Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein ahimiza kuendelezwa tafiti za historia ya uislamu Zanzibar

$
0
0
Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kuendelezwa tafiti zaidi juu ya historia ya uislamu Zanzibar ili kuweka kumbukumbu sahihi za kipindi ulipoingia na namna ulivyoingia nchini.
Dk. Shein ametoa wito huo leo wakati alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa Kuhusu Historia ya Ustaarabu wa Kiislamu Katika Afrika ya Mashariki linalofanyika kwa siku tatu katika hoteli ya La Gema huko Nungwi, Mkoa wa Kakazini Unguja.
Aliwaeleza washiriki wa kongamano hilo kuwa kumbukumbu za historia ya uislamu Zanzibar zinaonyesha simulizi tofauti kuhusu mwaka ulioingia na namna ulivyoingia hivyo ipo haja historia hiyo muhimu kufanyiwa tafiti zaidi ili kupata kumbukumbu sahihi.
“Kwa msingi huo, nashauri utafiti zaidi uendelee kufanywa kuhusiana na historia ya Uislamu hapa Zanzibar na fani mbalimbali zinazohusiana na utamaduni wa kiislamu ili tuweze kubaini mwaka halisi ambapo Uislamu uliingia Zanzibar na namna ulivyoingia” Dk. Shein alisisitiza.
Kuhusu mchango wa Zanzibar katika kukuza na kueneza ustaarabu wa kiislamu katika maeneo ya Afrika Mashariki Dk. Shein alieleza “masheikh na maulamaa mbalimbali wa Zanzibar walikwenda kueneza uislamu katika maeneo mengine kama vile Tanzania bara, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na wengine walifika Komoro na  baadhi ya nchi nyingine za Afrika Kaskazini na baadhi ya nchi za Asia”.
Aliongeza kuwa wananchi wa Zanzibar wanapata faraja kuona taarifa za Zanzibar zinatumika na kuthaminiwa katika kuelezea mchango wake kwa ajili ya kuendeleza ustaarabu wa kiislamu na mafundisho ya dini hiyo katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.  
Ili kuendeleza na kuhifadhi historia ya Uislamu katika ukanda huo Rais wa Zanzibar alitoa rai kwa waandaaji wa kongamano hilo na wadau wengine kuangalia uwezekano wa kuanzisha kituo cha historia na utamaduni wa kiislamu wa kanda hiyo Zanzibar na kueleza kuwa Serikali iko tayari kutoa ushirikiano unaostahiki kufanikisha rai hiyo.
“Serikali yangu iko tayari kutoa ushirikiano wa kila hali iwapo hili (la kuanzisha kituo cha historia na utamaduni wa kiislamu) litazingatiwa na kuona umuhimu wake kwa lengo la kulitekeleza”alisema.
Katika hotuba yake hiyo Rais wa Zanzibar alitambua mchango mkubwa wa lugha ya Kiswahili katika kueneza ustaraabu na mafundisho mengine ya dini ya kiislamu.
“Lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika ikiwa kama chombo muhimu cha kueneza ustaraabu na mafundisho mengine ya dini ya kiislamu kupitia mawaidha, darsa na pia tafsiri za vitabu vya dini”alieleza na kutolea mfano tafsiri ya Quran tukufu ya Sheikh Abdalla Saleh Al- Farsi aliyewahi kuwa  Kadhi Mkuu wa Zanzibar.
Dk. Shein  aliwaeleza washiriki wa kongamano hilo kuwa matarajio ni kuona kongamano hilo linatoa mchango mkubwa na muhimu kitaaluma na kuongeza maarifa kuhusu historia ya ustaraabu wa kiislamu kwa washiriki na watu wengine ambao watapata fursa ya kufuatilia kongamano hilo.
“kwa hivyo tuhakikishe kuwa elimu hii inawafikia kwa kutambua kuwa elimu ni amana na neema waliyopewa waja kutoka mwa Mola wao na hivyo ni wajibu wao kuwafikishia wengine kama walivyofanya maulamaa na masheikh wetu mbalimbali ambao baadhi yao tumewataja”alisisitiza.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa unaotolewa na taasisi za kidini na ndio maana imeanzisha Ofisi ya Mufti kusimamia masuala ya kidini.
Dk. Shein alihimiza pia mshikamano na umoja miongoni mwa waislamu na katika kusimamia na kuendeleza dini yao kwa kuwa hawapaswi kabisa kuhasimiana hasa kwa misingi ya dini na imani.
Aliwakata wananchi wa Zanzibar kulinda ustaarabu wa kuendesha mihadhara ya kumarisha dini, kusimamia amani na umoja na mapenzi miongoni mwa waislamu kama walivyofanya viongiozi wa dini waliotangulia.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefisu uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Ufalme wa Oman.
“napenda nitambue uhusiano mzuri na udugu uliopo kati ya Serikali na wananchi wa Zanzibar na  Serikali ya Ufalme wa Oman na watu kwake ” Dk. Shein waliwaeleza washiriki wa Kongamano la Kimataifa Kuhusu Historia ya Ustaarabu wa Kiislamu Katika Afrika ya Mashariki na kumtakia kila la heri kiongozi wa Ufalme wa Oman Sultan Qaboos.  

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles