Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein : Vitambulisho ni suala la kisheria

$
0
0
Na Said Ameir
The Hague, Uholanzi
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali haina nia ya kuwanyima wazanzibari wanaoishi ughaibuni kitambulisho cha mzanzibari mkaazi isipokuwa suala hilo ni la kisheria hivyo kupewa kwake ni lazima mhusika atimize matakwa ya kisheria.
 
Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni nchini Uholanzi alipokuwa akizungumza na watanzania wanaoishi nchini humo wakati wa ziara yake ya siku tano kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo bwana Mark Rutte.
 
“Kitambulisho cha mzanzibari ni suala la kisheria hivyo mlengwa ni lazima atimize matakwa ya kisheria mojawapo ni la mwanachi kukaa katika eneo lake si chini ya miezi 36” alibainisha Dk. Shein na kuongeza kuwa mzanzibari mwenye sifa za kupata kitambulisho hicho ikitokea akanyimwa anayo haki ya kukata rufaa kwa mamlaka husika.
 
 Alieleza kuwa nia ya kuanzisha idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na kitengo kama hicho katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kunaonesha sio tu kuwatambua watanzania hao wanaoishi nje ya nchi lakini kunathibitisha dhamira ya kweli ya serikali ya kuwashirikisha watanzania popote waliko katika kuleta maendeleo ya nchi.

 Dk. Shein aliwapongeza watanzania hao kwa kufuatilia kwa karibu taarifa kutoka nyumbani na kuonesha kuguswa na baadhi ya matukio yanayotokea nchini ambayo baadhi yake yanaathiri taswira nzuri ya Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa. “nimefurahi kuona kuwa mnafuatilia kwa karibu matukio yanayotokea nchini kwetu.
 
Risala yenu imethibitisha maelezo yangu”alieleza Dk. Shein na kuwaomba watanzania kuwa karibu na Ofisi za Ubalozi za nchi yao ili kupata taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo nchini. Alisema si kila chombo cha habari au mitandao ya habari inatoa taarifa sahihi kuhusu Tanzania hivyo suala la kuwasiliana na Ofisi za kibalozi hawana budi kulizingatia.
 
Aliwaeleza watanzania hao kuwa ni jambo la kujivunia kuona Serikali imeufungua tena ubalozi wake nchini Uholanzi baada ya kufugwa kwa miaka mingi kutokana na sababu za kiuchumi. “Tuliufunga ubalozi wetu hapa kutokana hali mbaya ya kiuchumi lakini tumejipanga na tunaufungua upya. Balozi ameshateuliwa na harakati za kuundaa ubalozi zinaendelea”alieleza Dk. Shein na kumpogeza balozi Willison Masilingi kwa kuteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini humo.
 
 Alieleza hatua hiyo ni muhimu katika kuendeleza uhusiano wa Tanzania na Uholanzi kwa kuwa nchi mbili hizo zimekuwa katika mahusiano mazuri kwa miaka arobaini sasa. Akijibu swali kuhusu namna serikali inavyochukua hatua za kusafisha taswira ya nchi kutokana na matukio ya hivi karibuni ya kumwagiwa tindikali vijana wawili toka Uingereza huko Zanzibar Dk. Shein alieleza kuwa hatua zimechukuliwa na bado suala hilo limo mikononi mwa vyombo vya dola kwa uchunguzi. “Ni vitendo vilivyoanza muda mrefu tangu mtu wa kwanza kumwagiwa tindikali mwaka 1996. Hatujui lengo la watu wanaofanya vitendo hivi… ni matukio yanayotutia aibu, kuharibu sifa ya nchi yetu pamoja na kuhatarisha uchumi wetu. Hivyo Serikali inalichunguza suala hili (la tindikali) kwa makini sana” Dk. Shein aliwaeleza watanzania hao.
 
Alibainisha kuwa matukio kama hayo yanapotokea Serikali huchukua hatua za haraka ikiwemo kuieleza jumuiya ya kimataifa kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano zikiwemo za kidiplomasia na mawasiliano ya wazi kupitia vyombo vya habari.
 
Wakati huo huo watanzania wanaoishi nchini Uholanzi wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuufungua tena Ubalozi wake nchini Uholanzi. Shukrani hizo hizo zimetolewa wa Jumuiya ya watanzania wanaoishi Uholanzi katika risala yao kwa Rais wa Zanzibar.
 
Akisoma risala hiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya watanzania hao Bwana Bulemo Francis Kweba alisema kufunguliwa kwa ubalozi huo kutawapunguzia gharama za kufuata huduma za kibalozi mjini Bruxelles Ubelgiji ambako kwa sasa ndiko zinakopatikana.
 
 Katika risala hiyo watanzania hao waliiomba serikali kuweka utaratibu mzuri utakaosaidia wao kupata fursa mbalimbali nchini kama vile viwanja vya kujenga nyumba za kuishi na biashara pamoja na ardhi ya kilimo. Walishauri serikali kulishughulikia suala la uraia wa nchi mbili kwa kueleza kuwa lina manufaa makubwa kwa taifa kwani litachochea uwekezaji nchini kwa kuwa watanzania wengi wamelazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine ili kupata mahitaji ya msingi kama elimu, afya na ajira nzuri.
 
 Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia. Rais wa Zanzibar alimaliza ziara yake nchini Uholanzi jana na anatarajiwa kurejea nchini kesho (Jumapili).

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>