Na Haji Nassor, Pemba
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mtoto mmoja amezaliwa huku sehemu zake za macho zikiwa hazionekani.
Mtoto huyo wa kike mwenye umri wa siku moja, amezaliwa usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Chake Chake kisiwani Pemba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, daktari wa macho katika hospitali hiyo, Ali Rashid, alisema kutokana na hali hiyo itakuwa vigumu mtoto huyo kufanyiwa upasuaji na ni dhahiri kwamba hataweza kuona katika maisha yake yote.
Alisema macho ya mtoto huyo kwa juu, yanaonekana kama kawaida na kuwepo kwa alama za mpasuko, ingawa ni vigumu kuona kiini chake cha ndani.
Alisema unapotaka kuona kiini cha ndani inabidi utumie nguvu za ziada, jambo linaloashiria kuwa mfumo wake wa kuona umeharibika.
‘’Kwa kweli hayawezi kutibika, pengine iwe kuna teknolojia mpya na kubwa kwa nchi zilizoendelea ndio inawezekana, lakini kwa haraka ameshapata upofu,” alisema.
Alisema hiyo ni kesi ya pili kuripotiwa, ambapo kesi ya kwanza iliripotiwa hospitali ya Vitongoji takribani miaka 10 iliyopita.
Alitaja sababu zinazosababisha tatizo hilo kuwa ni pamoja na mama mjamzito kukosa madini mwili na ukosefu wa kula matunda wakati wa ujauzito.
“Kuna vitu mbali mbali mjamzito akivikosa anaweza kuzaa mtoto akiwa katika mazingira kama haya, wala sio kesi ya urithi,” alisema.
Alimtaka mama wa mtoto huyo kumfikisha tena mwanawe hospitali hapo Septemba 26 mwaka huu, ili akutane na madaktari bingwa wa macho.
Mama wa mtoto huyo Mgeni Khalifa Simai (25) ambae hiyo ni mimba yake ya nne, alisema akipata maumivu makali wakati akiwa na ujauzito wa miezi minne.
Alisema wakati alipokuwa akihudhuria kliniki kituo cha afya Chonga Wilaya ya Chake Chake, alielezwa na wataalamu kuwa fuko lake la uzazi, limeshuka na kutakiwa kuacha kufanya kazi ngumu.
Alisema aliacha kufanya kazi nzito, hadi alipojifungua salama, na mwanawe huyo akiwa na uzito wa kilo 3.4.
Badhi ya wanawake wenzake waliolazwa katika hospitali hiyo pamoja, walisema kukosa macho sio mwisho wa maisha na kumtaka mama huyo kumtunza vyema mtoto wake kwani huo ni mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu.