Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya pamoja na Madaktari wa Jamhuri ya Uturuki mara baada ya kuwashukuru kufuatia kukamilisha mpango wao wa kutoa huduma mbali mbali za afya ukiwemo upasuaji hapa Zanzibar
Mdhamini wa Madaktari wa Uturuki waliokuwa wakitoa huduma za Afya hapa Zanzibar Profesa Murat Tuncer wa Chuo Kikuu cha Hacettepe Nchini Uturuki akiagana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada kukutano na madaktari hao katika ukumbi mdogo wa Jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.Na Othman Khamis Ame, OMPR
Mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Jamuhuri ya Uturuki katika kusaidia Sekta ya Afya Zanzibar umesaidia kuipunguzia mzigo mkubwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwahudumia Wananchi wake hasa wale wanaohitaji kusafirisha kwa ajili ya matibabu zaidi ya kitaalamu nje ya Nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiwashukuru Madaktari 45 na Maprofesa watano wa Jamuhuri ya Uturuki waliokuwepo Nchini kutoa huduma mbali mbali za afya ikiwemo upasuaji alipozungumza nao katika ukumbi mdogo wa Jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema ziara za kila mwaka kwa timu za madaktari wa Uturuki wanaokuja kujitolea Zanzibar katika sekta ya afya zimeleta faraja na upendo baina ya watu wa Uturuki na Zanzibar hali ambayo alieleza kwamba inapaswa kuimarishwa na kuenziwa zaidi.
Alifahamisha kwamba mpango wa Madaktari hao kupitia taasisi zao za misaada za kutoa msaada wa vyandarua 8,000 pamoja na usomeshwaji wa wazanzibari wapatao 86 tokea kuanza kwa mpango huo mwaka 2007 umetoa picha halisi kwa taasisi hizo jinsi zilivyokubali kujitolea kusaidia huduma za Kibinaadamu hapa Nchini.
“ Tunafurahi kuona kwamba msaada wenu huu wa vyandarua umekuja wakati muwafaka kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko katika mpango wa kumaliza kabisa maradhi ya malaria Nchini ambayo hivi sasa yamepunguwa kwa hatua kubwa sana “. Alieleza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Uturuki kupitia Taasisi zake za Misaada ya maendeleo ya vyuo Vikuu kwa jitihada zake inazochukuwa za kusaidia huduma za kijamii kwa mataifa rafiki ikiwemo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
“ Wapo wataalamu wetu wengi wa fani ya afya waliowahi kupata mafunzo yao ya juu nchini Uturuki hatua ambayo kwa kiasi kikubwa inaendelea kuipunguzia mzigo kubwa Serikali kwa kumsafirisha mgonjwa nje ya Zanzibar kwa matibabu ambao wengi kati yao hivi sasa wanayapata hapa hapa Nchini “. Alifafanua Balozi Seif.
Naye Kiongozi wa Madaktari hao kutoka Chuo Kikuu cha Fatih kinachoshughulikia masuala ya matibabu na utafiti kutoka Jamuhuri ya Uturuki Profesa Mkuu wa Upasuaji Omer Faruk Akinci alisema tatizo kubwa la Jamii linaloleta fadhaa na hatimae kutumbuka kwa maradhi tofauti ni msongamano wa mawazo yasiyokwisha.
Profesa Omer Faruk alisema kitu pekee kitakachoisaidia jamii popote pale katika kupunguza wimbi hilo la mawazo ni kwa wana jamii wenyewe kuelekeza nguvu zao zaidi katika kujipatia taaluma ambayo ndio mkombozi wa yote.
Wakitoa salamu katika kikao hicho wadhamini wa Madaktari hao wa Uturuki Profesa Seif Ali Tekalan kutoka Chuo Kikuu cha Fatih na Profesa MuratTuncer wa Chuo Kikuu cha Hacettepe Nchini humo walisema vyuo vyao hivi sasa vina jumla ya wafanuzi 25 wanaosomea fani tofauti kutoka Tanzania Bara pamoja na Zanzibar.
Walisema wakati Taasisi zao zimejikita zaidi katika kuimarisha sekta ya elimu kuanzia skuli hadi vyuo vikuu zimelenga kuongeza zaidi idadi ya viwango vya wanafunzi wanaotoka Tanzania.
Wametoa mwaliko kwa wanafunzi wa Tanzania kushiriki katika mashindano yatakayoandaliwa na vyuo vikuu hivyo hapo baadae katika masuala ya elimu yakijikita zaidi kwenyea masuala ya Utamaduni.
Mapema Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji alisema ushirikiano uliopo kati ya wananchi wa Mataifa ya Jamuhuri ya Uturuki na Zanzibar ni dalili nzuri ya uhusiano mwema kati ya pande hizo mbili.
Waziri Juma Duni Haji alishauri dalili hiyo nzuri ya uhusiano inapaswa kuendelea kuenziwa na kuimarishwa kwa ustawi wa vizazi vijavyo vya pande zote mbili rafiki.
Madaktari hao wa Jamuhuri ya Uturuki walipata fursa ya kutoa huduma mbali mbali za afya katika hospitali za Mnazi Mmoja, Nungwi, Kitope, Kivunge, Makunduchi kwa unguja na Chake chake wete, Mkoani na Vitongoji kwa Pemba.
Serikali ya Jamuhuri ya Uturuki kupitia Taasisi zake za vyuo vikuu vya mambo ya Afya imekuwa ikitoa msaada wa kiafya kwa kuwashirikisha madaktari wake wanaojitolea kuja kufanya kazi hapa Zanzibar kwenye mpango wake maalum ulioasisiwa tokea mwaka 2007.