Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein: Mapambano dhidi ya ukimwi yaende sambamba na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya

$
0
0
 
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema jitihada za kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI nchini hazina budi ziende sambamba na vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine ambavyo ni miongoni mwa vyanzo vya ugonjwa huo.
 
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Kituo cha Jamii na Watoto huko Welezo Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo Dk. Shein amesema imebainika kuwa maambukizi mapya ya virusi vya ugonjwa huo kwa vijana yanahusishwa na matumzi ya madawa ya kulevya.
 
“Katika miaka ya hivi karibuni imebainika kuwa maambukizi mapya ya UKIMWI yanawakumba zaidi vijana wanaotumia dawa za kulevya hapa nchini” Dk. Shein alieleza.
 
Kituo hicho kimejengwa na Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ugonjwa wa UKIMWI Zanzibar ZAPHA+ kwa msaada wa taasisi ya Stephen Lewis Foundation ya Canada ambayo ilichangia shilingi milioni 43.65 ambazo ni sawa na asilimia 40.45
 
Kwa hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali na washirika wengine katika mapambano dhidi ya maambukizi ya UKIMWI na dawa za kulevya kuiokoa jamii hasa vijana ambao ni tegemeo la taifa.
 
Dk. Shein amewaeleza wanachama wa ZAPHA+, wananchi na wageni waliohudhuria hafla hiyo kuwa tangu ugonjwa huo ulipogunduliwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikifanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha Zanzibar haipati maambukizi mapya na pia kuondosha unyanyapaa dhidi ya watu walioathirika na ugonjwa huo.
 
“...Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua hatua mbali mbali ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na Zanzibar isiyokuwa na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI, isiyokuwa na unyanyapaa wala ubaguzi unaotokana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI” Dk. Shein alieleza.
 
Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuunda taasisi za kuratibu na kushughulikia mapambano dhidi ya ugonjwa huo, kushiriki katika kutekeleza sera, mipango, na mikakati mbalimbali kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika mapambano hayo.

Kwa hiyo ametoa wito kwa wananchi kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kuzingatia utekelezaji wa mipango iliwekwa na Serikali kwa kushirikiana na sekta zisizokuwa za Serikali.
 
Kuhusu huduma na tiba kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ameeleza kuwa zimeendelea kuimarishwa kwa kuongeza vituo vya huduma na tiba hadi kufikia vituo kumi kutoka kituo kimoja mwaka 2005.
 
“...dawa za ARV zimekuwa zikipatikana katika vituo mbalimbali bila malipo...huku serikali imeimarisha huduma za uchunguzi wa maradhi ili kuongeza ufanisi katika kukabiliana na janga hili” Dk. Shein alibainisha.
 
Dk. Shein ameupongeza uongozi wa ZAPHA+ na wanachama wake kwa jitihada zao hadi kuweza kujenga jengo hilo ambalo litawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo. 
 
Akizungumzia kuendelea kupungua kwa misaada ya wafadhili kwa shughuli za UKIMWI Dk. Shein ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutafuta namna bora ya kusaidiana na taasisi kama ZAPHA+ ili kutekeleza majukumu ya mapambano dhidi ya UKIMWI.
 
Hata hivyo ametoa wito kwa uongozi wa ZAPHA+ kutafuta njia za kujiongezea mapato kwa kubuni miradi ikiwemo ya kujitegemea. 
  
Amewataka wananchi kutumia fursa ya kuwepo kwa jumuiya hiyo kwa kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu maradhi ya UKIMWI kwa manufaa yao binafsi na pia kama sehemu ya jitihada za pamoja kupambana na maradhi hayo nchini.
 
Rais alitumia fursa hiyo kuwashukuru watu na taasisi mbali mbali ambazo zimekuwa zikisaidia Zanzibar katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI tangu kugundulika kwake hapa Zanzibar miaka 27 iliyopita.
 
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Afya Juma Duni Haji,Mkuu wa Mkoa Mjini Maghribi Abdalla Mwinyi Khamis na washirika mbalimbali wanaounga mkono mapambano dhidi ya UKIMWI yakiwemo Mashirika ya Kimataifa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>