Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein ahimiza mashirikiano na maelewano katika kusimamia michezo

$
0
0
  

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

  Dar-es-Salaam                                                                                                 13.12.2014
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza ushirikiano na maelewano ndani ya vilabu pamoja na taasisi zinazosimamia michezo nchini na kukipongeza Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kwa kazi nzuri inayofanya.
 
Dk. Shein aliyasema hayo katika sherehe ya kukabidhi Tunzo kwa wanamichezo bora wa mwaka 2013, huko katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar-es-Salaam sherehe ambazo zimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
 
Katika hotuba yake Dk. Shein alisema kuwa bila ya kuwepo ushirikiano na maelewano mazuri, uendeshaji wa shughuli za michezo utakuwa na changamoto nyingi na kueleza kuwa michezo imekwua ikiwaunganisha Watanzania kwa lengo la kuendelea kuwa wamoja, wenye mshikamano na kusahau tofauti zao ziliopo zikiwemo za kisiasa, dini, kabila ama rangi.
 
Dk. Shein ambaye ana rikodi nzuri katika anga za michezo enzi zake, aliendelea kueleza kuwa michezo hujenga udugu, huimarisha mapenzi baina ya wanachama, wapenzi, wachezaji na washabiki wa timu mbali mbali na kueleza kuwa hivi sasa kila mmoja anashuhudia kuwa michezo ni chem chem ya furaha na si kuleta maudhi kwenye jamii.
 
Alisema kuwa michezo ina umuhimu mkubwa katika historia ya Tanzania ambapo imeweza kusaidia sana kuwaunganisha Watanzania katika nyakati mbali mbali akitolea mfano chama cha ASP ambacho kinatokana na chama cha African Association na Shirazi Association ambapo African Association chimbuko lake ni vuguvugu la michezo.
 
Dk. Shein ambaye alikubali ombi la TASWA kuwa mlezi, alieleza kuwa inafurahisha kuona kuwa chama hicho kinathamini umuhimu wa michezo na tangu kuundwa kwake zaidi ya miaka 40 iliyopita imefanya mambo mengi ya msingi katika kukuza vipaji vya wanamichezo nchini na  waandishi wa habari za michezo.
 
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa wakati umefika wa kuifanya Tanzania itajike katika michezo mbali mbali katika ngazi za Kikanda na Kimataifa kwani katika mashindano ya michezo katika ngazi za Kimataifa bado Tanzania haifanyi vizuri.
 
Alisema kuwa jitihada za ziada katika kuimarisha mpira wa miguu, riadha, netiboli na michezo mengine yote inayopendwa na Watanzania sambamba na kuwandaa wanamichezo wenye kuweza kufikia kiwango cha mabingwa wa zamani mfano Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na wengineo.
 
Kwa maelezo ya Dk. Shein kinachotakiwa hivi sasa ni kuimarisha uongozi na utendaji wa vyama na vilabu vya michezo ili muda mwingi utumike katika kuendeleza vipaji vya michezo badala ya hali iliopo hivi sasa ya kulaumiana.
 
"Lawama zisizokuwa na msingi hazijengi bali hubomoa hivyo tunahitaji kushirikiana na kujenga ari kwa pamoja",alisema Dk. Shein.
 
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa wakati umefika kwa vyama au vilabu vya michezo kuanzisha shule au vituo vya michezo kama ilivyokuwa ikifanya hapo zamani ili kukuza vipaji vya vijana mapema kama inavyofanyika katika nchi za nje.
 
Alisema kuwa kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano kunawafanya vijana walio wengi kuutumia muda mwingi sana kwa kutimiza michezo badala ya kushiriki katika michezo. " Utawakuta vijana wanawajua wachezaji wa timu za Ulaya bila ya kusoma popote lakini majina ya walimu wa skuli yake hayafahamu",alisema Dk. Shein.
 
Alisema kuwa Serikali zote mbili zimeweka mkazo maalum katika kurejesha michezo mashuleni kwa kutambua kuwa maskuli ndio chem-cehm ya kutoa wanamichezo wenye vipaji.
 
Nae Waziri wa  Habari, Vijana, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Tanzania Bara Mhe. Dk. Fenella Mkangara alisema kuwa jitihada za pamoja zinahitajika katika kuimarisha sekta ya michezo na kusisitiza haja ya kuwaenzi wanamichezo kuwa ni la kila mtu.
 
Mapema uongozi wa TASWA ulitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa kukubali mwaliko huo ambapo pia, ulieleza vigezo vilivyotumika katika kuwapata watunukiwa tunzo hao.
 
Akitoa wasfu wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambaye ametunikiwa tunzo ya heshima ya wanamichezo Bora, Mwandishi wa Habari Mkongwe Salim Said Salim alisema kuwa anamfahamu Mzee Karume kuwa mwanamichezo katika michezo ya dhuna, karata, bao pamoja na mpira wa miguu.
 
Alisema kuwa Marehemu hakuwa akifuatilia soka la visiwani peke yake bali alikuwa mpenzi mkubwa wa Yanga na klabu ya Liverpool ya Uiengereza ambapo baada ya kujenga uwanja wa Amani Mzee Karume alitoa Shilingi 200,000 ambapo kwa thamani ya sasa ni Tsh. Milioni 60 kwa ajili ya kujenga klabu ya Yanga iliyopo Jangwani na baadae akaisaidia Simba ili nayo ijenge jengo la klabu yake hapo Msimbazi.
 
Katika sherehe hizo Dk. Shein alimtunukia tunzo hiyo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambayo ilipokelewa na Mjane wake Bibi Fatma Karume ambaye baada ya kupokea tunzo hiyo alitoa shukurani kwa waandaaji na kutoa wito wa kuimarisha michezo sambamba na kusisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi.
 
Mzee Karume ameshinda tuzo maalum ya watu waliotoa mchango mkubwa kwenye michezo ikiwa ni pamoja na kuziwezesha Simba na Yanga kumiliki majengo yao. Aidha, Dk. Shein alitoa tunzo kwa Mwanamichezo bora wa Tanzania wa Mwaka 2013 Sherida Bonifas.
 
Wengine waliopata tunzo hizo ni kiungo wa Azam FC, Erasto Nyoni ameshinda tunzo ya Mwanasoka Bora ya Chama cha Waaandishi wa Habari Tanzania (TASWA), wakati Sheridah Boniface amekuwa mwanamichezo bora wa mwaka 2013/2014.
 
Nyoni aliyeibukia Vital`o ya Burundi, ameshinda tunzo baada ya kuwangusha Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub `Cannavaro` na mshambuliaji wa Simba Elias Maguli.
 
Nae mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta ameshinda tuzo ya mwanamichezo bora anayecheza nje, wakati Kipre Tchetche wa Ivory Coast amewashinda Mbuyu Twite (Rwanda) na Amis Tambwe wa Burundi katika tuzo ya mwanasoka wa kigeni nchini.
 
Sheridah ameshinda tuzo tatu, mwanamichezo bora wa jumla, mwanasoka bora wa kike na mwanamichezo bora chipukizi, Novatus Emmanuel ameshinda katika Tenis ya walemavu wanaume na kwa wanawake Rehema Said, Magongo ameshinda Joan Wilson na Kidawa Suleiman, Wavu wameshinda Teddy Mgwao na Kevin Peter, Riadha ni Alphonce Felix na Zakia Mrisho.
 
Katika kikapu Ahmed Liyamaiga, wakati netiboli ni Dolita Mbunda, Kuogelea mshindi ni Hilal Hila na Catherine Masoon, mshindi wa judo, Godfrey Mtao na Grace Mhanga.
Tenisi Omar Sule na Rehema Athumani, ngumi za kulipwa ni Francis Cheka, ridhaa ni Suleimani Kidunda, katika mshindi wa gofu ni Hassan Kadio wakati kwa ridhaa Nuru Mollel, Baiskeli Sofia na Richard Laizer.
 
Mpira wa mikono ni Ahmed Saleh na Veronica Mapunda ambapo Olimpiki maalumu ni Raphael Kalukula na Brandina Brasi.
 
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Tanzania Bara Dk. Fenella Mkangara, Kaimu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Zanzibar Mhe. Abdillah Jihad Hassan,Mkuu wa Mkoa wa Dar-es Salam  Mhe. Said Meck Sadik, pamoja na viongozi wa michezo mbali mvali na waandishi wa habari kutoka pembe zote za Tanzania.
 
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>