Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Mmiliki wa Hoteli ya Sun Set Bungalows iliyoko katika Kijiji cha Kendwa Nungwi Abdulsamad Ahmed Said akikagua athari iliyosababishwa na moto mkubwa uliyoyakumba baadhi ya majengo ya Hoteli hiyo juzi jioni.
Pembeni yao aliyevaa kofia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” Machano Fadhil Machano { Babla } na Nyuma yao aliyevaa suti za Bahari ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Pembe Juma Khamis akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hali halisi ya moto ulivyoikumba Hoteli ya White Sand iliyoko Kendwa Nungwi Mkoani humo juzi jioni.Baadhi ya Majengo ya Hoteli ya White Sand iliyopo pembezoni mwa Bahari ya Hindi katika Kijiji cha Kendwa Nungwi ikiwa ni miongoni mwa majengo 10 ya hoteli hiyo yaliyoteketea kwa moto mapaa yake juzi jioni.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.Na Othman Khamis Ame, OMPR
Hasara ya zaidi ya Shilingi Bilioni Moja Nukta 2 imepatikana kufuatia kuungua kwa moto hoteli mbili za Kitalii za White Sand na Sun Set Bungalows ziliopo katika Kijiji cha Kendwa Nungwi Wilaya ya Kaskazini “ A” Mkoa wa Kaskazini Unguja juzi majira ya saa 11.00 za jioni.
Hoteli ya Sun Set Bungalows inakadiriwa kupata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni mia 400,000,000/- wakati ile ya White Sand iliyoungua zaidi kutokana na moto huo inakadiriwa hasara ya zaidi ya shilingi Milioni mia 800,000,000/-.
Moto huo ulisababishwa na hitilafu za umeme katika moja ya majengo ya Hoteli ya Sun Set Bungalows iliyoezekwa makuti na kutoa cheche za moto zilizosambaa kwa haraka katika baadhi ya majengo mengine kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma katika eneo hilo.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitokea Bungeni Mjini Dodoma alifika eneo hilo la tokeo ili kuwafariji Wamiliki, Wafanyakazi wa Hoteli hizo pamoja na Wananachi wanaozizunguuka Hoteli hizo kutokana na maafa hayo makubwa kwa uchumi wa Taifa.
Akitoa ufafanuzi wa mkasa halizi wa tukio hilo Mmiliki wa Hoteli ya Sun Set Bungalows Abdullsamad Ahmed Said alimueleza Balozi Seif kwamba Moto huo umevikumba vyumba Vinane vya kulala wageni, Stoo pamoja na jiko la kupikia.
Abdullsamad alisema Wageni wapatao sabini waliokuwemo kwenye vyumba vya Hoteli hiyo waliweza kuokolewa kwa ushirikiano kati ya Wafanyakazi wa Hoteli hiyo na Wananchi walioizunguuka Hoteli hiyo jambo ambalo lilileta faraja kwa Uongozi pamoja na wafanyakazi wake.
Mmiliki huyo wa Hoteli ya Sun Set Bungalows aliwashukuru wananchi hao, Viongozi wa Serikali Wilaya na Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na Maafisa wa Kamisheni ya Utalii kwa msaada wao ulichangia kupunguza machungu ya janga hilo.
Balozi Seif Ali Iddi akikagua hali ya tukio la moto huo ambao pia uliathiri Hoteli nyengine ya jirani ya White Sand ambapo Mmoja miongoni mwa Viongozi wa Hoteli hiyo Ramadhan Msanif alimfahamisha Balozi Seif kwamba wakati wakijiandaa kutoa msaada kwa wenzao jirani wa Sun Set cheche za moto huo pia zikaanza kuvamia Hoteli yao na kulazimika kukabiliana nalo.
Bwana Msanif alisema licha ya juhudi walizochukua kukabiliana na moto huo lakini kasi kubwa ya upepo uliokuwa ukivuma wakati huo ulisababisha kuathiri mapaa ya nyumba 10 za hoteli hiyo katika kipindi kifupi kwa vile zilikuwa na mapaa ya makuti.
Akizungumza na Viongozi, Wafanyakazi wa Hoateli hizo pamoja na Wananchi wa jirani na Hoteli hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitoa wito kwa wananchi kuendelea kusaidia wawekezaji wakati yanapotokea majanga kwenye maeneo ya vitega uchumi.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inasisitiza na kutegemea sekta ya Utalii ambayo kwa sasa inasaidia kuongeza mapato ya Taifa sambamba na kutoa ajira kwa wananachi wanaovizunguuka vitega uchumi hivyo.
Hata Hivyo Balozi Seif aliendelea kuwakumbusha wawekezaji vitega uchumi mbali mbali Nchini kujenga utamaduni wa kuiwekeza Bima Miradi yao ili wakati wanapopatwa na majanga au maafa Bima hizo ziweze kuwasaidia.
Alisema inasikitisha kuona ipo miradi ya kiwango kikubwa cha fedha inayoendelea kuwekezwa Nchini lakini wamiliki wengi wa miradi hiyo wanashinda kuikatia bima na hatiame inakufa kabisa pale inapokumbwa na majanga kama ya moto.
“ Wawekezaji na hata Wafanyabiasharawengi bado wamekuwa wazito kuiwekea Bima miradi yao na kusahau kwa kuona ghali mpango huo ambao kumbe huwa unawasaidia wakati wanapopatwa na majanga “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi waliopo jirani na Hoteli hizo kwa juhudi kubwa waliyochukuwa na kusababisha kupungua kwa hasara kubwa iliyokuwa izikumbe hoteli hizo.
Alisema juhudi hizo zilizowaongezea nguvu za uokozi wafanyakazi wa hoteli hizo zimesaidia kuokoa mali na vifaa vya hoteli pamoja na wageni waliokuwa wakipata huduma ndani ya Hoteli hizo.
“ Nafarajika kusikia kwamba harakati za uokozi wa mali na vifaa katika Hoteli hizi mbili za White Sand na Sun Set Bungalows za Kendwa hakukuwa na ripoti za udokozi wa mali kama zilivyotokea Kwenye Hoteli ya Paradise Beach Resort iliyopo Marumbi wakati ilipowaka moto wiki moja na nusu iliyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Hoteli hizo kufikiria kubadilika katika mfumo wa ujenzi wa mapaa ya makuti ili kujilinda na majanga yanayoweza kuepukwa licha ya kwamba mfumo huo hutoa ajira kwa wananchi wanaouza makuti yao.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliangalia eneo lililopembezoni mwa Bara bara mbele ya Skuli ya Msingi na Sekondari ya Mto Pepo ambalo liko katika hali mbaya kimazingira.
Ziara hiyo ya ghafla ya Balozi Seif ilikuja kufuatia baadhi ya wananchi kufanya Biashara katika eneo hilo linalotishia afya za Binaadamu kutokana na kutuwama kwa maji machafu yanayoweza kusababisha maradhi ya kuambukiza.
Katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuagiza Sheha wa Shehia ya Mto Pepo pamoja na Diwani wa Wadi ya eneo hilo kufika Ofisini kwake Vuga Jumatatu ya Tarehe 9 Septemba asubuhi kulijadili suala hilo.
Hali ya mazingira ya eneo hilo mbali ya kutoa sura mbaya kwa wapita njia na wageni lakini pia inaweza kusababisha mripuko wa maradhi hasa kwa wanafunzi wadogo wasiozingatia afya zao wa Skuli ya jirani na eneo hilo.