Mwantanga Ame, Dodoma
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemamliza kikao chake cha siku tatu chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ikiwa imeridhia mapendekezo kadhaa ya Kamati Kuu ya CCM, ikiwemo kumfuta uanachama Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki Zanzibar, Mansoor Yusuf Himid.
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Nape Nnauye alisema baadhi ya tuhuma alizokutwa nazo Mansour ni kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama na kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya miongozi wa CCM.
Tuhuma nyengine ni kuikana ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM.
Alisema baada ya kujiridhisha vya kutosha na tuhuma dhidi Mansoor,Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) imeridhia uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi Zanzibar wa kumfukuza uanachama.
Alisema Kwa uamuzi huo wa kumvua uanachama Mansoor, yeye kwa sasa sio kiongozi tena wa CCM.
Kikao hicho pia kimeridhia, uteuzi wa Makatibu wateule wapya wa Jumuia za CCM, za Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuia ya Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Katika uteuzi huo, mapendekezo hayo yaliyofanywa na Kamati Kuu ya CCM, na kuridhiwa na NEC, kwa upande wa Umoja wa Vijana wa CCM ameteuliwa aliyekuwa Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, Sixtus Mapunda kuwa Katibu Mkuu na kwa upande wa Jumuia ya Wazazi ni mjumbe wa NEC kutoka Pemba, Seif Shabani Mohamed, huku kwa upande wa UWT akiachwa Katibu Mkuu wa sasa, Amina Makilagi.
Mapunda atachukua nafasi iliyokuwa imeshikiwa na Martine Shigela ambaye ameongoza UVCCM kwa miaka mitano sasa, na Seif Shabani Mohammed kutoka Pemba akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Khamis Suleiman Dadi ambaye pia amekuwa katika wadhifa kwa miaka mitano sasa.
Pia, NEC imeridhia mapendekezo ya Kamati Kuu kwa ajili ya kuziba nafasi Makatibu wa CCM wa mikoa mitatu ya Morogoro, Kaskazini Pemba na Geita ambayo kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa imekuwa wazi kwa muda mrefu sasa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.
Kufuatia mapendekezo hayo ya Kamati Kuu, ambayo yameridhiwa na NEC, walioteuliwa na mikoa yao ikiwa kwenye mabano ni Msaidizi Kitengo cha Uchaguzi, CCM Ofdisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Romuli Rojas John (Morogoro), aliyekuwa Katibu wa wilaya ya Mkinga, Kassim Mabrouk Mbarak (Kaskazini Pemba) na aliyekuwa Katibu wa CCM Igunga, Mary Maziku (Geita).
Kuhusu sakata la madiwani wa Bukoba mjini, CCM imesema suala hilo, linaendelea kushughulikiwa ambapo baada ya kikao hicho cha NEC, Kamati kuu iliendelea kukutana na viongozi wa wilaya ya Bukoba, Mwenyekiti wa CCM na Katibu wa wilaya hiyo.
Mapema kabla ya kikao cha NEC, Kamati Kuu ilikutana na Mbunge wa Bukoba mjini, Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba mjini na kuwahoji, wakati juzi Kamati Kuu ilikutana na Mwenyekiti na Katibu wa CCM mkoa wa Kagera.
Kufuatia hatua hiyo chama cha Mapinduzi kitatoa taarifa kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi kuondoa udhamini wake kwa mwanachama huyo kama mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Kiembesamaki.
Hatua hiyo itamfanya Spika kutangaza kiti cha jimbo hilo kuwa wazi na kuitishwa uchaguzi mdogo wa kugombea nafasi hiyo.
Mansoor aliwahi kuwa Waziri asiekuwa na wizara maalum katika awamu ya saba inayongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo kabla ya kuwa Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi katika serikali ya awamu ya sita iliyoongozwa na Rais mstaafu, Amani Abeid Karume.