Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein alipongeza Shirika la afya duniani kwa kuiunga mkono Zanzibar sekta ya afya

$
0
0


  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                         15.12.2014
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya ambazo zimeweza kupata mafanikio makubwa na kuzidi kuijengea sifa ndani na nje ya nchi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na  uongozi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ukiongozwa na Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Rofaro Chatora aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa lengo la kumtambulisha Mwakilishi mpya wa Shirika hilo kwa upande wa Zanzibar Dk. Andemichael Ghirmay Redae.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumkaribisha Mwakilishi huyo mpya wa (WHO) nchini na kumueleza kuwa Shirika hilo limekuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na Zanzibar  ambalo limeweza kutoa misaada mbali mbali katika huduma za afya na elimu hapa nchini.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika licha ya kuendelea kuungwa mkono na Washirika wa maendeleo likiwemo shirika la (WHO).

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar inathamini sana misaada ya Shirika la (WHO) ambayo imekuwa ikiitoa hapa Zanzibar kwa muda mrefu  hatua ambayo imewezesha kupiga vita maradhi mbali mbali yakiwemo Malaria, maambukizi ya virusi vya UKIMWI, vifo vya akina mama na watoto na mengineyo.

Alisema kuwa mbali ya juhudi hizo ongezeko la idadi ya watu hapa nchini pamoja na suala la bajeti ni miongoni mwa changamoto ambazo serikali imekuwa ikikabiliana nalo ambapo hata hivyo juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini.

Kwa upande wa kinga pamoja na matayarisho kwa maradhi ya kuambukiza kama vile Ebola, Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendelea kuweka mikakati katika kutekeleza hatua hizo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuchukua hadhari juu ya ugonjwa huo.


Nae Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Bwana Rofaro Chatora kwa upande wake, alimueleza Dk. Shein kuwa Shirika hilo limejikita katika maeneo sita ikiwa ni pamoja na kuhakikisha malengo ya Milenia yanafikiwa katika sekta ya afya pamoja na kusukuma ama kuchangia huduma za afya ili sekta hiyo izidi kuimarika.

Kwa maelezo ya Mwakilishi huyo wa (WHO) nchini, eneo jengine ni kuendeleza huduma muhimu zikiwemo bajeti kwenye sekta hiyo, kujihusisha zaidi katika kupiga vita maradhi yasioambukiza ambayo hivi sasa yameshika kasi kwa kama vile maradhi ya moyo, kisukari na mengineyo.

Aidha, kuimarisha  huduma za kijamii kama vile maji safi na salama, makaazi mazuri sambamba na kujiweka tayari kwa kinga katika kuyakabili maradhi mbali mbali ya kuambukiza kama vile ugonjwa wa Ebola ambao umekuwa tishio hivi sasa.

Katika suala zima la kujikinga na kujitayarisha na maradhi ya kuambukiza, Chatora alisema kuwa umefika wakati kwa Zanzibar kuweka mikakati maalum katika kujikinga na maradhi hayo.

Alieleza kuwa licha ya kuwa ukanda huu wa Tanzania ikiwemo Zanzibar dalili za ugonjwa huo ikifananishwa na  maeneo ya Magharibi mwa Afrika suala la kinga na matayarisho ya kuyakabili maradhi hayo ni jambo lisiloepukika.

Mwakilishi huyo alisisitiza kuwa katika hatua hiyo ya kujikinga na ugonjwa huo thakili si Wizara ya Afya peke yake yenye jukumu la kupambana na ugonjwa huo bali ni jukumu la  Wizara zote zilizomo ndani ya  Serikali zikashirikiana pamoja katika vita hivyo.

Nae Mwakilishi mpya wa Shirika hilo anaefanyia kazi zake Zanzibar Dk. Andemichael Ghirmay Redae amekiri juhudi zinazochukuliwa na Zanzibar katika kuiamrisha huduma za afya na kueleza haja ya kuimarisha mikakati huku akiahidi kutoa ushirikiano wake kwa upande wake kwa kupitia Shirika la WHO analolifanyia kazi hapa Zanzibar.

Mwakilishi huyo wa Zanzibar alieleza kuwa kuimarika kwa huduma za afya hapa Zanzibar ni suala muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ni visiwa vya kitalii.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Saleh Mohammed Jidawi alieleza mashirikiano sambamba na juhudi zinazochukuliwa na Shrikala (WHO) hapa Zanzibar katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma za afya na za kijamii.

Kwa maelezo ya Dk. Jidawi, miongozi mwa juhudi ambazo (WHO) imekuwa ikiendelea kuiunga mkono Zanzibar ni pamoja na kusaida maabara ya afya ya umma kisiwani Pemba ambayo ni kituo cha utafiti wa maradhi ya kuambukiza  pamoja na kuisaidia maabara ilioko katika Hospitali ya Mnazimmoja mjini Unguja ili kuendelea kupata hadhi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>