Dr. Ann Vndok wa Kliniki ya Tiba ya asili iliyopo katika Mtaa wa Vikokotoni akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif namna wanavyotoa huduma zao katika maadhimisho ya siku ya Waganga wa Tiba asili Afrika Hapo Victoria Garden Mnazi Mmoja.
Wataalamu wa Kliniki ya Tiba asili waliopo Vikokotoni wakiwa pamoja na Mrajiri wa Tiba asili Zanzibar Dr. Haji Kundi katika hafla ya maadhimisho ya siku ya Waganga wa Tiba asili Afrika
Balozi Seif akiangalia baadhi ya dawa Za Mwasele Herbalist Clinic ya Kikwajuni Weless kwenye maonyesho ya dawa za asili katika maadhimisho ya siku ya waganga wa tiba asili Afrika hapo Victoria Garden MnazI Mmoja Mjini Zanzibar
Balozi Seif akifurahia baadhi ya dawa na mafuta mbali mbali yaliyotengenezwa na huuzwa na wajasiri amali wa dawa za asilia wa Meli Nne wakiongozwa na Bibi Salma Khamis Mohd.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman KHamis Ame, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutambua umuhimu wa waganga wa Tiba asili itaendelea kushirikiana nao katika kuwaendeleza kwa kutoa elimu pamoja na kufanya utafiti wa dawa wanazotumia katika kutibu ili tiba yao iendane na sayansi na teknolojia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya 11 ya siku ya tiba asili Afrika yaliyofanyika katika uwanja wa Bustani ya Victoria Mnazi Mmoja na kushirikisha wawakilishi wa jumuiya za tiba asili hapa Nchini.
Balozi Seif alisema wakati umefika kwa waganga hao wa tiba asili kuondokana na ile tabia ya wengi kati yao kuficha taaluma walizokuwa nazo na hatimae kupotea kabisa taaluma hiyo wanapofariki Dunia kwa vile hushindwa kuwarithisha watoto au jamaa zao wa karibu.
Katika kufanikisha fani hiyo Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Waganya wa Tiba asili na Madaktari wa kisasa ili kuwapa fursa muhimu zaidi wagonjwa wanaowahudumia ambao walio wengi hapa nchini bado wanaimani ya kupendelea kutumuia tiba ya asili.
“ Ni wazi kuwa ushirikiano wa pande hizo mbili katika huduma zenu ni muhimu sana na ni vyema kwa mganga kutoa rufaa pale anapohisi taaluma yake imefikia kikomo na kuachana na tamaa ya fedha huku akielewa wazi kuwa uwezo wake wa kutibu ni mdogo katika maradhi husika “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba tiba asili hivi sasa imekuwa biashara kubwa Duniani na kuzitolea mfano China, Indonesia, India na Afrika Kusini ambazo zimepiga hatua kubwa katika kuajiri watu wengi pamoja na kuongeza mapato.
Balozi Seif aliwaomba wataalamu wa fani hiyo wapokutana kufikiria njia zitakazoisaidia Zanzibar kiuchumi kupitia fani hiyo kwa kupata fursa ya kusafirisha dawa za asili nje ya nchi kama zinavyofanya nchi nyengine Duniani.
Alieleza kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zimebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa miti shamba ya dawa kama zilivyo nchi nyengine ulimwenguni kufuatia utafiti uliofanywa na wataalamu kutoka Jamuhuri ya Watu wa China katika miaka ya 70.
Akizungumzia suala la mazingira Balozi Seif alisema ni jambo la kusikitisha kuona wananchi walio wengi wanaendelea na tabia ya kukata ovyo misitu asilia ambayo kwa kiasi kikubwa ndio inayotoa dawa za miti shamba zinazotumika kwenye tiba asilia.
Alifahamisha kwamba Serikali kwa upande wake itaendelea na jitihada za kuhifadhi miti asili chini ya sheria iliyopo ya mazingira ili tiba asilia iweze kuendelea kutoa huduma kwa kipindi kirefu kijacho.
Hata hivyo Balozi Seif alitahadharisha kwamba Serikali pekee haitaweza kuleta mafanikio bila ya ushiriki wa wananachi kikamilifu. Hivyo amewaomba waganga wa tiba asilia kuanzisha vitalu vya miti ambayo iko hatarini kupotea.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa vitalu hivyo mbali ya kusaidia kuhifadhi miti ya tiba asilia lakini pia vinaweza kuwa chanzo cha mapato kwa waganga hao kwa kuuziana miti ya tiba miongoni mwao au hata kusafirisha nje ya nchi ili kupata fedha za kigeni.
Katika kuunga mkono juhudi za waganga hao wa Tiba asili Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itajitahidi kusaidia kuwapatia waganga hao wa tiba asili eneo la kupanda miti kwa ajili ya shughuli zao hizo.
“ Tutawakatia eneo ili muweze kuotesha miti kwa ajili ya dawa zetu ili kuutumia utajiri mkubwa uliotuzunguuka ambao pia tutahitajika wataalamu wetu waufanyie utafiti wa kutosha kwa lengo la kupata tija zaidi “. Alisisitiza Balozi Seif.
Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Tiba asili na Mbadala Bibi Mayasa Salum Ali aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kupitisha sheria nambari nane ya mwaka 2008 ya kuwepo kwa Baraza hilo kisheria.
Bibi Mayasa alisema hatua hiyo imeweza kusaidia kuhamasisha waganga wa tiba asilia kujiunga na kuanzia jumuiya zao hali iliyopelekea kuwa na waganga wa tiba asili waliojisajili kufikia 162 Zanzibar, wasaidizi waganga wanane, Kliniki za dawa za tiba asilia Tisa, Maduka ya dawa za asili 31 pamoja na Viringe 28.
Mwenyekiti huyo wa Baraza la Baraza la Tiba asili na Mbadala alisema malengo ya Baraza hilo ni kuendelea kuelimisha jamii kupitia vyombo vya Habari, kujenga uhusiano mzuri kati ya Madaktari na waganga wa tiba asili.
Akitoa salamu za shirika la Afya Duniani { WHO } katika Maadhimisho hayo 11 ya waganga wa Tiba asili Afrika Mwakilishi wa shirika hilo hapa Zanzibar Dr. Pierre Kahodhi alisema Mataifa ya Bara la Afrika yanapaswa kuunga mkono utafiti wa dawa za asili ili ziendelee kusaidia afya na ustawi wa wananchi wao.
Dr. Pierre Kahodhi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani Hapa Tanzania Luis Gomez alieleza kwamba Siku hii ni muhimu katika kutafakari hatua za kuchukuwa kwenye tafiti za matumizi ya dawa za asili zisizo na Sumu.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya 11 ya waganga wa tiba asili Afrika Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji alisema Serikali itaendelea kuthamini mchango unaotolewa na waganga wa tiba asili Nchini .
Waziri Duni alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya haina ugomvi na watu wanaouza dawa za asili hasa kwenye misikitini baada ya wakati wa sala, lakini kinachosisitizwa kwa wauzaji hao ni kujisajili kwa kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia baraza la Waganga wa Tiba za asili Zanzibar.
Ujumbe wa mwaka huu wa siku ya Maadhimisho ya 11 ya Waganga wa Tiba ya Asili Afrika ni “ Tiba asili, Utafiti na Maendeleo"