Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein afanya mazungumzo na wabunge wa Ireland

$
0
0

 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

  Zanzibar                                                                                                         13.12.2014

---

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Wabunge wa Bunge la Ireland na kuwaeleza mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa huku viongozi hao wakiahidi nchi yao kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
 
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Wabunge hao huko Ikulu mjini Zanzibar ambapo wabunge hao waliongozwa na Balozi wa Ireland nchini Tanzania Mhe. Fionula Gilsenan.
 
Katika maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao hatua mbali mbali zilizopitiwa katika kuanzisha Serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa ikiwa ni pamoja na marekebisho katika vipengele vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
 
Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa hapa nchini kumeweza kuleta mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na mashirikiano katika kuendeleza na kukuza uchumi wa nchi sambamba na kuimarisha amani na utulivu uliopo.
 
Alisisitiza kwamba kubwa kuliko yote ni kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuwepo hapa nchini ambapo yeye akiwa ni kiongozi na Rais wa Zanzibar ameweza kuhakikisha hilo linaendelezwa kwa mashirikiano ya wananchi na viongozi wao.
 
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi zake kwa Ireland kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano kati yake na Zanzibar na kusisitiza haja ya kuimarishwa zaidi ushirikiano kupitia Shirika lake la misaada.
 
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa nchi hiyo imeweza kusaida katika sekta ya afya, miundombinu na mawasiliano, huduma za zimamoto, ufugaji na sekta nyenginezo.
 
Dk. Shein pia, aliueleza uongozi huo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya uvuvi na kueleza changamoto zilizopo hivi sasa ikiwa ni pamoja na azma ya kufikia uvuvi katika bahari kuu hatua ambayo inaweza kuungwa mkono na nchi hiyo ambayo tayari imepata mafanikio katika sekta hiyo.
 
Alisema kuwa bado kuna eneo kubwa la bahari ya Zanzibar ambalo halijafikiwa katika kutekeleza shughuli za uvuvi licha ya kuwa na rasilimali za kutosha, hiyo ni kutokana na ukosefu wa miundombinu na utaalamu katika kuendeleza sekta hiyo.
 
Katika maelezo hayo pia, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii ambayo ni sekta mama katika kuinua uchumi wa Zanzibar.
 
Dk. Shein aliwataka viongozi hao kuitumia fursa hiyo ya ziara yao hapa Zanzibar kwa kutembelea katika maeneo mbali mbali ya kitalii ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Zanzibar nchini kwao.
 
Nao viongozi hao kwa nyakati tofauti walieleza kufarajika kwao katika ziara yao hapa Zanzibar sambamba na mapokezi mazuri waliyoyapata ambayo yanatokana na ukarimu wa Wazanzibari wa kupenda wageni huku wakipongeza mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa chini ya uongozi wa Dk. Shein.
 
Wabunge hao walitumia fursa hiyo kueleza  mafanikio ya kisiasa yaliopatikana nchini Ireland pamoja na changamoto mbali mbali zilizopo ambazo hivi sasa zimeweza kupatiwa ufumbuzi kwa mashirikiano ya nchi mbali mbali ikiwemo Marekani, Uingereza, Canada, Jumuiya ya Ulaya na nyenginezo.
 
Aidha, Wabunge hao mbali ya maelezo yao kadhaa pia, walimueleza Dk. Shein juhudi wanazozichukua katika kuhakikisha ushirikiano na uhusiano kati ya Ireland na nchi za Afrika unaendelezwa kupitia Umoja wa Wabunge wa Afrika na Ulaya ‘AWEPA’.
 
Wabunge hao kutoka chama tawala na chama cha upinzani nchini Ireland, pia walieleza mashirikiano yaliopo kati ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania na Bunge la Ireland ambapo ujio wao unatokana na uhusiano mwema wa pande hizo ambapo tayari Wabunge wa Tanzania wameshafanya ziara kama hiyo mwezi  Julai mwaka huu kwa lengo la kujifunza na kukuza ushirikiano wa pamoja.
 
Wakieleza lengo la uhusiano na ushirikiano huo ni pamoja na kuendeleza maeneo ambayo bado hayajapewa kipaumbele likiwemo eneo la uvuvi ambalo ukusanyaji wake wa mapato ni tofauti na sekta nyengine, hivyo linahitaji msukumo.
 
Miongoni mwa viongozi walioambatana na Wabunge hao ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Wawi Mhe. Hamad Rashid  Mohammed akiwa pamoja na  maafisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>