamia majukumu yao vizuri na kuweza kudhihirisha wazi kuwa CUF na viongozi wake wanauwezo mkubwa wa kuwaletea mabadiliko ya maisha Wazanzibari. CUF inawaomba Wanzanzibari wote kutuunga mkono katika jitihada hizi za kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa wananchi wote.

3. Taarifa ya Utekelezaji wa kazi za Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuanzia Januari-Julai,2013

Baraza kuu limepokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kipindi cha Januari-Julai, 2013.
Linawapongeza kwa kazi nzuri ya kuzisimamia serikali zote mbili kikamilifu na kuweza kufichua ubadhilifu na ufisadi wa kutisha katika wizara mbalimbali.

Baraza Kuu linahitaji Kamati za Bunge na Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali kufanya ukaguzi wa kina na kutoa maelezo kwa Watanzania na hususani Wananchi wa Mtwara kwamba fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2010/2011, Sh. 540 milioni ambazo zilikuwa ziende kwenye mradi wa Mnazi Bay Gas and Electricity Development Project, fedha hiyo imetumikaje wakati mradi wenyewe haupo, na hali mradi huo ulikuwa umeingizwa katika vitabu vya bajeti ya Serikali.

Wawaeleze Watanzania ni kwa sababu gani mradi huo wameufuta na fedha hizi zimekwenda wapi? Baraza Kuu pia limetaka upembuzi yakinifu wa mradi wa bomba la gesi na mikataba ya kujenga bomba iwekwe wazi ili wananchi waweze kubaini faida na hasara zake.

Aidha, limewataka Wabunge kufuatilia taarifa ya ufisadi zilizofichuliwa na kamati ya hesabu za serikali kuu kiasi cha shilingi bilioni 247 za commodity import support hazijalipwa Hazina na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa. Vilevile Bunge lichukue hatua za kuwawajibisha Mawaziri waliolidanganya Bunge kuhusu miradi hewa ya barabara iliyotengewa fedha shilingi bilioni 252.

4. Hali ya amani, usalama wa Taifa na Haki za Binaadamu Nchini;

a) Kuhusu Kuteswa na Kudhalilishwa kwa Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni Shaweji Mketo na wenzake.Baraza Kuu la Uongozi linalaani vikali vitendo vya kikatili walivyofanyiwa Viongozi wa Cuf na JWTZ vya kuwateka nyara, kuwatesa na kuwadhalilisha katika kambi ya JWTZ, Naliendele, Mtwara. Aidha, linalaani vikali hatua za Jeshi la Polisi, Mtwara la kuwabambikizia kesi ya uchochezi Mketo na wenzake hali wakijua fika kuwa askari wa JWTZ waliwateka nyara na kuwatesa kinyume sheria.

Kuteswa na kudhalilishwa kwa Mketo na wenzake kunatokana na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliotamka Bungeni ya Piga tu, Tumechoka. Wakati Mketona wenzake wanateswa, askari wa JWTZ walieleza kuwa wamepewa ruhusa ya kupiga hata kuua wakorofi wachache na hawatachukuliwa hatua zozote. Hatima utekelezaji wa kauli hiyo unaendelea katika maeneo mbali mbali ya Nchi kama vile Mtwara na Handeni Kata ya Misima.

b) Madawa ya kulevya
Baraza Kuu linasikitishwa na kukithiri kwa biashara ya madawa ya kulevya, huku Vyombo vya Dola vikijikita zaidi katika kushughulikia Viongozi wa Dini, Vyama vya Siasa na Wananchi kadhaa katika maeneo mbali mbali na kwa kutumia Nguvu kubwa na rasilimali nyingi zaidi ili kutia khofu wananchi wasiweze kuhoji na kuisimamia Serikali ya CCM kwa ahadi walizotoa kwa Watanzania.

Baraza Kuu linasikitishwa na kuona kuna mapungufu makubwa kwa Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya kilichopo Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam mpaka kufikia Waziri wa Uchukuzi Dr Harison Mwakyembe kushughulikia jambo hilo.

Waziri wa Uchukuzi ana majukumu mazito ya kusimamia reli, bandari, viwanja vya ndege usafirishaji na uchukuzi kwa ujumla. Polisi na Wizara ya Mambo ya ndani iko wapi mpaka Waziri wa Uchukuzi ndiye aende kusimamia kukamatwa kwa wanaosafirisha madawa ya kulevya kupitia Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Serikali haiko makini katika kupambana na uhalifu wa madawa ya kulevya kama inavyodhihirishwa na hatua sahihi ya kumsimamisha au kumfukuza kazi Askari Polisi mwenye cheo cha Koplo ambae utekelezaji wa majukumu yake usingeweza kuzuwia uingizaji au usafirishaji wa Madawa hayo kupitia eneo lake la kazi na badala yake aliepaswa kupewa adhabu hiyo ni kiongozi wake ambae ndie Muhusika Mkuu wa Masuala ya Ukaguzi wa Madawa ya Kulevya.

b)Kupigwa Risasi kwa Sheikh Ponda.
Baraza Kuu linalaani vikali tendo la kupigwa risasi Sheikh Ponda na linaitaka Serikali kuunda Tume Huru itakayochunguza suala hili kama illivyoundwa Tume Huru kwenye matukio kadhaa ya uvunjwaji wa Haki za Binadamu. Baraza Kuu linamtaka Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Christopher Shilogile ajiuzulu kupisha uchunguzi wa tukio hili la kikatili dhidi ya Sheikh Ponda.

c) Mahusiano yetu na Rwanda
Baraza Kuu linatambua mantiki na kuunga mkono ushauri aliotoa Rais Kikwete kuwa njia muhimu ya kumaliza migogoro ya kisiasa na kiusalama na kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni kwa nchi jirani za Kongo, ikiwemo Rwanda na Uganda zenye waasi toka nchi zao waliokimbilia Kongo ni kuzungumza na kufikia muafaka wa kisiasa na mahasimu na waasi wao. Ushauri wa Rais Kikwete umetafsiriwa visivyo nchini Rwanda na kusababisha kuzorota kwa uhusiano kati ya nchi zetu mbili. Ukilinganisha na nchi jirani Tanzania ina ukomavu mkubwa wa kisiasa na kidiplomasia. Baraza Kuu linatoa wito kwa Rais Kikwete kutafuta njia za kidiplomasia ili kuweza kutatua mgogoro wa kisiasa unaoanza kujitokeza na kuhatarisha maelewano baina yetu na Rwanda.

d) Sakata la Rwanda na Uganda Kutotumia Bandari ya Dar es Salaam
Baraza Kuu la Uongozi limesikitishwa na Kufadhaishwa na hatua iliotangazwa na Rwanda na Uganda, kuhusu kutotumia Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu ya ubabaishaji wa kiutendaji wa Mamlaka ya Bandari, ubabaishaji wa Vyombo vyetu vya Dola kama Jeshi la Polisi, askari wa Usalama Barabarani na miundombinu mibovu ya Barabara na Bandari zetu.

Baraza Kuu linaitaka Serikali kulitazama jambo hili katika sura ya kiuchumi na siyo vyema kulitazama jambo hili katika mtazamo wa kisiasa ili kuweza kuwa na Mkakati wa Kunusuru hali hii. Bandari ya Dar es Salaam haifanyi kazi kwa ufanisi. Utafiti wa Benki ya Dunia unaonyesha kuwa, ikiwa bandari ya Dar es Salaam itafanya kazi kwa ufanisi kama bandari ya Mombasa, pato la taifa la Tanzania litaongezeka kwa dola bilioni 1.8 kila mwaka sawa na asilimia 7 ya pato la taifa la sasa. Nchi jirani zinazotumia bandari ya Dar es Salaam zitaongeza mapato yao kwa dola milioni 800. Utendaji mbovu wa bandari zetu unatokana na ombwe la uongozi, ufisadi na menejimenti mbovu.

Tanzania inaweza kukuza uchumi wake kwa asilimia 10 kila mwaka na kuongeza ajira kwa wingi ikiwa itatumia fursa za jiografia zikiwemo bandari zake kuwa kituo cha usafirishaji, viwanda na biashara kwa nchi sita zinazopakana na Tanzania na ambazo hazina bandari.

e) Kuhusu Matukio Kadhaa ya Mauaji na Tume za Uchunguzi zilizoundwa kuchunguza Matukio hayo.

Baraza Kuu linaitaka serikali kutoa taarifa juu ya Ripoti za Uchunguzi zilizowasilishwa na Tume hizo ili Wananchi wapate kujua ukweli wa matukio hayo na hatua zinazochukuliwa baada ya upatikanaji wa taarifa hizo.

f) Uwepo wa Watendaji Bandia wa Jeshi la Polisi.

Baraza Kuu limepokea na kujadili taarifa za uwepo wa askari bandia katika Jeshi la Polisi upande wa Usalama Barabarani na askari wa kawaida, nakufikia maazimio yafuatayo:
Baraza linaona na kusisitiza uwepo wa Ombwe la Uongozi , jambo ambalo linapelekea utendaji mbovu wa Jeshi la Polisi na kupelekea wananchi na hata Jumuiya ya Kimataifa kukosa imani na Uongozi wa Nchi yetu. Moja ya sababu ya Rwanda na Uganda kuamua kutotumia Bandari ya Dar es Salaam ni utendaji mbovu wa vyombo vyetu vya dola likiwemo Jeshi la Polisi.

5. Kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamuhuri wa Tanzania.
Kuhusu Rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Baraza Kuu linaipongeza Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Katiba inayoongozwa na Jaji Warioba kwa kupokea Mapendekezo ya CUF-Chama cha Wananchi na kuyaingiza kwenye Rasimu ya Katiba Mpya. Mambo yaliyopendekezwa na CUF na kuingizwa kwenye Rasimu ya Katiba Mpya ni pamoja na mfumo wa Muungano wa serikali tatu, kuruhusiwa mgombea binafsi, Rais kutangazwa kushinda akipata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe kwa wale wawili walio ongoza kwa kura, Tume huru ya uchaguzi, Mawaziri kutokuwa wabunge, Spika kutokuwa mbunge, haki za watu wenye ulemavu, kupanuliwa kwa haki za binadamu.

Baraza Kuu linaitaka Tume ya Jaji Warioba kuhakikisha inakamilisha suala la andiko la Katiba Mpya yenye Tume Huru ya Uchaguzi kama ilivyowaahidi Watanzania.
6. PROGRAM YA CHAMA SEPT-JULY,2013 NA UCHAGUZI WA NDANI YA CHAMA.
Baraza kuu limeiagiza Kamati ya Utendaji Taifa kuendelea na maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama kwa kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unaratibiwa vizuri ili kupata viongozi makini kwa ngazi zote watakaoweza kukipatia ushindi mkubwa chama chetu katika chaguzi zijazo.

MWISHO;

The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) na viongozi wake inawahakikishia Watanzania wote juu ya uwezo wake kwa kushirikiana na wananchi wote wa kuandaa sera mbadala za nchi yetu ya kutekeleza mabadiliko wanayoyataka watanzania kwa kuwa na AGENDA YA MAENDELEO KWA WOTE (AGENDA FOR INCLUSIVE DEVELOPMENT) Tunatoa wito kwa Watanzania kujiunga na CUF - Chama cha Wananchi ili kwa pamoja tuweze kupata Serikali makini yenye mipango na usimamizi mzuri wa mali asili na rasilimali za Taifa letu itakayokuza uchumi unao ongeza ajira kwa manufaa na maendeleo ya wananchi wote.

HAKI SAWA KWA WOTE.
 

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>