Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Kampeni tatu za Katiba zaibuka Zanzibar

$
0
0
Na Mwinyi Sadallah
 
 Makundi matatu yameibuka visiwani Zanzibar yakifanya kampeni tatu tofauti ikiwamo ya kuunga mkono, kupinga Katiba Inayopendekezwa na kususia kufanyika kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa mwakani.
Kampeni hizo zimeanza kuibua hali ya wasiwasi kuhusu kufikiwa malengo ya kupata Katiba Mpya, baada ya kupitishwa kwa asilimia 50 ya Wazanzibari kama masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inavyosema kupitia mfumo wa kura ya maoni.
Hata hivyo, iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa, Tanzania itakuwa imefanikiwa kuandika historia mpya baada ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya kuwa na Katiba inayotokana na ushirikishwaji wa wananchi wake.
Tayari visiwa hivyo vinashuhudia mjadala wa aina yake kutokana na viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kugawanyika akiwemo Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein ambaye amekuwa akiwataka wananchi kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa kinyume na msimamo wa msaidizi wake, Makamu wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Akihutubia mikutano ya hadhara visiwani humo hivi karibuni, Dk Shein alisema kwamba Katiba Inayopendekezwa imezingatia masilahi ya Zanzibar na watu wake na itasaidia kufungua milango ya kiuchumi, hasa baada ya suala la mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Katika mikutano yake Rais Shein amekuwa akiwapa nafasi wasaidizi wake wengine kupigia chapuo Katiba Inayopendekezwa katika majukwaa akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, Waziri wa Dhamana wa Ardhi, Ramadhan Abdalla Shaaban, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini.
Wakisaidiwa na watendaji wakuu wa CCM Zanzibar akiwamo Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai na Makamu Mwenyekiti wa UWT, Asha Bakary Makame ambao walisema kimsingi Katiba Inayopendekezwa imezingatia makundi mbalimbali katika jamii wakiwamo watu wenye ulemavu, wanawake na watoto.
Wakati viongozi hao wakitetea Katiba hiyo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alisema kwamba Katiba hiyo haikuzingatia masilahi ya Zanzibar ya kiuchumi na uhusiano wa kimataifa katika mfumo wa Muungano wa Serikali mbili unaopendekezwa kinyume na Rasimu ya Katiba iliyotokana na wananchi na kupendekeza Muungano wa Serikali tatu.
Maalim Seif katika mikutano yake ya hadhara amekuwa akiongezewa nguvu za kisiasa na mawaziri kutoka chama chake cha CUF, wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa akiwamo Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Juma Duni Haji, Waziri wa Viwanda na Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazruy na Waziri wa Sheria na Katiba Abubakar Khamis.
Maalim Seif alisema kwamba Katiba Inayopendekezwa aina tofauti na ile ya mwaka 1977 na kuendelea kusisitiza kuwa ataendelea kudai mamlaka kamili ya Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kwa upande wake Waziri wa zamani wa SMZ, Mansoor Yusuph Himid na Kiongozi Mwandamizi wa Kamati ya Maridhiano alisema kwamba itakuwa mwafaka kama wananchi wa Zanzibar watasusia Kura ya Maoni kwa sababu Katiba Inayopendekezwa haikutokana na maoni ya wananchi.
“Kitendo cha kujitokeza kupiga kura ya maoni sawa na mtu kushiriki kula chakula ambacho hukushiriki kupanga bajeti yake, upishi au kupakua,” alisema Mansoor.
 
Akizungumza katika Kongamano la Katiba alisema kama Katiba hiyo itapitishwa italeta mgangano mkubwa katika matumizi ya ardhi kutokana na jambo hilo kuingizwa katika mambo ya Muungano wakati mafuta na gesi yakiondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
 
Chanzo: Mwananchi

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>