Mkuu wa Chuo cha Dilpomasia Jijini Dar es salaam Balozi Dr. Mohammed Maundi yeye na ujumbe wake akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi juu ya mfumo wa kuanzisha mafunzo ya Uhusiano wa Kimataifa kwenye chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar
Balozi Seif akisisitiza jambo juu ya mfumo wa kuanzishwa kwa mafunzo ya Diplomasia kwenye chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar.
Kulia yake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Utumishi wa Umma Zanzibar Nd. Yakout Hassan Yakout
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifurahia wazo lake alilolitoa la kuazishwa ushirikiano wa mafunzo ya Diplomasia kwenye chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar wakati akizungumza na Uongozi wa pande hizo mbili hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Uongozi wa Chuo cha Diplomasia Cha Jijini Dar es salaam umepongezwa kwa hatua zake ulizoanza kuzichukuza katika harakati za kusaidia Taaluma ya masuala ya Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Balozi Seif alitoa pongezi hizo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Uongozi wa Chuo cha Diplomasia ukiongozwa na Mkuu wa chuo hicho Balozi Dr. Mohammed Maundi uliofika Zanzibar kwa hatua za awali za namna ya kuanza mpango huo.
Balozi Seif ambae aliwahi kutoa ombi hilo wakati akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya Tano ya chuo cha Utawala wa umma Machi 30 mwaka huu huko Tunguu alisema taamula hiyo inaweza kusaidia wanafunzi hao wakati wanapoamua kuendelea na mafunzo yao katika ngazi za Kimataifa.
Alifahamisha kwamba Dunia hivi sasa ina mfumo wa mazingira ya kutegemeana hivyo ni vyema kwa watumishi wa umma pamoja na wana jamii wakaanza utaratibu wa kujipatia taaluma inayofanana na mazingira hayo ya Ushirikiano wa Kimataifa.
“ Nimefurahi na kushukuru kuona kwamba lile wazo langu nililolitoa kwenye mahafali ya chuo cha utawama wa Umma Zanzibar Mapema mwaka huu limeanza kutoa matumaini mazuri ambayo kwa kweli yananipa moyo mkubwa “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa taaluma hiyo ikienea zaidi miongoni mwa jamii italenga kukomaza mfumo wa uhusiano wa Kidiplomasia hapa Nchini.
Naye Mkuu wa Chuo cha Diplomasia cha Mjini Dar es salaam Balozi Dr. Mohammed Maundi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa chuo hicho unajiandaa kuleta wataalamu Zanzibar ili kuangalia na kuona hatua za pamoja za kuchukuliwa katika muelekeo wa pamoja na chuo cha Utumishi wa Umma wa kuanzisha mitaala ya mafunzo ya Diplomasia.
Balozi Maundi alisema ipo haja ya kubadilishana mihula ya wanafunzi kati ya vyuo hivyo ili kuongeza ushirikiano kati ya wana taaluma wa Chuo cha Diplomasia Dar es salaam na wale waChuo cha Utawala wa Umma hapa Zanzibar.
“ Tunaweza kuanzisha mafunzo ya pamoja miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vyote viwili. Hii itasaidia pande zote husika kwa vile uwezo wa walimu wetu unaweza kutumiwa na pande zote mbili “. Alifafanua Balozi Maundi.
Alisema chuo cha Diplomasia hivi sasa kiko katika mchakato wa kuanzisha kiwango cha Digirii ya kwanza kufuatia ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoomba kujiunga na chuo hicho ambao wengi wao wanatokea Visiwani Zanzibar.
Mkuu huyo wa Chuo cha Diplomasia anayehusika zaidi na fani ya usuluhishi katika migogoro ya rasimlali asilia Balozi Maundi alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa wazo lake lenye mustakabali wa kuwajengea uwezo zaidi wa kitaaluma wanafunzi wa Zanzibar