Muandishi wa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Faki Mjaka akiuliza maswali kwa Katibu Mtendaji wa Chama cha Mchezo wa Mazoezi ZABESA Ameri Mohd Makame kuhusiana na Maadhimisho ya siku ya mazoezi Kitaifa ambayo yatafanyika kwa mara ya kwanza 01/01/2015 Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Muandishi wa Habari kutoka Chuchu FM Radio Yahya Saleh akiuliza maswali kwa Katibu Mtendaji wa Chama cha Mchezo wa Mazoezi ZABESA Ameri Mohd Makame kuhusiana na Maadhimisho ya siku ya mazoezi Kitaifa ambayo yatafanyika kwa mara ya kwanza 01/01/2015 Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Mchezo wa Mazoezi ZABESA Amer Mohd Makame akielezea madhumuni ya kufanyika kwa Tamasha la kwanza la siku ya mazoezi 01/01/2015 katika ukumbi wa Wizara ya habari Utamaduni Utalii na Michezo alipokutana na Waandishi wa Habari Zanzibar.
Mwenyekiti wa Chama cha Michezo wa Mazoezi ZABESA Mohd Zidi akifafanua jambo katika mkutano na Waandishi wa Habari kuhusiana na Maadhimisho ya siku ya Mazoezi Kitaifa 01/01/2015 yatakayo fanyika Uwanja wa Amaan Zanzibar,ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein,na Ujumbe wa Mwaka huu ni Fanya Mazoezi Imarisha Afya yako Epuka Maradhi yasioambukiza.
PICHA NA YUSSUF SIMAI-HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
Na Abdulla Ali-Maelezo Zanzibar
Chama cha mchezo wa mazoezi ya viungo Zanzibar (ZABESA) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo kimeandaa maadhimisho ya siku ya mazoezi ya kitaifa yatakayofanyika Januari 1 mwaka 2015 katika uwanja wa Amani.
Maadhimisho hayo yatakayofanyika majira ya Asubuhi yatahudhuriwa na watu mbalimbali ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Moh’d Shein anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Kikwajuni mjini Zanzibar, Katibu mtendaji wa ZABESA Ameir Mohammed Makame amesema maadhimisho hayo yatafuatiwa na matembezi yatakayoanzia Uwanja wa Tumbaku, Miembeni kupitia Ng’ambu stesheni, Mfereji wa wima, Mikunguni na kumalizia uwanja wa Amani.
Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi, kwani ni muhimu kwa mwanadamu kimwili na kiakili na husaidia kuimarisha afya zao kwa ujumla.
Akitaja miongoni mwa faida hizo katibu huyo amesema ni pamoja na kutanua mifumo ya mishipa ya damu, kupunguza mafuta na sukari iliyozidi mwilini na kuimarisha misuli yote ya mwili.
“Vyakula tunavyokula mara nyingi vinakua havina ubora kwani vinakua na mafuta mengi na kemikali na kusababisha matatizo mengi kiafya ikiwemo maradhi ya shindikizo la damu, kensa, uzito uliokithiri na mengne mbalimbali” amesema Katibu Ameir.
Aidha alisema matumizi ya teknolojia na kukua kwa uchumi kumesababisha watu kukaa kitako kwa muda mrefu kuangalia television, kutopenda kutembea na matumizi holela ya vyombo vya usafiri hupelekea kupata maradhi yasiyoambukiza kama vile presha na kisukari.
Katika shamrashamra ya maadhimisho hayo Vilabu vya mazoezi zaidi ya 70 kutoka Tanzania Bara na Visiwani vinatarajiwa kuungana pamoja katika maadhimisho hayo.
Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein ameiasisi Januari mosi kuwa siku ya mazoezi ya kitaifa Zanzibar ambapo Wananchi hujumuika na kufanya mazoezi mbalimbali ya Viungo ikiwemo kutembea na kukimbia.
Kikundi cha ZABESA kilianzishwa rasmi mwaka 2010 na kusajiliwa na mrajisi mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo ujumbe wa mwaka huu ni;“Fanya mazoezi, imarisha afya yako na epuka maradhi yasiyo ya kuambukiza”.