Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTPC
Wenyeviti Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania
Sekretariati ya UTPC
Wadau wa Habari Tanzania
Mabibi na Mabwana, Asalam aleykum, Tumsifu Yesu Kristu.
Leo ni mwaka mmoja kamili tangu aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Iringa Daudi Mwangosi auawe pale kijiji cha Nyororo Mufindi wakati akiwa katika kazi yake ya kuandika habari.
Familia yake na ndugu zake, IPC, UTPC na wadau wengine hawawezi kamwe kusahau mauaji ya Daudi Mwangosi kwani yalikua ni mauaji ya kinyama na ukatili wa hali ya juu.
Mpaka sasa hatujui sababu zilizo pelekea Daudi Mwangosi kuuawa, lakini tunaamini kwamba kwamba Serikali itafanya kila njia kuhakikisha wote waliohusika, hatua sitahiki zinachukuliwa.
Zipo sababu nyingi za serikali kufanya hivyo lakini kubwa ni kwamba:-
1. Niwajibu wa Serikali kuwalinda raia wake wote bila kujali itikadi zao za dini, rangi, kabila au siasa. Hivyo pale inapotokea raia wake ameua katika mazingira yasio ya kawaida serikali inawajibu wa kufanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia hatua wote waliohusika. Kwa kufanya hivyo Serikali yetu itakua inatimiza wajibu wake wa kuwalinda raia wake. Hivyo ndivyo utawala wa sheria unavyo taka.
2. Ndugu zangu wakati tunaangahikia maisha ya duniani tukumbuke kwamba, kuna maisha mengine huko Mbinguni ambako kila mmoja wetu atahesabiwa haki yake kulingana na matendo yake hapa duniani. Hivyo hata aliyemuua Daudi Mwangosi ipo siku atakufa na atawajibika kujibu kwanini alimua Daudi Mwangosi.
Tunaweza kushinda hapa duniani lakini kama hatutatenda yale yampendezae Mungu hatuwezi kushinda mbinguni hata siku mmmoja.
Ndugu zangu nalisema hili ili tukumbuke kwamba, hapa duniani tunapita tu na kama hapa tunapita ni kazi bure kuasi na kutompendeza Mungu wetu kwani maisha yetu yote mwisho wake uko huko.
Ninawaomba waandishi wenzangu, kifo cha Mwangosi kitukumbushe kwamba kuna watu wasiopenda maendeleo ya Tanzania au ya Watanzania ambao watafanya kila njia kuvuruga tasnia yetu kwa kutumia njia zozote zile ikiwa ni pamoja na kupiga waandishi, kuua waandishi na kufanya kila wawezalo ilimradi tu waandishi tusiweze kufanya kazi zetu vizuri.
Ninawaomba waandishi wenzangu, kama waandishi tubaki kuwa sauti ya watu wote, wana siasa, na wasio wanasiasa, wenye dini na wasio na dini, wenye nacho na wasio nacho, masikini na matajiri sisi ni wa wote na nilazima tubaki hivyo. Katika kufanya kazi yetu hii jamii lazima ituelewe hivyo. Tukiweza kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi yetu bila ya kuegemea upande wowote ule tutaifanya kazi yetu kuwa nyepesi sana, Lakini lililo la muhimu sana kwa leo niwakumbushe ndugu zangu kuweka USALAMA WETU MBELE KULIKO KITU KINGINE CHOCHOTE. KWANI HAKUNA HABARI YENYE THAMANI SAWA NA UHAI WAKO.
UTPC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na Wafadhili tunajiandaa kuwajengeeni uwezo wa kutathimini mazingira mnayofanyia kazi na hivyo kuweza kufanya uamuzi sahihi wa namna ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi. Wakati tunajianda kufanya haya, tukumbuke kwamba katika kila jambo tukiwa na balance na kufuata maadili, jamii itasimama na sisi hata pale tutakapo onewa na wasio penda maaendeleo ya Tanzania. Watu wanaodhani kwamba wanaweza kushinda duniani na mbinguni.
Mwisho tumuombe ndugu yetu Daudi Mwangosi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.Amina
Kenny Simbaya
Rais UTPC